Kilimo ikolojia ni njia ya kilimo inayolenga kuhifadhi mazingira, kuhimiza uendelevu, na kukuza ustawi wa jamii kwa kuzingatia mifumo ya ikolojia na utamaduni wa eneo husika. Ni mfumo ambao unazingatia uhusiano wa karibu kati ya mimea, wanyama, binadamu, na mazingira yao, na kujaribu kuiga mifumo ya asili ili kudumisha bioanuai na kuzuia uharibifu wa mazingira.
Kanuni na vipengele 13 vya kilimo ikolojia
1.Ushiriki: Kuhamasisha wakulima na wadau wengine kushiriki katika usimamizi wa mifumo ya kilimo na chakula, huku wakitoa maoni yao na kuchangia maamuzi yanayowahusu.
2.Utawala wa wa ardhi na rasimali: Kulinda rasilimali asilia na kusaidia usimamizi endelevu unaofanywa na wakulima wadogo ili kuhifadhi mazingira na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali.
3.Umoja na mfumo wa usambazaji: Kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji na watumiaji wa bidhaa za kilimo, na kuirudisha mifumo ya chakula katika uchumi wa ndani wa jamii husika ili kusaidia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
4.Uumbaji wa maarifa kwa pamoja: Kukuza ushirikiano na kubadilishana maarifa ya kilimo na uvumbuzi wa kisayansi ili kuboresha njia za kilimo na kukuza tija.
- Thamani za kijamii na lishe: Kupigania mifumo ya chakula inayoheshimu tamaduni na maadili ya jamii za eneo husika, na kuhakikisha upatikanaji wa vyakula vinavyofaa kiafya na vyenye kulinda utu.
6.Uadilifu: Kusimamia mifumo ya kilimo yenye usawa na haki, na kuhakikisha kuwa wote wanaochangia katika mfumo wa kilimo ikolojia wanapata faida na haki zinazostahili.
7.Utofautishaji wa kiuchumi: Kukuza uwezo wa kifedha miongoni mwa wakulima wadogo ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa kanuni za kilimo ikolojia na kuboresha maisha yao.
8.Bioanuai: Kuhakikisha kuwepo kwa utofauti wa kimaumbile wa mimea na wanyama katika mazingira ya kilimo ili kudumisha usawa na kuboresha mazingira ya uzalishaji wa chakula.
9.Afya na ustawi wa wanyama: Kulinda na kuhakikisha ustawi wa wanyama wote wanaohusishwa na mifumo ya kilimo ikolojia, kwa kuzingatia heshima na mahitaji yao asili.
- Afya ya udongo: Kudumisha afya ya udongo kama msingi wa uzalishaji wa chakula na afya ya mazingira, kwa kuhimiza mbinu za kilimo zinazozingatia udhibiti wa ardhi na uhifadhi wa udongo.
- Mwingiliano: Kukuza mifumo ya kilimo ambayo inaunganisha vizuri mimea, wanyama, maji, udongo, na miti katika mazingira ya ushirikiano, kwa lengo la kudumisha utendaji bora na uthabiti wa mifumo ya kilimo ikolojia.
- Ufanisi wa rasilimali: Kukuza matumizi endelevu ya rasilimali na mbinu za kilimo zinazosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuhifadhi rasilimali za asili.
- Kupunguza matumizi ya pembejeo: Kupunguza utegemezi kwa rasilimali za nje kama vile mbolea za viwandani, dawa za kemikali, na nguvu kazi kutoka kwa vyanzo visivyosaidia mazingira, kwa kuzingatia mbinu za kilimo zinazohimiza utumiaji wa rasilimali za ndani na kuzalisha taka kidogo. Kanuni hizi za kilimo ikolojia zinatafuta kuleta mabadiliko ya kimfumo katika njia za uzalishaji wa chakula, kwa lengo la kusaidia mazingira na kuhakikisha ustawi wa jamii za vijijini kwa vizazi vijavyo.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Paul Chilewa kutoka TOAM kwa simu namba 0756950273