Katika zama za kale, beetroot (kiazi sukari/ bitiruti) ilikuwa ikitumika kama dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali kama kuvimbiwa, majeraha pamoja na matatizo mbalimbali ya ngozi (mizizi ndiyo iliyokuwa ikitumika).
Hadi kufikia karne ya 16 zao hili lilikuwa tayari limekwishapata umaarufu hasa katika Amerika ya Kati na Ulaya ya Mashariki na baadaye kupokelewa katika nchi zingine kama Roma, Ufaransa, Poland,USA, Russia na ujerumani huku ikija kwa maumbile tofauti na rangi tofauti pia.
Matumizi ya zao hili yaliendelea kuongezeka (ikiwa ni pamoja na kulimwa kwa ajili ya chakula) hivyo kulifanya kulimwa kwa wingi katika nchi mbalimbali dunia ikiwa ni pamoja na nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Aina za beetroot
Kuna aina mbalimbali za beetroot kama nyekundu, nyekundu yenye mistari meupe kwa ndani, pamoja na nyeupe. Hata hivyo, beetroot nyekundu ndiyo inayolimwa kwa wingi hapa nchini.
Aina zote hizi huweza kuliwa majani na mizizi pia. Hata hivyo kutokana na kiwango cha sukari inayopatikana, huwa na ladha zaidi kama ikiliwa mbichi.
Matumizi
Zao hili lenye madini ya foliate, chuma, magnesiamu, vitamini C na potasiamu lina matumizi mengi kwa binadamu na hata kwa wanyama.
- Beetroot hutumika kama chakula au kiungo kama vile karoti kwa ajili ya kuongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali.
- Zao hili pia hutumika kutengenezea juisi. Unaweza kutumia beetroot pekee au ukachanganya na matunda mengine.
- Huongeza damu mwilini pamoja na kuupa mwili nguvu na kusaidia kuboresha kumbukumbu.
- Ni dawa na hutumika kutibu ugonjwa wa sukari, kuvimbiwa, majeraha na magonjwa ya ngozi.
- Zao hili pia majani yake huweza kutumiwa kama lishe kwa ajili ya kulishia mifugo wa aina yeyote.
Udongo
Zao hili hufaa zaidi kulimwa katika udongo wa tifutifu na wenye rutuba ya kutosha (loam soil). Halifai kulima katika udongo wa mfinyanzi. Ikiwa shamba halina rutuba ya kutosha basi ni vyema kuweka mbolea ya mboji katika shamba kabla ya kuotesha.
Hali ya hewa
Zao hili hufaa zaidi kulimwa katika hali ya baridi kidogo (cool temperature) hasa nyuzi joto 18˚C hadi 27˚C
Uandaaji wa shamba
Kutokana na kuwa zao hili huoteshwa ama kusiwa moja kwa moja shambani, mkulima ni lazima kuandaa shamba mapema sana mara tu anapohitaji kufanya hivyo.
- Ili kurutubisha udongo na kupata mavuno mengi, weka mbolea ya samadi iliyoiva ama mboji shambani kabla ya kulima. Hii itasaidia udongo na mbolea kuchanganyika vizuri wakati wa kulima.
- Tengeneza matuta katika shamba zima. Kitaalamu, matuta ya kunyanyua ni mazuri zaidi katika kilimo cha kumwagilia hasa kwa zao la bustani kama hili. Matuta haya husaidia maji kupenya ardhini na kuruhusu mizizi kupata maji ya kutosha huku mmea ukitanuka vizuri na kujitengenezea chakula.
- Mwagilia matuta yale kwa kuweka maji ya kutosha, tayari kwa kuotesha siku ya pili.
Namna ya kuotesha.
Kumbuka, kwa kila ekari moja, waweza kutumia mbegu za beetroot kiasi cha gramu 50 na kwa kutumia vipimo sahihi utakuwa na jumla ya mimea 108000.
Otesha mbegu katika mistari kwenye matuta huku ukihakikisha kuna nafasi ya kutosha kati ya mstari na mstari na kati ya mche na mche.
Baada ya kuotesha, mbegu zitachipua baada ya siku 10 (wiki na zaidi).
Nafasi
Ni vizuri zaidi ukatengeneza matuta yenye upana wa sentimeta 150 kila moja na katika kila tuta weka mistari minne ya beetroot.
- Nafasi kati ya mche na mche iwe ni sentimeta 10
- Mstari na mstari iwe ni sentimeta 15
Umwagiliaji.
Baada ya miche kuchipua, anza kumwagilia katika wiki ya pili. Mwagilia kila wiki mara moja au mbili kulingana na ukavu wa shamba. Zao hili halihitaji maji mengi kwani kutasababisha fangasi pamoja na kuoza kwa kiazi hivyo usimwagilie kila wakati.
Palizi.
Ni muhimu kufanya palizi kila mara unapoona majani yamechipua yaani muda wote kuanzia ukuaji hadi kuvuna. Ondoa magugu yakiwa bado machanga kwani zao hili haliwezi kuendelea kwani yana uwezo mdogo sana kushindana na magugu.
Magonjwa na wadudu
Kama ilivyo kwa mazao mengi ya bustani, zao hili pia hushambuliwa na magonjwa kama powdery mildew na down mildew na yote haya husababisha fangasi.
Aidha, wadudu kama thiripi, inzi weupe na utitiri pia ushambulia zao hili.
Namna ya kuzuia
Hakikisha unaotesha katika eneo lenye hali ya hewa inayohitajika,na kusiwe ni katika kipindi cha mvua nyingi wala usiweke maji mengi.
Ikiwa utatumia viuatilifu, basi hakikisha unapata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo.
Mavuno
Zao hili hukomaa na kuvunwa baada ya miezi mitatu (siku 90). Hata hivyo huweza kuvumilia kusubiri soko ikiwa mkulima atalazimika kufanya hivyo (huweza kukaa takribani miezi 3 toka kukomaa bila kuharibika kwa kuvuna na kuhifadhi sehemu yenye ubaridi kiasi).
Kumbuka
Kutokana na matumizi ya zao hili hasa kutumiwa kama dawa, usitumie kemikali. Ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo hai ili kulinda afya za watu.