Ulezi ni zao asili na chanzo kubwa ya virutubisho muhimu vya kujenga kinga ya mwili kwa familia. Kwa nafaka zote, Ulezi una mkusanyiko mkubwa wa madini. Kutokana na faida hii, unasoko na kuleta faida kwa mkulima.
Ulezi pia unajulikana kama wimbi ni zao ambalo limelimwa kwa karne nyingi tangu enzi za babu zetu. Linajumuishwa katika mazao yatima kwa sababu linapandwa na wakulima wachache ikilinganishwa na nafaka zingine kama mahindi, ngano, mpunga, shanyiri, mchele, mtama na uwele.
Kwa sababu hiyo, umekuwa ukikosekana mezani kwa watu wengi, huku nafasi yake ya hapo awali ikichukuliwa na chai, mkate, soseji, na mayai. Hata hivyo, zao hili limepata sifa na kutambuliwa kwa sababu za faida zake nyingi za kiafya ambazo zinaweza kuzuia shida nyingi za lishe na magonjwa yanayohusiana na vyakula vya kisasa na mitindo ya maisha.
Virutubisho ndani ya mbegu
Mbegu ya ulezi haina gluteni na imejaa vitamini na madini. Chakula kisicho na gluteni kimsingi hutumiwa kuzuia na kudhibiti magonjwa yanayoshambulia kinga ya mwili. Gluteni hupatikana kwenye nafaka kama ngano na shayiri.
Ulezi imethibitishwa kujaa virutubisho na madini mengine yanayo hitajika na mwili. Haya ni pamoja na:
- Magnesiamu – husaidia kupunguza maumivu makali ya kichwa, shinikizo la damu na mstuko wa moyo.
- Kalsiamu na potasiamu – Kwa nafaka zote, ulezi una kiwango cha juu zaidi cha kalsiamu na potasiamu. Kalsiamu ni muhimu katika kujenga na kudumisha mifupa yenye nguvu, moyo, misuli na mishipa. Potasiamu ni muhimu katika kuzuia kiharusi, matatizo ya moyo na figo, wasiwasi na mafadhaiko, na kuimarisha usawa wa maji na mfumo wa neva.
- Niacin (vitamini B3), husaidia kupunguza lehemu.
- Fosforasi husaidia mwili kusaga na kutaumia mafuta, ukarabati wa tishu za mwili na kutengeneza nguvu mwilini.
- Nyuzinyuzi hulinda mwili katika mmengenyo wa chakula.
- Dawa za kemikali kama phytic asidi hupunguza lehemu, wakati phytate, inahusishwa na saratani iliyopunguzwa.
- Protini: ina amino asidi muhimu, ambayo hutumiwa kujenga mwili.
Ni muhimu kuyataja madini na virutubisho hivi ili kuonyesha umuhimu na jukumu kubwa la ulezi katika afya ya familia, zaidi kwa watoto, mama wajawazito na hasa wakati ambapo kuna haja ya kujenga kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.
Matumizi
Ulezi unatumika katika utengenezaji wa michanganyiko ya chakula na nafaka za kiamsha kinywa kwa watoto na wagonjwa. Unga wake unaweza kuchanganywa na unga wa muhogo, soya, viazi lishe, na unga wa ngano na bidhaa zingine za kuooka.
Ulezi una sifa nzuri katika utengenezaji wa pombe (ya pili baada ya shayiri) na ina uwezo mkubwa katika kutengeneza pombe za kienyeji kama busaa na bia.
Inatoa nyasi bora na masalia yake hutumiwa kama lishe kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi. Majani yanayotokana na mavuno ya nafaka ni ya thamani na yanaweza kulishwa moja kwa moja kwa mifugo au kutumiwa katika mifumo ya kukata na kubeba. Aidha, gharama ya kulisha mbegu kwa mifugo ni kubwa ikilinganishwa na nafaka zingine.
Kukuza Ulezi
Ulezi ni zao bora katika maeneo makavu ama yenye mvua kidogo na mbegu yake inaweza kukaa kwenye udongo kwa wiki mbili hadi mvua itakaponyesha.
Zao hili hustawi katika mazingira yenye mvua ya kati, kiwango cha joto cha 15°C hadi 30° C na pH ya mchanga ya 5.0 hadi 8.2. Wakati wa kukomaa kwa mbegu na kukomaa kiwango cha chini cha mvua na unyevu mdogo unahitajika.
Ulezi unaweza kupandwa pamoja na nafaka kama mtama, maharagwe na mikunde, na mazao ya mafuta kama karanga, ufuta, na mazao ya mizizi kama mihogo.
Imekuwa mazoea kupanda kwa njia ya kurushwa tu shambani. Njia ya kisasa ni kupanda kwa mistari ili kupata mavuno mengi na urahisi wa kupalilia.
Tengeneza mifereji iliyotengwa kwa urefu wa futi moja (sentimeta 30).
Kwa mifereji, weka mbegu na ufunike kwa udongo mdogo (kilo moja kwa ekari).
Fanya palizi la kwanza wiki mbili baada ya kuibuka. Fanya palizi ya pili wiki mbili baada ya palizi la kwanza na upunguze wingi wa mimea kiasi kwamba kila mmea uwe mkono moja kutoka mwingine.
Vuna mara tu mbegu inapokuwa ngumu ya kutosha. Usisubiri mazao kukauka kabisa shambani, kwani ndege wanaweza kuvuna kwa niaba yako.
Ndege ndio tishio kubwa kwa ulezi hasa ikiwa ni mkulima moja tu ama wachache ndio wanakuza katika eneo. Wakulima wanaweza kupanda wakati mmoja ili kugawana hasara inayosababishwa na ndege kula ulezi shambani.
Ulezi unatoa fursa bora kwa wakulima kupata mavuno ya uhakika haswa katika mazingira yenye mvua za kusuasua, chache, na kiwango kidogo cha rutuba katika udongo.
Usindikaji na Matumizi ya Ulezi
Ulezi kawaida husindikwa kwa kutumia njia za jadi. Uvunaji wa vidole vya ulezi zilizoiva (kichwa cha nafaka) hufanywa zaidi kwa kutumia visu.
Baada ya kuvuna, ulezi hukaushwa vizuri na kusagwa kabla ya bidhaa za ulezi kutengenezwa na kutumiwa.
Kwa sababu ya ukosefu wa habari, matumizi ya ulezi yanayojulikana ni kwaajili ya kutengeneza uji, ugali na pombe ya busaa.
Hata hivyo kuna bidhaa zingine za chakula na malisho ambazo zimetengenezwa kutokana na ulezi.
Biashara ya Ulezi
Punje la ulezi inastahimili kuoza na wadudu na hukaa muda mrefu ikihifadhiwa vizuri. Hii inaifanya kuwa chakula kizuri na chanzo cha kipato. Ikiwekwa kwenye ukavu, inaweza kuhifadhi kwa muda wa miaka mitano bila kutumia kemikali yoyote.
Mbali na uhifadhi wa muda mrefu, bei ya ulezi haibadiliki sana kulingana na misimu kama bei ya nafaka zingine. Kwa ujumla, bei ya ulezi ni mara mbili ya bei ya mahindi na mtama.