Katika kilimo, matumizi ya Molasi ni muhimu kwa kuboresha hali ya udongo, kudhibiti wadudu, kuwezesha udongo kuwa na rutuba, kurekebisha hali ya udongo na pia kupunguza matatizo kwa mimea inayopandikizwa.
Matumizi na kiasi cha kutumia
- Kuboresha umbile la udongo. Molasi husaidia kuboresha udongo na kuunganisha chembe za udongo na chembe za rutuba na viumbe hai ardhini. Ili kuwa na matokeo mazuri, Molasi ichanganywe kwenye udongo mfululizo kwa kiasi cha lita 20-25 kwa hekta kwa wiki na kipindi chote cha kumwagilia.
- Kuongeza viumbe hai kwenye udongo. Kwa ajili ya umajimaji wake, molasi inaweza kuchanganywa kwenye maji kwa urahisi. Ingawa inafanya kazi kwa muda mfupi, lakini inasababisha kuongeza uhai wa udongo. Matumizi endelevu ya molasi inaongeza viumbe hai kwa asilimia 0.5-1 kwa mwaka.
- Inasaidia kupunguza athari za wadudu kwenye udongo (nematodes)iwapo itatumika kwa muda wote wa uzalishaji. Tumia lita 20-25 kwa kiwango katika hekta moja.
- Molasi pia husaidia kwenye maeneo yenye tatizo la mchwa na wadudu wanaosafirishwa na mchwa. Kiasi cha kutumia ni kilekile cha lita 20-25 kwa hekta kwa wiki na itumike wakati wote wa kumwagilia.
- Kwa kutumia molases ina asili ya tindikali, inafanya kazi ya kusafisha mipira ya umwagiliaji, mchanganyiko wa lita 25 za molases katika kubiki mita 10 za maji.
- Kuna dalili kuwa molasi inasaidia mizizi kuwa na nguvu ya kufyonza virutubisho katika udongo hasa mizizi inapokuwa imekosa maji.
Matumizi ya molasi ni muhimu kwa sababu inafanya kazi ikiwa hai sio sawa na kemikali, na kwa sababu udongo unahitaji ili kuwezesha ukuaji wa mizizi ya mimea, kwa kuweka uwiano wa viumbe hai katika udongo na kuboresha muundo wa udongo unaoruhusu maji kusafiri bila shida.
Mizizi yenye afya huwezesha mmea kufyonza virutubisho ardhini na mmea kuwa na afya. Umbile na udongo wenye virutubisho ndio msingi wa uzalishaji bora wa mazao ya mboga na matunda.
Tumia molasi sambamba na makingo hai
Matumizi ya makingo hai ni muhimu kwa kudhibiti mimea ambayo iko hatarini kushambuliwa na wadudu na magonjwa yatokanayo na virusi vinavyosambazwa na wadudu. Wadudu aina ya kimamba wanaoruka kutafuta mimea ya kula, huongozwa na harufu.
Kimamba wanavutiwa na maeneo yaliyo kando ya barabara, kando ya mifereji au mashamba yenye mazao yaliyo na umbali wa sentimita 20.
Wanavutiwa zaidi na mimea yenye rangi hasa za njano kama alizeti.
Kutokana na tabia hizi za wadudu, kupanda mimea jamii ya nyasi inasaidia wakulima kuwadhibiti wadudu aina ya Kimamba. Kuweka mazao yenye jamii ya nyasi karibu na bustani au shamba la mboga husaidia kuwapunguza wanaoingia shambani.
Mazao gani hutengeneza kingo hai?
Mtama hutumika kama kingo hai, kwa sababu unaweza kupandwa karibu karibu. Mazao kama mahindi na nyasi pia huweza kutumika kama kingo hai.
Iwapo utatumia mahindi, kumbuka kuwa huyatengenezei kichaka hivyo unatakiwa kuyapanga kwa umbali wa sentimeta 15-20 kati ya mmea na pia kupanda mistari 5 au zaidi kwa kupishana (zigzag).
Tatizo la kuotesha mahindi kama mkingo hai ni kuwa yanaweza kutokuwa na uwezo wa kuzuia kwa kipindi mazao yakiwa shambani.
Matumizi ya nyasi pia hayaruhusiwi kwa kuwa ni zao la msimu na yanaweza kushindana na zao la msimu na kwa sababu ya ufupi hazitatoa kizuizi cha uhakika.
Jinsi ya kupanda kingo hai
Kingo zipandwe kwa upana wa mita moja. Pia zipandwe wiki moja au mbili kabla ya mazao kuoteshwa shambani, zikipandwa baada ya wakati huu, mazao ya shambani yatakuwa marefu kuliko kingo hivyo itakuwa kazi bure.
Katika eneo wazi weka vinasa wadudu vyenye dawa. Hii itakusaidia kuwanasa wadudu warukao kabla ya kuifikia mimea.
Kimamba husafirisha virusi kutoka sehemu moja hadi nyingine; Wanaposafiri na kukutana na kingo hai, hunaswa pale na kwa kubakiza virusi ambavyo hukosa uhai na kutofikia mazao shambani. Inashauriwa kung’oa mimea yote iliyoshambuliwa kabla ya mazao kutoa matunda ili kuondoa kila aina ya wadudu waliopo shambani.