Kupitia makala mbalimbali katika jarida la Mkulima Mbunifu, tumeweza kutoa elimu juu ya usindikaji wa mazao mbalimbali yatokanayo na wanyama na mimea. Hii ni kwa madhumuni ya kusaidia jamii kujifunza na kufanya kwa vitendo kisha kuongeza pato na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Katika makala hii, tunafundisha namna ya kusindika baadhi ya mazao ambayo yatatumika kama chakula, hivyo kujenga afya ya mlaji.
- Boga lishe
Boga lishe ni miongoni mwa vyakula vilivyopo katika kundi la mimea ya Cucurbitaceae au familia ya squash. Boga hili huwa na umbo la kibuyu na rangi yake huwa ni ya kijani mpauko kabla ya kukomaa na likikomaa huwa na rangi ya chungwa kwa nje na ndani.
Kwa sehemu ya nje, gamba lake huwa ngumu lakini likipikwa hulainika. Ndani ya mboga kuna mbegu ambazo pamoja na nyama ya ndani yake huliwa.
Kipande cha gramu 80 cha boga (lililochemshwa) huwa na gramu 0.5 za protini, gramu 0.2 za mafuta, gramu 1.5 za nafaka, gramu 1.4 za sukari, gramu 1.2 za faiba (nyuzinyuzi), miligramu 67 za potasiam, miligramu 764 za carotene na miligramu 6 za vitamini C.
Faida zigine za kula boga lishe ni pamoja na, kuboresha afya ya ngozi, kuboresha afya ya macho, kusaidia mfumo wa kinga ya mwili, kujenga mifupa na kusaidia kuzuia saratani.
Namna ya kusindika boga lishe
Boga lishe huweza kusindikwa na kupata unga ambao utatumika kupikia uji, ugali, supu na hata kuongeza kwenye mbogamboga kama kiambaupishi.
Hatua za usindikaji
- Chukua kiasi cha maboga unayohitaji kwa ajili ya kusindika.
- Osha maboga yote kwa maji safi na salama na hakikisha hakuna sehemu yeyote ya mboga yenye uchafu.
- Bila kumenya wala kutoa mbegu yake ya ndani, pasua kwa kutumia kisu kikali kisha kata maboga yote vipande vyembamba vidogovidogo kwa uwiano sawa.
- Vipangilie vipande vyote kimojakimoja kwenye kaushio la jua bila kuweka kipande juu ya kingine.
- Acha vikauke kiasi cha kuweza kusaga kupata unga. Yaweza kuchukua siku 5 au Zaidi kutegemeana na ukataji pamoja na hali ya hewa.
- Mara baada ya kukauka, saga vipande hivyo kupata unga kisha hifadhi kwenye mifuko maalumu ya kuhifadhia unga tayari kwa matumizi au kupeleka sokoni.
Muhimu: Unaweza pia kuchanganya na majani yake wakati wa kukausha.
Hii ni kwa kuchuma majani yalio laini, kuyamenya, kuosha na kisha kukata na kukausha pamoja kwenye kaushio la jua.
- Kiazi sukari/ kiazi chekundu
(Beetroot) Kiazi sukari ama hufahamika kama kiazi chekundu ni zao jamii ya mizizi.
Kiazi sukari hutumika kama dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali kama kuvimbiwa, majeraha, pamoja na matatizo mbalimbali ya Ngozi (mizizi ndiyo hutumika).
Hadi kufikia karne ya 16, zao hili lilikuwa tayari limekwishapata umaarufu hasa katika Amerika ya Kati na Ulaya ya Mashariki na baadaye kupokelewa katika nchi zingine kama Roma, Ufaransa, Poland, USA, Russia na Ujerumani, huku ikija kwa maumbile na rangi tofauti.
Matumizi ya zao hili yaliendelea kuongezeka (ikiwa ni pamoja na kulimwa kwa ajili ya chakula) hivyo kulifanya kulimwa kwa wingi katika nchi mbalimbali dunia ikiwa ni pamoja na nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Aina za kiazi chekundu ama kiazi sukari
Kuna aina mbalimbali za kiazi sukari kama nyekundu, nyekundu yenye mistari myeupe kwa ndani, na nyeupe. Hata hivyo, beetroot nyekundu ndiyo inayolimwa kwa wingi hapa nchini.
Matumizi
Zao hili lenye madini ya foliate, chuma, magnesiamu, vitamini C na potasiamu lina matumizi mengi kwa binadamu na hata kwa wanyama.
- Kiazi sukari hutumika kama chakula au kiungo ilivyo karoti kwa ajili ya kuongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali.
- Zao hili pia hutumika kutengenezea juisi. Unaweza kutumia kiazi sukari pekee au ukachanganya na matunda mengine.
- Huongeza damu mwilini pamoja na kuupa mwili nguvu na kusaidia kuboresha kumbukumbu.
- Ni dawa na hutumika kutibu ugonjwa wa sukari, kuvimbiwa, majeraha na magonjwa ya ngozi.
- Majani yake huweza kutumiwa kama lishe kwa ajili ya kulishia mifugo wa aina mbalimbali.
Namna ya kusindika kiazi sukari
- Chukua viazi kiasi unachohitaji kwa ajili ya kusindika, osha kwa maji safi na salama.
- Kata vipande vidogovidogo na vyembamba kwa uwiano unaolingana.
- Panga vipande hivyo kwenye kaushio la jua. Acha juani mpaka vikauke kisha saga na hifadhi kwenye mifuko ya kuhifadhia unga tayari kwa kutumia au kupeleka sokoni.
Namna ya kutumia unga kiazi sukari
Unga wa kiazi sukari hutumika kutengeneza/kukoroga juisi, kunywa kama chai, kuongeza kwenye supu au uji.
- Bamia
Bamia ni aina ya tunda mboga lenye utajiri wa virutubishi ambavyo ni muhimu sana katika mwili wa mwanadamu hasa katika usagaji wa chakula.
Faida za ulaji wa bamia
- Umeng’enyaji na uwekaji sawa wa mfumo wa sukari mwilini.
- Kulainisha choo na kuzuia kuvimbiwa.
- Kuondoa lehemu katika mishipa ya damu kwenye mwili.
- Kuwepo kwa wingi wa virutubisho vya protini ambavyo vinahitajika katika mwili wa mwanadamu.
- Wingi wa virutubisho vya vitamin A na B.
- Husaidia kuzuia kuzaliwa kwa mtoto mwenye tatizo la kupasuka kwa uti wa mgongo au kuwa na tatizo la mgongo wazi.
- Husaidia kuongeza kinga ya mwili.
- Kudhibiti matatizo ya vidonda vya tumbo.
- Husaidia kuzuia saratani ya tumbo.
Namna ya kusindika bamia
- Chuma matunda kisha yaoshe kwa maji safi na salama.
- Mara baada ya kutoa kwenye maji, anika kwa muda kidogo kuhakikisha maji yamekauka, yaani usikate bamia zikiwa bado zina maji.
- Mara baada ya kukausha, kata vipande vidogo-vidogo na vyembamba.
- Panga vipande hivyo kwenye kaushio la jua moja moja bila kuweka kipande juu ya kingine.
- Acha bamia zikauke kiasi cha kuweza kufaa kusaga.
- Saga bamia kisha hifadhi unga kwenye mifuko maalumu ya kuhifadhia tayari kwa matumizi au kupeleka sokoni.
- Unga huu ukihifadhiwa vizuri huweza kukaa kwa muda wa miaka miwili bila kuharibika.
Namna ya kutumia unga huu
Unga wa bamia hutumika kwa kutengeneza juisi, yaani kukoroga unga huu kwenye maji au kwa kuchanganya na matunda mengine.
Kwa maelezo zaidi kuhusu usindikaji wa bidhaa hizi, wasiliana na Rukia Seme kwa simu namba 0754 821 133.
Nimependa, Asante sikuwahi juwa kama bamia liñaweza kukaushwa na kuhifadhiwa
Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida letu. tunafurahi kuwa umejifunza kitukipya na utaweza kukifanyia kazi siku za usoni endapo utakuwa mkulima wa bamia