Kwa Tanzania matunda ya dragon au kama yajulikanavyo kwa kiswahili Pitaya au Pitahaya ni aina mpya.
Matunda haya asili yake ni Mexico au maeneo ya Amerika Kaskazini lakini kwa sasa yanalimwa sana bara la Asia na kwa ukanda wa Afrika Mashariki kwa sasa yanalimwa Kenya.
Kwa sababu ya kutolimwa sana Tanzania, matunda yake ni aghari huuzwa kati ya Sh 10,000/ na Sh 15,000/ kwa moja. Bei hii inatokana matunda yake kutopatikana kwa wingi hivyo iwapo litalimwa bei yake inaweza kushuka kwa kiasi Fulani hivyo kuwa rahisi kwa wengi zaidi kulitumia.
Eneo linalofaa kwa kilimo chake:
Kwa kuwa mmea huu ni jamii ya Cactus, matunda haya yanafaa kulimwa sehemu kame zisizo na maji mengi, hazipaswi kulimwa katika eneo chepechepe sababu haihitaji maji mengi kama mimea mingine.
Pitaya inaweza kulimwa na kusitawi kwenye aina yoyote ya udongo, hivyo inaweza kulimwa hata eneo lenye udongo wa changarawe hivyo ni fursa kubwa hapa nchini kwa wakulima wa maeneo mengi. Lazima ipandwe eneo lenye jua sababu huhitaji sana jua na siyo kivuli.
Pitaya hupandwa na nguzo:
Ili kukua vyema matunda haya hayawezi kupanda au kusimama bila usaidizi, hivyo ni lazima uyawekee nguzo kama ilivyo kwa zabibu, lakini nguzo zake zinapendekezwa kuwa imara zaidi sababu mimea hii hudumu kwa miaka 40.
Nguzo zinazopendekezwa ni za saruji na zinapaswa kuwa na urefu wa futi 7 na kuchimbiwa kiasi cha futi 1au 1.5 ardhini lakini juu iwe na lingi kwa ajili ya kusambaa. Ikipandwa kwenye nguzo Pitaya hustawi Kwenda juu hadi kufika mwisho wa nguzo na hapo itaanza kukua kuelekea chini hivyo inapaswa kusaidiwa kusambaa ili kuongeza matawi mengi yatakayosaidia ongezeko la matunda wakati wa kuzalisha matunda.
Kwa wale wasio na uwezo wa kuandaa nguzo za saruji wanaweza kuipanda hata juu ya mti mkubwa au kuiwekea nguzo za miti inayoweza kustahimili mchwa hivyo kudumu kwa muda mrefu. Katika nguzo moja inapendekezwa kupandwa miche minne.
Muda wa kutoa matunda:
Kuna namna mbili ya kuzipanda Pitaya, kwanza ni kwa kupanda miche ya machipukizi (Cuttings) na kwa kupanda miche ya mbegu, iwapo utaotesha mbegu zake na kupanda basi hukua hadi kukomaa na kutoa matunda ya kwanza huchukua muda wa miaka mitatu hadi minne, lakini ikipandwa machipukizi huchukua miezi 12 hadi 18 kuanza kutoa matunda.
Hata hivyo tangu inapoanza kutoa maua hadi tunda kukomaa huchukua kati ya siku 30 hadi 50. Lakini tunda lake huivia mtini hivyo inashauriwa kuvuna baada ya kuiva sababu ukichuma kabla halijaiva haliwezi kuendelea kuiva kama ilivyo papai au Chungwa.
Faida za matunda yake kwa mlaji:
Ukweli ni kwamba licha ya kuwa aghali tunda hili huendelea
kununuliwa hii ni kutokana na kuwa na faida kiafya kwa watumiaji wake.
Zifuatavyo ni sehemu ya faida za kula matunda haya;
- Lina utajiri wa virutubisho vingi mwilini
- Hulinda afya ya ngozi ya mtumiaji
- Husaidia mwili kupambana na magonjwa sugu
- Huzuia Kansa
- Huimarisha chembe hai za mwili
- Na kuimarisha kinga ya mwili.
Faida hizi mlaji anaweza kuzipata kwa kula matunda yenyewe au kwa kunywa Juisi iliyoandaliwa kutokana na matunda yake, pia linaweza kutumika kuandalia jamu na hata likikaushwa na kuandaliwa vyema linaweza hutumiaka kama Ladha mbadala katika ugandishaji maziwa mgando au uokaji wa keki.
Upatikanaji wa miche yake:
Hata hivyo licha ya kuwa linaweza kulimwa sehemu kubwa ya nchi yetu, bado tatizo lingine limekuwa ni upatikanaji wa miche yake au mbegu, kwa kutambua hali hiyo kwa sasa tumekuwa tukiotesha machipukizi kwa ajili ya kusambaza mbegu kwa watu wenye uhitaji.
Hivyo kwa wahitaji wanaweza kuwasiliana na Mwandishi wa Makala haya kwa ajili kujipatia mbegu. Simu: +255 622642620