Kila baada ya kujaza udongo katika trei moja, weka punje za mbegu kwenye kila tundu la trei, na tumia kijiti chembamba kiasi kusukumiza mbegu kuzama kwenye udongo ndani ya tundu lakini mbegu isizame sana, wala isifike katikati ya tundu bali juu kiasi na iwe imefunikwa na udongo.
Fanya hivyo kwa trei zote mpaka utakapomaliza kusia mbegu zako, tayari kwa ajili ya kukuza miche.
Eneo la kukuzia mbegu kwa siku mbili hadi saba
Andaa kichanja kitakachotosheleza kuweka na kupanga trei zote zenye mbegu mahali penye kivuli. Unaweza hata kuweka ndani chini ya uvungu, lakini kuwe ni sehemu penye utulivu na giza.
Kama ni nje, chukua nailoni nyeusi kisha tandaza juu ya kichanja na panga trei zote juu. (Hakikisha kabla ya kupanga trei juu ya kichanja, umenyunyizia maji kidogo kulowanisha udongo kwa kutumia bomba la kupiga dawa au spray pump).
Kama trei ni nyingi, weka trei kwa kupandanisha juu ya zingine, huku ukipishanisha kuhakikisha hakuna trei inayokaa juu ya nyingine kwa mwelekeo mmoja kwani vitobo vikipandana mbegu itashindwa kuota kwa kukosa sehemu ya kutokea.
Baada ya kupanga trei zote, chukua nailoni nyingine nyeusi kisha funika trei zote vizuri tayari kwa kusubiri mbegu ichipue.
Nini cha kufanya baada ya kufunika mbegu
Katika siku ya pili jioni, anza kuangalia mbegu kama imeanza kuchipua kwani kuna baadhi ya mbegu huchipua haraka sana. Fanya hivyo kila siku asubuhi na jioni. Ukishaona mbegu moja tu imejitokeza, ondoa nailoni na hamishia trei zote kupeleka kwenye eneo la kukuzia miche.
Eneo la kukuzia miche likoje
Eneo la kukuzia miche linatakiwa liwe ni kichanja ambacho kwa chini hakijazibwa bali kina viupenyo. Unaweza kutumia miti migumu kama nguzo (lakini zisiwe zile za kuliwa sana mchwa) na ukapigia mianzi kutengeneza kichanja.
Weka pia miti kidogo kwa juu kwa kuzikunja kutoa upande wa kushoto kwenda kulia ili ikusaidie kufunika kwa kuweka nailoni juu ya miche yako hasa kipindi cha mvua kubwa kwani mvua huweza kufanya miche kuvunjika na hata udongo kudondoka kwenye matundu na mwisho miche kufa.
Nini cha kufanya kwenye kichanja cha kukuzia miche
Baada ya mbegu kuanza kuchomoza, hamisha na panga trei zako zote kwenye eno la kukuzia miche kisha anza kunyunyizia maji kwa kutumia spray pump kila siku mchana. (Usinyunyizie maji asubuhi wala jioni ili kukwepa barafu na pia kushamirisha kuwepo kwa wadudu).
Hakikisha wakati wa kunyunyiza maji, huruhusu kuingia maji mengi kwani kutafanya udongo kupotea kwa kudondoshwa na maji kidogo kidogo na mwisho udongo wote kuisha na hatimaye mbegu kunyauka na kufa.
Mara unapoona kuna magugu yanajitokeza, ondoa mapema yakiwa bado madogo sana kwa sababu zikikomaa ni ngumu kuondoa. Endelea kutunza bustani yako kwa muda ambao utaona miche iko tayari kupelekwa shambani, kulingana na aina ya zao ulilosia.
Faida ya kusia kwa kutumia trei
- Njia hii ni rahisi sana kwa mkulima kutunza miche yake bila usumbufu.
- Miche inayokuzwa kwenye trei, mara ni vigumu sana kushambuliwa na wadudu pamoja na magonjwa kutokana na kuwa udongo uliotumika umetibiwa wakati ule ulipowekewa maji yaliyochemka.
- Mkulima anakuwa na uhakika wa kiasi cha miche ama idadi ya miche aliyonayo kwa ajili ya kupeleka shambani kwake. Hii ni kutokana na kuwa kila trei linakuwa na matundu idadi fulani.
- Miche inayokuzwa kwenye trei haiwezi kufa na kila mbegu huota ilimradi tu mbegu iliyowekwa ilikuwa na kiini.
- Miche inayokuzwa kwenye trei, hushika chini haraka na kukua kwa haraka sana shambani kwani wakati wa kuhamisha, mizizi haikatwi na miche huhamishwa au kuoteshwa pamoja na udongo wake wa kutoka kitaluni.
- Halikadhalika, miche inayokuzwa kwenye trei, mara nyingi haishambuliwi na magonjwa na wadudu kwa haraka baada ya kuhamishiwa shambani kwani kupitia kwenye udongo ule huwa na ukinzani mzuri.
Mimea inayoweza kusiwa kwenye trei
Si mimea yote yanayoweza kusiwa kwenye trei, isipokuwa ni baadhi ya mazao ya bustani kama vile nyanya, pilipili hoho, kabichi, matango.
Maelezo ni mazuri