- Kilimo

Mahindi zao kuu la chakula linalopendwa na kutumiwa sana

Sambaza chapisho hili

Huu ni mwendelezo wa makala inayokuhusu kilimo cha mahindi kutoka toleo lililopita

Inapendekezwa kuweka mbolea baada ya udongo kupimwa. Mbegu ya mahindi iliyoboreshwa inaweza kufanya vizuri inapowekewa mbolea halisi inayohitajika, kulingana na uhitaji wa virutubisho.  Mbolea ya mboji inaweza kuwekwa kwenye shimo wakati wa kupanda.

Palizi

Hakikisha kuwa, shamba lako halina magugu ambayo hushindana na mazao kupata maji na virutubisho. Palizi inaweza kufanyika kwa kutumia mikono au mbinu nyinginezo za kupalilia. Palizi inayofanyika kwa mikono inaweza kufanyika katika kipindi cha wiki 3 tangu kupanda au kutegemeana na ukuaji wa magugu katika eneo husika. Shamba ni lazima liwe safi wakati wote bila magugu hadi mahindi yanapokaribia kukomaa, wakati ambao magugu hayawezi tena kusababisha upungufu wa uzalishaji wa mazao.

Fahamu na udhibiti magonjwa ya mahindi uepuke hasara

Upotevu wa mahindi unaotokana na magonjwa mara nyingi huwa mkubwa sana. Katika msimu ambao una hali ya hewa inayosababisha uwepo wa magonjwa, kunaweza kuwepo na mlipuko ambao matokeo yake ni upotevu mkubwa wa mavuno.

Magonjwa ya mahindi yaliyozoeleka nchini Tanzania yanaweza kugawanywa kama magonjwa ya mizizi, shina, muhindi na magonjwa ya majani.

Mbegu za kienyeji zina uwezo wa kukabiliana na magonjwa kuliko mbegu zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Ingawa mbegu za kisasa zinakuwa zimefanyiwa utafiti kwa muda mrefu, ni vizuri kuelewa kuwa mazingira na hali ya hewa hubadilika mara kwa mara. Vimelea wanaosababisha magonjwa wana uwezo wa kukubalina na mazingira kwa haraka na kukabiliana na vipingamizi.

Magonjwa ya majani

Ugonjwa wa majani unaonekana na kugundulika kwa urahisi, hivyo udhibiti unaweza kufanyika haraka ili kuzuia upotevu wa mavuno.

Ugonjwa wa mizizi, shina na hewa

Mwanzoni ni vigumu sana kugundua magonjwa haya kama ilivyo kwa ugonjwa wa majani, na madhara yake hudhihirika zaidi kwenye mavuno. Madhara huonekana kwa njia mbalimbali. Yanaweza kuonekana moja kwa moja, au ugonjwa unaokuwepo kwa muda, kuwa na punje nyepesi au zenye ubora hafifu, au kuwa na mahindi ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu au wanyama. Hatua za udhibiti kama vile mzunguko wa mazao inaweza kupunguza madhara haya. Matumizi ya kemikali mara nyingi hayasaidii katika kutatua tatizo hili.

Ugonjwa masizi (Boil Smut): Husababisha vivimbe vinavyoziba matundu ya hewa. Ugonjwa huu huanza kwa kuwa na muonekano wa rangi ya fedha na kahawia, kisha baadaye hugeuka na kuwa na rangi nyeusi. Vivimbe hivi huwa na ngozi nyororo ambayo baadaye hupasuka na kuwa vitundu vyenye rangi ya kahawia na nyeusi.

Ugonjwa wa kutu: Ugonjwa huu huathiri sehemu ya majani peke yake, na unaweza kuonekana kwenye sehemu ya juu na chini. Madoa haya husambaa sehemu ya juu ya jani, ambayo baadae hugeuka kuwa madoa madogo. Madoa hayo hugeuka na kuwa na unga wa kahawia. Udhibiti unaweza kufanyika kwa kupanda mbegu zenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa, pamoja na kuteketeza mabaki yote ya mimea ilishambuliwa na ugonjwa huo.

Masizi kwenye mahindi: Uvimbe huu hutokea na kuonekana kwenye ncha ya muhindi. Uvimbe huu huwa na kiasi kikubwa cha weusi kama masizi. Mmea ulioathiriwa na ugonjwa huu hautengenezi muhindi.

Diplodia ear rot: Ugonjwa huu huanza kwa kuwa na ukungu mweupe, ambao baadae hugeuka na kuwa na rangi ya kahawia, ambayo huamia kwenye maganda ya muhindi na kwenye guzi, sehemu ya chini ya punje, na haufuati mstari wa punje.

Fusari na uozo wa kiini: Ugonjwa huu unaonekana kwa mahindi kuwa na vitundu vyeupe na rangi ya pinki. Punje zilizoathirika huzunguka gunzi zikiwa miongoni mwa punje ambazo hazijaathirika. Muhindi athiorika unakuwa na nyuzi nyeupe  na muonekano wa nyota wakati wa kuchanua.

Madoa ya kijivu: Ugonjwa huu unaathiri majani. Jeraha huanza likiwa na rangi ya kahawia, kisha kugeuka na kuwa na rangi ya kijivu. Kidonda hiki huwa na umbo la pembe nne, na husambaa mkabala na mishipa ya jani. Ugonjwa huu huanza na majani ya chini na kwenda juu. Ugonjwa huchachamaa zaidi wakati wa unyevu mwingi. Kudhiti chagua mbegu zinazovumilia magonjwa, na ufanye mzunguko wa mazao kwa miaka miwili.

Ugonjwa wa milia: Ugonjwa huu husababishwa na virusi wa mahindi. Unaathiri majani. Husababisha mistari myeupe na ya njano kwenye majani, ambapo muonekano wake huwa na kijani kilichokolea na chepesi. Mimea iliyo athirika hudumaa na kuonekana kuwa ya njano. Ugonjwa huu husambazwa na nzige.

Wadudu wanaoshambulia mahindi

Viwavi jeshi vamizi: Wadudu hawa hula mahindi ambayo ni machanga na hata yanayokomaa. Huanza kwa kula majani ya chini kwenda juu, wanaweza pia kula aina nyingine za mazao na kumaliza kabisa. Kwa kawaida wadudu hawa hula wakati wa usiku na wakati wa mchana hujificha ardhini.

Sota: Aina hii ya wadudu hushambulia zaidi mahindi yanayoota na mpaka yanapokuwa kwenye hatua ya kuwa na majani manne. Sota hukata shina la muhindi chini kabisa, na hutengeneza tundu chini ya jani la kwanza. Uharibu huanza kabla mahindi hayajachipua vizuri.

Kudhibiti sota: Magugu kidogo yanayosalia shambani, humuwezesha sota kuendelea kuishi na kuwamo shambani mpaka msimu mwingine wa mazao. Ikiwezekana magugu yote yaondolewe shambani wiki 5-6 kabla ya kupanda. Katapila hufa kutokana na njaa.

Wadudu wanaopekecha: Wadudu wanaopekecha mahindi, hushambulia mahindi ambayo yamehifadhiwa. Madhara yanaweza kuanzia shambani, au kwenye sehemu mahindi yaliko hifadhiwa, au vifaa vinavyotumika kuhifadhia. Mahindi hubaki yakiwa na matundu na bila kiina na hayafai tena kwa ajili ya chakula. Safisha sehemu ya kuhifadhia mahindi.

Vipepeo wa mahindi: Wadudu hawa hutaga mayai nje ya sehemu yenye mahindi. Lava wa vipepeo wa mahindi hujilisha kwa kutoboa mahindi. Safisha stoo ya kuhifadhia mahindi vizuri. Usichanganye mahindi ya zamani na mapya, ili kuepuka kueneza maambukizi.

Vidukari: Huathiri majani. Wadudu hawa hunyonya maji kutoka kwenye majani ya mahindi. Kiasi cha juisi ya mmea inayozidi hutolewa kama vile nta ya asali. Maambukizi yakizidi yanaweza kusababisha majani kunyauka na hatimae mmea kufa.

Buibui: Wadudu hawa hujilisha kwa kunyonya sehemu ya chini ya jani. Madhara yakizidi hufanya jani kunyauka na kufa au kulifanya lionekane kama limeungua. Upande wa pili wa jani huonekana likiwa na rangi ya njano. Madhara yanayotokana na buibui yamezoeleka zaidi kwenye eneo lenye joto, na husababisha usumbufu kwa mimea na kuifanya isikue vizuri.

Bungua (Stemborer): Madhara makubwa yanayotokana na katapila ni kuharibu mahindi. Lava wa katapila huwa na rangi ya njano, na kichwa chenye rangi ya kahawia. Lava hawa hutoboa shina la muhindi na kuingia ndani kisha kula ndani kwa ndani kuelekea juu.

Funza weupe: Funza weupe huharibu mahindi machanga. Mahindi yaliyoathiriwa hugeuka rangi na kuwa njano, au zambarau kutokana na virutubisho kuharibiwa au kukosekana kabisa. Mmea hunyauka, kukua taratibu na mara nyingine hufa, jambo linalopunguza idadi ya mimea shambani. Tumia dawa za kuulia wadudu endapo kuna dalili ya funza weupe shambani mwako.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *