- Kilimo

Kutibu udongo kwa kutumia njia ya mvuke au mionzi ya jua

Sambaza chapisho hili

Katika toleo lililopita, tuliangazia kwa undani kidogo kuhusu njia ya kutibu udongo kwa kutumia mvuke ambapo katika toleo hili tutamalizia kwa kuangalia faida zake na njia ya pili ya kutibu kwa kutumia mionzi ya jua.

Kutibu udongo kwa kutumia mvuke ni njia ambayo hutumika kwenye kilimo cha ndani na cha nje ili kuondoa na kuua masalia ya magugu, bakteria na fangasi.

Ni muhimu sana kutibu udongo ili kuua bakteria hatari wa mazao

Faida ya kutibu udongo kwa mvuke.

  • Kuuwa vimelea vya magonjwa kwenye udongo.
  • Kuua mbegu za magugu kwenye udongo mfano baktreria, fangasi na kuvu
  • Ni njia mbadala ya kemikali.
  • Inarahisisha upatikanaji wa virutubisho vya mimea kutoka kwenye udongo.
  • Inaongeza ukuaji wa miche iliyo bora.

Hii ni njia rahisi ya kutibu udongo ambayo mkulima mdogo na mkubwa wanaweza kutumia, pia ni njia salama ya kutibu udongo badala ya kutumia kemikali ambazo huleta madhara kwenye udongo.

Kutibu udongo kwa kutumia mionzi ya jua (solarization)

Matumizi ya mionzi ya jua ni njia rafiki kwa mazingira inayotumika kudhibiti vijidudu, bakteria na magugu kwenye udongo. Mbinu hii inahusisha ufunikaji wa ardhi kwa kutumia mtego. Mara nyingi huwa ni nailoni angavu ambayo hutumika kuruhusu au kusharabu mwanga wa jua.

Jua huunguza udongo katika joto ambalo huua bakteria, wadudu, minyoo fundo, magugu na mbegu za magugu.

Hatua za kutibu udongo kwa kutumia mionzi ya jua.

  • Amua wakati wa kufanya, inashauriwa kutibu udongo wako kipindi cha kiangazi ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya jua kwa kipindi kisicho pungua miezi miwili.
  • Chagua eneo unalotaka kutibu udongo wako.
  • Safisha eneo ulilochagua kutibu udongo wako kwa kuondoa masalia ya mazao na aina yoyote ya mimea.
  • Lima na tifua udongo wako, hakikisha unakuwa laini kwa kutumia jembe na chepeo (beleshi).
  • Sawazisha udongo wako uwe katika usawa kwa kutumia reki.
  • Mwagilia udongo wako mpaka uwe na unyevu na usiwe tope.
  • Funika udongo wako kwa karatasi ya nailoni angavu na nyembamba. Hakikisha karatasi yako inagusa udongo, bana karatasi yako pembezoni kwa kufunikia na udongo.

Angalizo

  • Hairuhusiwi kutumia karatasi za nailoni zenye rangi kwa sababu haziruhusu mionzi ya jua kufika kwenye udongo.
  • Acha nailoni yako kwenye udongo kwa muda wa mwezi mmoja ikiwa ni kipindi cha joto kali (kiangazi) na muda wa wiki sita hadi nane kwa kipindi cha joto la kawaida.
  • Joto linalo hitajika ni 50 hadi 60 sentigredi chini ya karatasi ya nailoni ambalo linaweza kuuwa bakteria, minyoo fundo na mbegu za magugu sumbufu.
  • Angalia joto ridi la udongo kwa kila baada ya wiki kadhaa kwa kutumia kipima joto.
  • Ondoa nailoni juu ya udongo baada ya kupata joto ridi linalohitajika, unaruhusiwa kuondoa karatasi hiyo ya nailoni juu ya udongo wako baada ya miezi miwili. Na tayari utakuwa umeweza kutibu udongo wako.

Faida.

  • Huua wadudu wote waharibifu katika udongo.
  • Huwapa nafasi wadudu rafiki wa mazingira kuendelea kuishi katika udongo.
  • Njia hii ni rafiki kwa mazingira na afya ya binadamu
  • Ni njia rahisi kutibu udongo ukilinganisha na njia nyingine za kutibu udongo

TAHADHARI: Njia ya kutibu udongo kwa kutumia mionzi ya jua huua wadudu wote wafaao na waharibifu. Hivyo basi wakulima wanashauriwa kuweka mboji ili kufanya vijidudu vifaavyo kuendelea kuishi.

 

Kwa maelezo zaidi, unaweza kuwasiliana na Suleiman Mpingama wa Horti-Tengeru. Barua Pepe: mpingama@yahoo.com Simu:+255 685 460 300

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Kutibu udongo kwa kutumia njia ya mvuke au mionzi ya jua

    1. Habari

      Tafadhali jipatie nakala yako ya majarida yetu hapa hapa kwenye tovuti yetu. Fungua sehemu palipoandikwa jarida, na utapata nakala za kila mwezi toka mwaka 2011 hadi sasa.

      Karibu sana Mkulima Mbunifu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *