Mara nyingi wafugaji wa mbuzi na hata wale wa wanyama wengine huendesha pia shughuli za kilimo. Katika mashamba yao ya mazao huotesha pia mimea ya aina nyingine, hii ikiwa ni pamoja na miti. Kilimo mseto ni mfumo wa kilimo wa kuchanganya miti na mazao katika shamba moja.
Miti sahihi kwa kilimo mseto humnufaisha mfugaji kwa njia nyingi. Miti hiyo huweza kutumiwa kama malisho ya mifugo. Baadhi ya miti hutoa matunda mazuri kwa matumizi ya binadamu. Zaidi ya hayo, kilimo mseto huzuia mmomonyoko wa udongo na kurutubisha ardhi. Kadhalika kilimo mseto hudumisha rutuba iliyoko kwenye udongo.
Kuzuia mmomonyoko wa udongo
Miti huimarisha zaidi makingo ya maji katika shamba na kuzuia mmomonyoko wa udongo kwa namna ifuatavyo;
- Kupunguza kasi ya maji, kufanya maji yaingie kwa wingi kwenye ardhi na hivyo kupunguza maji yatembeayo juu ya shamba.
- Kupunguza kasi ya upepo, hivyo kupunguza uwezo wa upepo kuchukua udongo.
- Kunasa udongo uliochukuliwa na maji au upepo.
- Kuongeza mfuniko wa ardhi kutokana na matawi na majani yaangukayo, hivyo kupunguza uwezo wa matone ya mvua kuanzisha mmomonyoko wa udongo.
- Kusababisha kutokea kwa ngazi (terrace) kutokana na kukusanyika kwa udongo toka sehemu ya juu za shamba.
- Kuimarisha umbile la udongo kutokana na mbojiinayojitengeneza na majani yanayoanguka. Hali hii huufanya udongo uwe na uwezo wa kuhimili nguvu za maji na upepo ili zisiweze kuanzisha mmomonyoko wa udongo.
Kurutubisha na kudumisha rutuba ya udongo
- Kutokana na kuzuiliwa kwa udongo, rutuba itadumu kwa muda mrefu zaidi kwani kutakuwa hakuna upotevu.
- Miti mingi itumikayo kwa kilimo mseto ina uwezo wa kuchukua kirutubisho cha aina ya naitrojeni kutoka hewani na kukitunza kwenye mizizi, mashina na majani. Majani yaangukayo shambani na kuoza huongeza katika udongo kirutubisho hiki muhimu kwa mazao.
- Kadhalika baadhi ya miti huweza kuwa na mizizi mirefu inayopenya kwa kina kirefu ardhini na kufyonza virutubisho kutoka chini sana kwenye udongo, eneo ambalo mizizi ya mazao mengi ya kawaida haiwezi kufika. Kwa kufanya hivyo, miti hiyo huleta virutubisho hivyojuu na kuviweka kwenye sehemu za mmea wenyewe kama vile majani. Mara majani hayo yanapoanguka ardhini na kuoza, virutubisho hivyo hubaki kwenye udongo lakini sasa katika kina kinachoweza kufikiwa na mizizi ya mazao ya kawaida.
- Mboji itokanayo na kuoza kwa majani yaliyoanguka huongeza uwezo wa udongo kushikilia virutubisho bila kuviachia viyeyushwe na maji na kupenya chini zaidi kwenye kina kirefu ambacho hakitaweza kufikiwa na mizizi ya mazao na hivyo kupotea bure. Pia, mboji husaidia kudumisha unyevu kwenye udongo.
- Kutokana na uwezo wa miti kurutubisha na kudumisha rutuba ya udongo, matumizi ya mbolea ya chumvichumvi yatapungua sana na hayatakuwepo kabisa. Kwa kuwa hakutakuwa na haja ya kununua mbolea za aina hiyo gharama za uzalishaji wa mazao zitapungua.
Kutoa malisho ya mifugo
Miti ya kilimo mseto kama vile….hutumika kwa malisho ya mifugo kama mbuzi, ng’ombe na kondoo. Wafugaji wadogo wa mbuzi wanaweza kutumia matawi, majani, vikonyo, matunda au mbegu za miti kuongeza malisho ya wanyama wao.
Wakati mwingi wa kiangazi chakula cha wanyama huwa haba wakati ambapo miti huendelea kutoa malisho.
Faida zitokanazo na miti ya kilimo mseto
- Miti iliyopandwa na kuachwa kurefuka hutoa kivuli ambacho huburudisha wanadamu pamoja na mifugo pia.
- Miti huweza kumpatia mkulima kuni.
- Miti itumikapo kama kuni humpunguzia mkulima umbali na muda ambao angeutumia kutafuta kuni.
- Miti ni kinga au akiba kwa mkulima na anaweza kuiuza au kutumia wakati wa matatizo ya kiuchumi.
- Mazao ya miti yanaweza kumwongezea mkulima kipato.
- Miti ya matunda inapotumika kwa kilimo mseto, hutoa matunda kama maparachichi, mapera, maembe na machungwa ambayo ni sehemu muhimu kwa lishe ya binadamu.
- Miti hutoa vifaa vya ujenzi kama mbao, fito na nguzo.
- Miti hufanya mazingira ya shamba na nyumba za wakulima kupendeza na kuvutia zaidi.
- Miti huweza kuvuta nyuki ambao wakiwekewa mizinga wataweza kuzalisha asali.
Madhara ya kilimo mseto kama hakitaendeshwa vizuri
Kama masharti ya kilimo mseto hayatafuatwa kama inavyotakiwa, madhara kadha huweza kutokea. Kwa mfano inashauriwa kuwa matawi ya miti ya kilimo mseto yapunguzwe mara kwa mara. Ikiwa hayatapunguzwa vizuri;
- Mazao karibu na miti hayatastawi na kuzaa vizuri. Hii ni kwasababu mazao hayo hayatapata mwanga wa kutosha. Vilevile, mazao hayo yatakosa virutubisho pamoja na unyevu wa kutosha kutokana na mahitaji makubwa ya virutubisho na unyevu ya miti yenye matawi mengi.
- Yanaweza kuwa sehemu ya kujificha ndege, wanyama waharibifu, wadudu au hata mgonjwa na kudhuru mazao hapo baadaye.
Aina ya miti inayofaa kwa kilimo mseto
Katika kilimo mseto, si miti yote inafaa kupandwa, miti ya kilimo mseto huwa na sifa maalumu ambapo mkulima anafaa kuchagua miti anayoipenda kutegemeana na mahitaji yake na sifa za miti.
Sifa ya miti ya kilimo mseto
- Iwe na matumizi ya aina nyingi kama vile kuni, mkaa, nguzo, fito, mbao, matunda, madwa na malisho kwa mifugo.
- Iwe na mizizi inayokwenda chini ardhini na inayosambaa kido tu kwenye udongo wa juu.
- Iwe ni miti ambayo haishindani na mazao mengine yaliyoko shambani katika kujipatia virutubisho kutoka kwenye udongo.
- Iwe ni miti ambayo ina uwezo wa kukua haraka.
- Iwe na uwezo wa kutoa majani mengi kwa malisho ya mifugo.
- Iwe na uwezo wa kuchipua tena baada ya kukatwa au kuvunwa matawi yake kwa ajili ya kuni au kulishia mifugo.
- Iwe ni miti ambayo ina ladha nzuri kwa mifugo na yenye uwezo wa kuipatia mifugo viini lishe muhimu kwa afya yao.
- Iwe ni miti ambayo inaruhusu mwanga kwa ajili ya mazao mengine yaliyomo shambani.
- Iwe ni miti ambayo ina uwezo wa kurutubisha ardhi kama vile miti ya maji ya mikunde ambayo huongeza virutubisho vya aina ya Naitrojeni kwenye udongo.
- Iwe ni miti ambayo itamzalishia mkulima mazao kama vile matunda, na nguzo, na ambayo itampatia kipato kabla na baada ya kuvunwa.
Kupanda na kutunza miti ya kilimo mseto
- Kwa kuwa miti hupandwa pamoja na mazao ya aina nyingine, mkulima anatakiwa kuwa na mpango maalumu wa kupanda miti kama ifuatavyo;
- Kwenye maeneo ya mwinuko, miti ipandwe kwa kufuata making yaliyotengenezwa vizuri.
- Panda miti ya malisho upande wa nyuma wa kingo (upande wa chini).
- Panda miti ya matunda, miwa, migomba kwenye makingo (juu au chini).
- Miti inaweza kupandwa kuzunguka mipaka ya shamba. Hii itasaidia kuzuia upepo usilete madhara shambani.
- Miti ya matunda, kivuli au urembo ipandwe kuzunguka au karibu na nyumba ya mkulima.
- Kwenye maeneo tambarare, miti ipandwe kwa mistari na mazao mengine yapandwe katikati ya mstari na mstari.
Nafasi kati ya mti na mti au mstari na mstari itategemea malengo ya mkulima ya kupanda miti hiyo kwa mfano;
- Kwenye makingo miti aina ya lukina, kaliandra au sesbania yapandwe kwa mita 15 kutoka mti hadi mti kama lengo ni malisho tu.
- Miti kama grevilea kwenye kilimo msetoiliyopandwa kwa ajili ya mbao au nguzo, basi nafasi iwe mita 10 kati ya mti mmoja hadi mwingine.
- Nafasi kati ya mstari na mstari hutegemea aina ya miti na malengo ya mkulima, lakini kwa kawaida isizidi mita 30 ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Aina za matunzo ya miti
- Palizi
Palizi ni muhimu kwa aina zote za miti hasa inaapokuwa michanga. Miti kama vile lukina, kaliandra na sesbania huhitaji palizi mara mbili au tatu kwa mwaka wa kwanza ili iweze kustawi vizuri.
Lengo la palizi ni kuiondoa mimea aina nyingine isiyotakiwa shambani ambayo hushindana na mazao pamoja na miti iliyopandwa katika kujipatia virutubisho vilivyoko kwenye udongo.
- Ulinzi
Miti ikishapandwa hihitaji kulindwa ili isiliwe na wanyama kama mbuzi na ng’ombe.
- Upogoaji wa miti
Upogoaji au upunguzaji wa matawi ya pembeni ni muhimu sana ili;
- Kupunguza kivuli cha miti kisiathiri mazao mengine yaliyopandwa pamoja na miti.
- Kuwezesha mashine au vifaa vingine vinavyotumika kwa kilimo kama matrekta au maksai kupita kwa uraisi.
- Kupunguza au kupogoa matawi ya miti mapema kabla hayajakauka huifanya miti itoe mbao bora ambazo hazina makovu au mafundo.
- Kupata malisho ya mifugo, kuni na matandazo.
- Kusadia mmea kuwa na matawi machache lakini yenye nguvu na mara mmea uanzapo kuzaa, matawi hayo hubeba matunda makubwa na mazuri zaidi.
Namna ya kupogoa miti
- Upogoaji wa matawi na mizizi ufanywe mapema kabla miti haijapandwa shambani.
- Upogoaji ufanywe kwa kutumia mkazi mkali ili kutoathiri ukuaji mzuri wa miti hiyo.
- Ukataji wa matawi uanze kwa upande wa chini wa matawi na kusihia upande wa juu ili kuepuka tawi kumeguka na kuchuma ngozi au ganda la ndani.
- Matawi yaliyokatwa yanaweza kutumiwa moja kwa moja kulishia mifugo, au kuyaacha shambani kwa wiki moja na kisha kutikiswa ili kutenganisha majani yaliyokauka na miti ya matawi. Matawi hayo yanaweza kutumika kama kuni na majani kutumika kulishia mifugo na kupata mboji.
- Ili kupata virutubisho kutoka kwenye majani kwa haraka, udongo utifuliwe na kuchanganywa na majani mapema.
- Kukata miti juu
Hii ni njia inayotumika pia katika kilimo mseto kwa ajili ya kutunza miti ya grevilea ili kupunguza kivuli kwenye mazao. Kwa kufanya hivyo, mkulima hupata kuni, fito na matandazo kutokana na matawi yaliyokatwa. Shina la mti uliokatwa kichwa huendelea kuongezeka unene kwa ajili ya mbao miaka ijayo na wakati huo huo huendelea kutoa machipukizi ambayo mkulima huyakata kila baada ya mwaka mmoja kwa ajili ya kujipatia kuni, fito na matandazo.
Uvunaji wa miti ya kilimo mseto kulishia mifugo
Tofauti na miti iliyopo kwenye pori au ranchi za kufugia mifugo ambako wanyama hula matawi moja kwa moja kutoka mitini, miti iliyopandwa pamoja na mazao mengine huhitaji utaratibu maalumu (kukata majani au matawi ya miti na kupelekea mifugo) wa kuvuna na kulishia ili;
- Kuzuia mifugo isiingie shambani na kula mazao mengine yaliyopandwa pamoja na miti.
- Kuzuia miti isiharibiwe na mifugo na kushindwa kutoa machipukizi mapya msimu unaofuata.
- Kuzuia mifugo isiharibu mpango uliowekwa shambani na kuepuka mmomonyoko wa udongo kwenye makingo au uharibifu wa mimea ya aina nyingine.
Miti jamii ya mikunde iliyopandwa kwenye making kama vile lukina, kaliandra na sesbania huachwa ikue hadi kufikia urefu wa mita 2 kisha kukatwa katikati na sehemu ya juu kulishia mifugo. Ili kuweza kukata mara kwa mara bila kusababisha miti kufa, sesbania huhitaji kukatwa juu zaidi, urefu upatao mita moja na nusu.
Sababu ya kukata miti kwenye urefu wa mita 2
- Miti hukatwa katika urefu huo na si zaidi ili kuzuia usileta kivuli shambani.
- Sehemu iliyoachwa baada ya kukatwa huendelea kutoa machipukizi na kila mara mkulima huweza kukata na kupelekea mifugo.
Majani yaliyochukuliwa hutakiwa kunyaushwa juani kabla ya kulishia mifugo na majani yaliyokaushwa vizuri huweza kuhifadhiwa kwenye magunia kwa ajili ya kulishia mifugo baadaye wakati hayapatikani kwa urahisi.
Mkulima anashauriwa kuvuna miti yake kwa ajili ya malisho wakati wa kiangazi ambapo huwa kuna uhaba wa malisho ukilinganisha na wakati wa masika.
Miti ya matunda hupunguzwa katika muda maalumu baada ya kuzaa matunda lakini kabla ya kutoa maua kwa ajili ya matundwa kwa msimu utakaofuata.