- Kilimo, Udongo

Kilimo hai kwa vitendo

Sambaza chapisho hili

Mtazamo

Virutubisho hai

Mbolea zisizo za asili hazitumiki katika kilimo hai. Virutubisho vya asili vinavyotokana na mimea hutumika kurutubisha udongo. Kuongeza rutuba kwenye udongo huchukuliwa kama nguzo muhimu. Mbolea za asili hutumika kuboresha au kushikilia rutuba ya udongo, kwa kuongeza mbolea inayotokana na mifugo, mbolea vunde, na kuacha mabaki ya mazao shambani yatumike kama matandazo. Mbolea za asili huwa na virutubisho kama vile N,P na K. virutubisho hivi hupatikana wakati viumbe hai wadogo walioko kwenye ardhi wanapovunja vunja mbolea hizo wakila.

  • Nitrojeni (N): Chanzo kizuri cha asili ya nitrojeni kwa mimea kinatokana na mkojo wa wanyama na aina zote za samadi za wanyama. Mbolea zinazotokana na mimea na wanyama hutoa nitrojeni nzuri kwa mimea. Mimea jamii ya mikunde na mbolea vunde ni chanzo kizuri cha asili kuweza kuipatia mimea nitrojeni.
  • Fosiforasi (P): njia za asili za kupata fosiforasi ni kupitia mbolea ya miamba, mbolea ya kuku na wanyama wengineo.
  • Potashiamu (K): njia za asili za kupata potasiamu ni majivu, samadi ya mbuzi, kondoo na mifugo mingine.

Udhibiti wa wadudu na magonjwa kwa njia za asili

Kulima kwa mzunguko ni njia kuu ya kuweza kudhibiti wadudu na magonjwa. Mazao yanayostahimili aina fulani ya wadudu na magonjwa ni lazima yapewe kipaumbele. Kilimo hai ni lazima kisaidie ustawi wa wadudu wenye faida pamoja na wanaosaidia kula visumbufu vya mazao, kwa kuwa husaidia kufanya mimea kuwa na afya na kuiwezesha kukabiliana na wadudu na magonjwa.

Udhibiti wa magugu

Udhibiti wa magugu katika kilimo hai hutegemea mzunguko wa mazao, kupanda mimea inayotambaa, na kutumia mbolea vunde sehemu ambayo kuna uhaba wa mimea inayotambaa, pamoja na kufunika ardhi kwa kutumia aina tofauti za matandazo (hii ni pamoja na kutumia plastiki). Kupalilia mapema, kuandaa ardhi mapema na kuacha mabaki ya mazao shambani, husaidia kupunguza wingi wa magugu. Kupalilia kwa mikono au jembe, au kufyeka na kuacha magugu shambani kama matandazo ni muhimu kwa mazao mengi.

Ufugaji wa asili

Mifugo ni moja ya sehemu muhimu sana katika kilimo hai. Wanyama hutoa samadi ambayo hutumika kama mbolea. Mimea ya malisho inaweza kutumika katika mzunguko wa mazao. Nyasi na malisho ya jamii ya mikunde ni malisho bora kwa wanyama wanaocheua lakini pia husaidia kujenga udongo, kuupatia nitrojeni, na ni mazuri katika kufanya mzunguko wa mabaki ya mazao. Afya ya wanyama, inapewa kipaumbele kwa kuwa kuzuia magonjwa ni moja ya nguzo muhimu katika kilimo hai.

Afya ya mifugo katika kilimo hai, huimarishwa kwa kuzingatia kuwa na mbegu bora, kuwa na malazi safi na makavu pamoja na nyumba bora, kuchunga pale inapowezekana, pamoja na ulishaji unaozingatia upatikanaji wa virutubisho vyote na kwa kiwango kinachojitosheleza.

Ni faida gani zinazoweza kutarajiwa kutokana na kilimo hai?

  • Kilimo hai huongeza rutuba kwenye udongo kwa muda mrefu. Udongo hai una kiasi kikubwa cha virutubisho vinavyotokana na uozo wa malighafi za asili. Pia huongeza uwezo wa ardhi kuzalisha, kuhifadhi maji kwa muda mrefu na kukabiliana na ukame.
  • Kilimo hai hakihitaji kuwekeza gharama kubwa. Kilimo hai hutumia miundo mbinu inayopatikana kirahisi hivyo kumuepushia mkulima mdogo gharama za pembejeo za viwandani.
  • Kilimo hai hakimuweki mkulima pamoja na familia yake katika athari ya kupata magonjwa yanayotokana na matumizi ya kemikali na mbolea za viwandani.
  • Kilimo hai kinajumuisha tafiti za kisayansi na kilimo cha kijadi katika kilimo endelevu.
  • Hata kama kanuni za kilimo hazijazingatiwa ipasavyo, na hata kama hakuna soko la mazao ya kilimo hai yaliyozalishwa, mazao na bidhaa zake yanaweza kupatikana, na shamba pia hufaidika kwa kutumia mbinu za kilimo hai.

Kwa maelezo zaidi Unaweza kuwasiliana na Mkulima Mbunifu kwa simu namba +255 0717266007 au kwa barua pepe info@ mkulimambunifu.org

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *