(Beetroot) Kiazi sukari ama hufahamika kama kiazi chekundu ni zao jamii ya mizizi.
Kiazi sukari hutumika kama dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali kama kuvimbiwa, majeraha, pamoja na matatizo mbalimbali ya Ngozi (mizizi ndiyo hutumika).
Hadi kufikia karne ya 16, zao hili lilikuwa tayari limekwishapata umaarufu hasa katika Amerika ya Kati na Ulaya ya Mashariki na baadaye kupokelewa katika nchi zingine kama Roma, Ufaransa, Poland, USA, Russia na Ujerumani, huku ikija kwa maumbile na rangi tofauti.
Matumizi ya zao hili yaliendelea kuongezeka (ikiwa ni pamoja na kulimwa kwa ajili ya chakula) hivyo kulifanya kulimwa kwa wingi katika nchi mbalimbali dunia ikiwa ni pamoja na nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Aina za kiazi chekundu ama kiazi sukari
Kuna aina mbalimbali za kiazi sukari kama nyekundu, nyekundu yenye mistari myeupe kwa ndani, na nyeupe. Hata hivyo, beetroot nyekundu ndiyo inayolimwa kwa wingi hapa nchini.
Matumizi
Zao hili lenye madini ya foliate, chuma, magnesiamu, vitamini C na potasiamu lina matumizi mengi kwa binadamu na hata kwa wanyama.
- Kiazi sukari hutumika kama chakula au kiungo ilivyo karoti kwa ajili ya kuongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali.
- Zao hili pia hutumika kutengenezea juisi. Unaweza kutumia kiazi sukari pekee au ukachanganya na matunda mengine.
- Huongeza damu mwilini pamoja na kuupa mwili nguvu na kusaidia kuboresha kumbukumbu.
- Ni dawa na hutumika kutibu ugonjwa wa sukari, kuvimbiwa, majeraha na magonjwa ya ngozi.
- Majani yake huweza kutumiwa kama lishe kwa ajili ya kulishia mifugo wa aina mbalimbali.
Namna ya kusindika kiazi sukari
- Chukua viazi kiasi unachohitaji kwa ajili ya kusindika, osha kwa maji safi na salama.
- Kata vipande vidogovidogo na vyembamba kwa uwiano unaolingana.
- Panga vipande hivyo kwenye kaushio la jua. Acha juani mpaka vikauke kisha saga na hifadhi kwenye mifuko ya kuhifadhia unga tayari kwa kutumia au kupeleka sokoni.
Namna ya kutumia unga kiazi sukari
Unga wa kiazi sukari hutumika kutengeneza/kukoroga juisi, kunywa kama chai, kuongeza kwenye supu au uji.