Kwa kawaida viumbe hai vyote ni vya asili. Fikra na mitazamo juu ya kilimo hai inaonekana kama vile viumbe hai wana sehemu yao maalumu tangu miaka mingi iliyopita. Hii inajumuisha viumbe wadogo wadogo waliopo ardhini, kwenye mimea, wanyama pamoja na binadamu mwenyewe.
Mfumo wa kilimo hai umetelekezwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko katika sekta ya viwanda, ongezeko la watu na mahitaji makubwa ya chakula katika nchi zilizoendelea kwa karne nyingi na zinazoendelea hivi sasa.
Kilimo hai kimejaribu kuangalia na kupata picha nzima ya mazingira siyo tu aina moja ya wadudu wanaweza kuuliwa, lakini kilimo hai kimejaribu kuweka sawa shughuli za kilimo kwa njia za asili za uzalishaji wa mazao ya chakula na mazao mengine kwa mzunguko wa kiasili.
Rutuba ya udongo, mimea, binadamu
Kilimo hai ni lazima kiwezeshe na kiongeze rutuba ya udongo, afya ya mimea, wanyama na binadamu.
Udongo ni nguzo muhimu katika maisha ya viumbe wote kwa ujumla. Udongo ulioharibiwa hauwezi kuzalisha chakula kizuri pia malisho ya kutosha kwa ajii ya mifugo. Ili kuweza kupata chakula cha kutosha kwa ajili ya binadamu na malisho ya wanyama, ni lazima kuboresha rutuba ya udongo. Afya ya binadamu na wanyama inaenda sambamba na umuhimu na ubora wa udongo.
Mashamba ni sehemu ya ikolojia
Kilimo hai ni lazima kitegemee mzunguko na mfumo mzima wa ikolojia. Mambo hayo hayawezi kutenganishwa lazima yapokelewe katika hali zote na kukubalika katika nyanja za kilimo, kijadi na kiutamaduni.
Usawa katika mahuusiano yote
Wakulima wanaofanya kilimo hai wanahitaji kuona kuwa wanashirikiana katika maisha ya ulimwengu huu na viumbe hai wote, pamoja na hayo binadamu na wanyama wanatakiwa kupata nafasi yao ya kuwa na afya njema na furaha. Hii inajumuisha usawa katika ngazi zote na kwa wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara. Kilimo hai kinalenga kuhakikisha ubora wa maisha ya kila mtu, na kuchangia ukombozi wa chakula na kupunguza umaskini. Uasili na mazingira ni lazima vitunzwe kwa ushirikiano na ikolojia.
Uangalifu- Tahadhari
Wakulima wa asili hutekeleza majukumu yao kama watumiaji makini wa ardhi. Ardhi kwa ajili ya kilimo na miundo mbinu mingine kama vile vyanzo vya maji, ni lazima vitunzwe katika hali nzuri, kwa ajili ya kizazi kijacho. Watu na wanyama ni lazima watunzwe na kuangaliwa kwa umakini ili kihakikisha afya zao zinaendelea kuwa salama.
Teknolojia ya kisasa, pamoja na njia za kiasili ni lazima zichunguzwe na kuangaliwa kwa kufuata taratibu za kiasili. Tahadhari za kuzuia ni lazima zizingatiwe ili hatari zinazoweza kujitokeza zidhibitiwe na maamuzi yazingatie thamani na mahitaji ya viumbe wote wanaoweza kuathiriwa.
Mbinu za kilimo hai kwa ufupi
Kilimo cha asili
Mfumo wa kilimo cha asili unajumuisha muundo wa kilimo cha jadi ambao umekuwa ukitumika kwa karne nyingi. Kwa kawaida huzingatia matumizi mazuri ya miundo mbinu inayopatikana na njia za kienyeji, hali ya ikolojia na mahusiano thabiti. Ikiwa mbinu za kijadi zikifuatwa, mbali na mabadiliko ya hali halisi, zinaweza kusababisha madhara, vinginevyo ni lazima zirekebishwe. Mfano mbinu za kiasili ya kufyeka na kuchoma moto, hili si tatizo endapo ni sehemu ndogo tu ya ardhi ndiyo inayotumika kwa kilimo. Mbinu hiyo hiyo iinaleta uharibifu wa misity pamoja na arddhi, pale tu kunapokuwepo ongezeko la watu, hivyo kupunguza utunzaji wa ardhi.
Kilimo mchanganyiko
Mtindo wa kilimo mchanganyiko unajumuisha faida za mbinu zote zinazotumika katika kilimo. Hupunguza na kuepuka madhara yanayotokana na kilimo cha kisasa kwa kujumuisha mbinu za kilimo hai, kwa kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani na kemikali, na kuchagua kwa uangalifu viuatilifu. Katika nchi nyingi hii inaonekana kuwa njia sahihi ya kurekebisha madhara yanayotokana na kilimo cha kisasa.