Kabla ya kusindika maziwa ya mgando au mabichi ni lazima kufanya vipimo vya awali ili kujua kama maziwa yanafaa kusindika au hayafai. Kipimo kikubwa kinachotumika kupima maziwa ni alkoholi (Ethanol)
Kipimo hiki hutumika kutambua maziwa yaliyoharibika na maziwa yaliyoanza kuganda.
Namna ya kupima
Chukua kiwango kinacholingana cha Alkoholi (ethanol) na maziwa mabichi kisha changanya pamoja kwa kuweka katika chombo maalum cha kupimia. Kwa mfano: ml.1 ya maziwa na ml.1 ya ethanol.
Tengeneza mchanganyo kwa kutikisa kisha angalia kama maziwa yataganda. Ikiwa maziwa yataganda, basi hayafai kutumiwa.
Usindikaji wa maziwa mabichi
Maziwa mabichi (fresh) ni maziwa halisi ambayo yamekamuliwa katika hali ya usafi na kuhifadhiwa kama yalivyo yaani hayajaongezwa wala kupunguzwa kitu chochote. Maziwa haya husindikwa na kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila kuharibika na yakatumika katika matumizi ya kawaida huku yakiwa bado halisi.
Mahitaji
- Maziwa mabichi (Kiasi unachotaka kusindika)
- Alkoholi (Ethanol)
- Jiko
- Sufuria
- Chupa au keni lenye mfuniko
- Kipimajoto kwa ajili ya kupimia joto
- Maji kwa ajili ya kuchemshia maziwa
Hatua
- Hakikisha maziwa hayo ni fresh. Pima kwa kutumia alkoholi (mililita 1 ya ethanol – mililita 1 ya maziwa).
- Andaa jiko kisha bandika sufuria tayari kwa kuchemsha maziwa.
- Weka maji kiasi unachoona hakitamwagika pindi utakapotumbukiza keni lenye maziwa.
- Weka maziwa kwenye keni na funika vizuri kisha tumbukiza kwenye maji yaliyo jikoni tayari kwa kuchemsha.
- Chemsha maziwa yakiwa ndani ya keni hadi kufikia nyuzi joto kati ya 80°C na 90°C kwa muda wa dakika nne hadi tano.
- Baada ya hapo epua na anza kufungasha maziwa yakiwa bado ya moto.
- Weka maziwa yaliyofungushwa kwenye maji ya baridi kwa ajili ya kupoozea mpaka yafikie nyuzi joto kati ya 10°C na 20°C
- Chukua maziwa na weka katika chumba chenye ubaridi, yakae humo kati ya masaa 5 hadi 8
- Baada ya hapo maziwa yatakuwa tayari kwa kuuza au kupeleka sokoni.
Usindikaji wa maziwa ya mgando
Maziwa mgando ni maziwa ambayo hayapo tena katika hali ya ubichi bali yameganda, kunakosababishwa na bakteria wasio na madhara na ambao wamekuwa ndani ya maziwa.
Wadudu hao hubadilisha baadhi ya chembe chembe za maziwa kuwa na asidi ambayo hubadilisha ladha ya maziwa. Maziwa ya mgando au mtindi huanza kufanyiwa usindikaji yakiwa bado katika hali ya ubichi.
Mahitaji
- Maziwa mabichi (fresh)
- Alkoholi (Ethanol)
- Kimea (Culture)
- Kipimajoto
- Jiko
- Sufuria
- Maji kwa ajili ya kuchemshia maziwa
Hatua
- Hakikisha maziwa ni fresh (Pima kwa kutumia alkoholi) mililita 1 ya ethanol – mililita 1 ya maziwa).
- Andaa jiko kisha bandika sufuria tayari kwa kuchemsha maziwa.
- Weka maji kiasi unachoona hakitamwagika pindi utakapotumbukiza gudulia lenye maziwa.
- Weka maziwa kwenye gudulia na funika vizuri kisha tumbukiza kwenye maji yaliyo jikoni tayari kwa kuchemsha.
- Chemsha maziwa kwa dakika 4-5 yakiwa katika nyuzi joto kati ya 78°C na 82°
- Epua maziwa na weka katika maji ya baridi kwa ajili ya kupooza kisha acha yapoe mpaka yafikie nyuzi joto kati ya 25°C na 30°
- Weka kimea kijiko kimoja cha chakula (Kwa kila lita 10 ya maziwa).
- Koroga kwa dakika 5 kisha acha kwa muda wa saa 8-9 na maziwa yatakuwa tayari yameganda. Tumia upao kukoroga. Koroga kuelekea upande mmoja tu, usikoroge kuelekea upande wa kulia na upande wa kushoto kwa wakati mmoja.
- Fungasha na weka katika chumba chenye ubaridi kwa saa 5-8.
- Baada ya hapo maziwa yako tayari kwa kuuzwa au kupelekwa sokoni.