- Binadamu, Mazingira, Usindikaji

Shambani hadi mezani; Fursa ya biashara ya chakula

Sambaza chapisho hili

Kuna fursa mbalimbali za kibunifu zinazoweza kumsaidia mkulima kujikwamua kiuchumi. Ikiwa wakulima wengi wamekua na changamoto ya soko la mazao wanayozalisha, shambani kwenda mezani ni fursa nzuri kama utazingatia na kuifanya kwa ufanisi.

Shambani kwenda mezani ni msemo unaoweza kumaanisha mambo tofauti kwa watu tofauti. Hata hivyo maana yake ni kwamba chakula kilichoandaliwa mezani kimetoka moja kwa moja shambani, bila kupita sokoni, dukani au kutoka kwa mtu anaesambaza njiani. Mtu yeyote anaezalisha mazao kwa njia salama yaani kwa mbinu za kilimo hai anaweza kufanya biashara ya aina hii.

Katika uhalisia wake, humaanisha meza iko shambani, yaani wapishi huchukua chakula shambani, kukiandaa na kuweka mezani. Chakula hiki huandaliwa kiasili kwa kuzingatia uhitaji wa watu wanaokula. Vilevile, huwa ni chakula cha asili cha kitamaduni katika eneo ambapo shamba lipo.

Mfano wa vyakula ambavyo huandaliwa ni kama vile Maharage, magimbi, mihogo, ndizi za kupikwa, supu ya boga, mahindi ya kuchemsha, mboga za majani, saladi, juice ya matunda yaliopo katika msimu na yanayopatikana eneo hilo, samaki, kuku, nyama ya ng’ombe ama kuku.

MUHIMU: Ni vema vyakula hivi vikawa ni vyakula vya asili vinavyopatikana shambani kwako au kwa jirani ambaye anazalisha kwa mbinu za kilimo hai.

Mahitaji:

  • Hakikisha wewe ni mkulima wa kilimo hai na unazalisha aina mbalimbali ya mazao ya chakula katika shamba lako. Kama vile mboga mboga na matunda, mazao jamii ya mikunde, mahindi, mazao ya mizizi, mihogo, magimbi, viazi lishe, viazi mbatata, vibere.
  • Kama huna kuku, nyama ya Mbuzi, ngombe, kondoo na samaki, shambani kwako, ni vema ukapata kwa wafugaji unaowaamini na wanaofuga kiasili.
  • Jiko safi la kupikia chakula
  • Vyombo safi vya kupikia na kupakulia chakula
  • Andaa sehemu ya kukaa kwaajili ya chakula
  • Tafuta wateja: Kuna njia mbalimbali za kupata wateja, kupitia mitandao ya kijamii, simu ya mkononi makundi ya whatsApp, magazeti, marafiki, hoteli za kitalii, bandika matangazo na kumbuka kuweka anuani ya simu na anuani ya eneo husika.

Jinsi ya kuandaa

  • Andaa orodha ya vyakula utakavyohitaji kupika kulingana na wateja waliokuhakikishia watafika.
  • Andaa mahitaji yote yatakayokusaidia kuandaa vyakula ulivyoorodhesha, bila kusahau vyakula vinavyoliwa vibichi kama kachumbari na saladi.
  • Andaa vyakula vyako kwa usafi kwa ubunifu, bila kupoteza virutubisho na ladha.
  • Andaa matunda na juisi ya matunda yanayopatikana katika msimu husika.

MUHIMU: Zingatia mlo kamili katika orodha ya vyakula unavyoandaa.

  • Baada ya kuviandaa unaweza kuvipanga katika meza ya chakula tayari kwa kupakua na kula.

Mkulima Mbunifu ilipata fursa ya kutembelea shamba la kilimo hai Zanzibar; Msonge Organic Family Farm. Ambapo, mbali na kuzalisha mazao ya kilimo hai wamejikita pia katika kuandaa chakula cha kiasili mezani.

Kila jumapili, shamba hili huandaa chakula na kualika wateja kutoka sehemu mbalimbali ambao huhudhuria na kuchangia kiasi kidogo cha fedha ambacho kinasaidia kuendeleza mzunguko wa uzalishaji chakula shambani.

Mkulima Mbunifu inashirikisha uzoefu huu maradufu kwa wakulima wengine wa kilimo hai nchini Tanzania kubuni miradi mbalimbali kutokana na mazao wanayo zalisha. Aidha, mfumo huu unaelimisha juu ya uandaaji wa chakula ili kuboresha afya kwa binadamu bila kupoteza virutubisho muhimu. Vile vile ni fursa ya kibiashara ambayo mkulima anaweza kuitumia kujiingizia kupato.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Dr. Mwatima Juma kwa simu namba 0754536630

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *