Mazingira ni jumla ya mambo yote yanayomzuguka mwanadamu na viumbe hai katika maisha yao. Kwa hiyo kila unachokiona ni mazingira yako.
Mazingira yakiwa katika hali ya usafi hupendeza na kuvutia. Mazingira yasipowekwa katika hali ya usafi huatarisha afya ya viumbe hai waishio katika mazingira hayo ikiwamo binadamu, wanyama, na mimea pia.
Pamoja na serikali kutangaza kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilifungwa rasmi tarehe 31/5/2019, bado kumekua na changamoto ya watu kutupa makopo ya plastiki holela katika maeneo mbali mbali ya jamii zetu.
Hali hii inahatarisha afya ya mazingira kwani makopo hayo huokotwa na watoto au watu wazima, wakati mwingine bila kufahamu makopo hayo yalitumika kuweka kimiminika cha aina gani. Makala hii itaelezea madhara ya utupaji holela wa makopo yaliokwisha matumizi ya viuatilifu.
Viuatilifu
Viuatilifu ni sumu ambayo hutumika kuua, kuangamiza, kufukuza, au kuzuia visumbufu katika mimea. Visumbufu vya mimea vinaweza kuwa wadudu, kuvu (fangasi), magugu, pamoja na baadhi ya wanyama na ndege.
Kituo cha Utafiti wa Viuatilifu Tanzania – TPRI (Tropical Pesticide Research Institute) kinafanya tafiti na kinatoa mafunzo na huduma katika afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira. Kituo hiki kinatoa ushauri kwa jamii hasa wakulima wanaotumia viuatilifu kutokuvitupa holela vifaa vinavyotumika kutunzia viuatilifu baada ya kuvitumia.
Utupaji holela wa makopo vya plastiki
Viuatilifu vingi baada ya kutengenezwa viwandani huifadhiwa katika makopo au mifuko ya plastiki au chupa na huwa na maelezo kuhusu kimiminika ama kiuatilifu hicho.
Watu wengi hasa baadhi ya wakulima wamekua wakitupa kiholela/isivyo sahihi vitunzio vya viuatilifu (viwekeo ama chupa tupu) baada ya kumaliza matumizi yake. Baadhi ya vitunzio hivyo kama makopo ama vifuko vya plastiki vimekua vikirushwa katika vyanzo ama mifereji ya maji ambayo hutumiwa kwa matumizi ya binadamu na hata wanyama pia.
Kutokana na kushamiri kwa biashara za makopo ya plastiki katika maeneo mengi ya nchi, vijana wengi kutokana na ugumu wa maisha, lakini pia watoto wa shule wamekua wakitembea na kuokota makopo ya plastiki ili kujipatia kipato. Mbali na kwamba uokotaji wa makopo haya ya plastiki inasemekana umesaidia kupunguza uzagaaji wa makopo hayo katika jamii, ni dhahiri kwamba ukusanyaji wa makopo hauzingatii afya ya muokotaji.
Katika maeneo mengi usalama wa vyanzo vya maji umekua katika hatari ya kuathiriwa kutokana na utupaji holela wa vifaa vilivyotumika kutunzia vimiminika vyenye kemikali zenye sumu kama viuatilifu au mbolea za viwandani. Kemikali hizo kawaida hazionekani kwa macho na ni vigumu kuzigundua. Hivyo, maji yanapaswa kupimwa kwenye maabara kuchunguza uwezekano wa kuwepo sumu ama kemikali za viwandani. Taasisi ya TPRI imekua ikifanya na inaendelea kufanya chunguzi huu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Athari za utupaji holela wa vifaa vilivyokwisha matumizi ya viuatilifu
Kwa binadamu: Maji yaliochafuliwa huweza kuwa na mabaki ya viuatilifu ambavyo huweza kumuathiri binadamu atumiapo maji hayo. Na madhara haya kwa kawaida huonekana haraka kwa wazee na watoto kwani wao huwa na kinga ya mwili (immunity) ndogo. Madhara ambayo binadamu hupata ni kama kuvurugika kwa afya, tumbo kuuma, kuharisha, kuharibu mfumo wa damu, huathiri ini na mengineyo.
Kwa wanyama: Wanyama hutumia kiasi kikubwa cha maji hivyo pindi wanapokunywa maji yale yenye mchanganyiko wa kemikali hizo za viuatilifu maji hayo huweza kuharibu homoni za kike na kiume na vina saba, hata pengine kusababisha mnyama kuzaa kiumbe ambacho hakijakamilika.
Kwa mimea: Mimea ambayo haikua lengwa kwa kiutilifu hicho huathirika kwani hunyonya kemikali hizo na baadae hufa. Mimea hiyo yaweza kua ni chakula ama hutumika kama hifadhi kwa wanyama waishio kwenye maji. Inapoathirika na kufa huathiri wanyama wale tegemezi kwa mimea hiyo.
Kwenye Udongo: Udongo huathirika kwani kemikali zile hufyonzwa kwenye udongo na kuua wadudu ambao ni rafiki wa mazingira na muhimu katika urutubishaji wa udongo. Wadudu kama minyoo, konokono, mchwa na hata vyura ambao huitajika katika ekolojia ya eneo hilo hufa.
Nini kifanyike kuzuia utupaji holela wa makopo/vifuko vya plastiki vilivyokuwa vimewekea viuatilifu
- Njia pekee ya kuzuia utupaji wa makopo ya plastiki holela ni kuihamasisha jamii kutenga maeneo kwaajili ya kutupa makopo hayo ya plastiki yaliyokua na viuatilifu.
- Ili kutupa chupa iliyokwisha kiuatilifu, unashauriwa kuisuuza kwa maji mengi mara tatu na baada ya hapo unashauriwa kuiharibu kwa kuitoboa ili isiweze kutumika tena na kuipeleka katika eneo la kukusanyia chupa hizo au viwekeo hivyo tupu.
ANGALIZO:
- Muoshaji anatakiwa kuvaa gloves wakati wa kuosha kikopo hicho au chupa iliyokwisha kiuatilifu.
- Maji yaliyotumika kusuuza kikopo/chupa hicho yachanganywe kwenye bomba la kunyunyizia kabla mkulima hajajaza bomba lake. Mchanganyiko unyunyiziwe kwenye mimea lengwa au kwenye majani pembeni ya shamba na endapo unyunyiziaji tayari umekamilika maji hayo yasimwagwe karibu na au kwenye chanzo cha maji.
- Ili kulinda maji yasichafuliwe na kemikali zenye sumu ni vizuri kuzuia uchafuzi kwenye vyanzo vya maji. Iwapo unadhani maji yenu yamechafuliwa, mnaweza kuihamasisha jamii yenu kuchunguza vyanzo vya maji na kutafuta matatizo yanayochangia uchafuzi na hatimaye kuchukua hatua kukomesha uchafuzi huo. Lakini njia ya kujua kwa uhakika ni kemikali gani zipo kwenye maji ni kwa kipimo cha maabara.
- Wakulima wanashauriwa kutumia njia za asili za kuzuia wadudu na mbolea za asili (mboji) badala ya kemikali zenye sumu. Hii itasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa madhara yatokanayo na matumizi ya viuatilifu au mbolea za viwandani.
Kwa maswali tafadhali wasiliana na Mwema Felix, Kitengo cha Udhibiti wa Viuatilifu na Utunzaji wa Mazingira, TPRI, kwa simu namba 0766486611