Gusa bomba ni teknologia inayokuwezesha kusafisha mikono yako bila kugusa chanzo cha maji.
Kwa kawaida tumezoea kuwa unaenda bombani kunawa mikono kabla ya kula chakula, baada ya kutoka chooni, au wakati wowote unapohisi kuchafuka. Unapofika kwenye bomba huku mikono yako ikiwa michafu, unafungua bomba, maji yanatoka halafu unanawa mikono.
Baada ya kumaliza kunawa mikono unafunga bomba. Wakati wa kufunga bomba, unafunga huku mikono yako ikiwa misafi hivyo utachafua kwani ulifungua bomba.
Vifaa vinavyohitajika kutengeneza gusa bomba
- Dumu cha lita 3 au 5
- Kamba ngumu au waya
- Fito 3 (2 mita 1, 1 nusu mita)
- Misumari
Hatua za kutengeneza gusa bomba
- Chukua fito zako za mita 1 na ziunganishe pamoja na fito yako ya nusu mita kwa kutumia misumari.
- Chimba mashimo mawili umbali wa nusu mita na simamisha fito ulizoziunganisha pamoja hapo juu.
- Chukua msumari na uweke kwenye moto kisha toboa vitundu kwenye dumu. Utatoboa sehemu ya kumwaga maji, sehemu kushikilia dumu kwenye fito na sehemu ya kuungia.
Chukua kamba ngumu au waya na uingize kwenye sehemu ya kushikilia dumu, kisha fungia kwenye fito zako ulizozisimamisha.
- Funga kamba au waya wa pedali kulingana na umbali wa dumu uliopo. Baada ya kufunga kamba, weka kijiti chini na kifungie kwenye hii kamba. Kijiti hiki kitakuwa pedali. Hakikisha kijiti hiki kimenyanyuka kidogo ili unapokuwa unakikanyaga kidumu kibinuke na kutoa maji.
MUHIMU: Njia hii ni nzuri na salama zaidi hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Mkurugenzi wa Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Janeth Maro, kwa simu namba +255 754 925 560