- Binadamu, Kilimo, Kilimo Biashara, Kutuhusu, Masoko

Fahamu ukubwa wa soko la bidhaa za kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Historia inaonesha miaka ya zamani kilimo kilikuwa kinafanyika kupitia mbegu za mkulima mwenyewe. Hali hiyo ilitokea kutokana na utaratibu au utamaduni ambao wakulima walirithi kwa mababu kuwa mbegu, mbolea na viuatilifu vya msimu ujayo vinatoka shambani na si kwingineko.

Ujio wa mapinduzi ya viwanda duniani unatajwa kuwa ulikuja na faida na hasara zake ambapo moja ya sekta ambayo imepata hasara ni sekta ya kilimo ambayo kwa sasa asilimia 60 inategemea pembejeo kutoka viwandani ili kuweza kutekelezeka shughuli za uzalishaji.

Jarida la Mkulima Mbunifu, ni miongoni mwa wadau wakubwa katika kueneza teknolojia ya uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai kwa wakulima wadogo nchini Tanzania kupitia machapisho mbalimbali ikiwemo jarida lenyewe, moduli, vitabu mbalimbali pamoja na matoleo maalumu.

Kwa kushirikiana na wadau wengine katika sekta ya kilimo ikolojia, wakulima wengi wamehamasika na wameanza kulima au kuzalisha kwa kufuata mfumo wa kilimo ikolojia pamoja na kutumia bidhaa zake.

Matokeo chanya hayo yametajwa kuibua changamoto nyingine ya masoko ya bidhaa zao ndani au nje ya nchi, hoja ambayo inajibiwa na wauzaji wa bidhaa hizo za kiikolojia.

Kampuni TANZPRO Greens Limited (maafuru Be Organic) ni mmoja ya wadau ambao wamewekeza katika maduka ya kuuza mazao ambayo yanazalishwa kwa mfumo wa kilimo ikolojia.

Meneja uendeshaji wa TANZPRO, Samuel Mwanga anasema soko la mazao na bidhaa zilizozalishwa na kuandaliwa kwa mfumo wa kilimo ikolojia hai ni kubwa na kwamba wanakaribisha mkulima yoyote mwenye vigezo apeleke mazao na bidhaa zake.

Mwanga anasema duka lao lipo Masaki, Kinondoni mkoani Dar es Salaam na wamekuwa wakifanya biashara za bidhaa za kiikolojia kwa muda mrefu.

“Sisi kama TANZPRO tupo Masaki jijini Dar es Salaam, tunauza mazao na bidhaa zilizozalishwa kwa njia ya kiikolojia, tunawakaribisha wakulima wenye bidhaa zenye sifa hiyo watuletee hapa tutanunua,” anasema.

Meneja huyo anasema bidhaa zao zina soko kubwa kwa watanzania na wageni hasa wenye elimu kubwa na kipato, hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa jamii nzima ili ijue faida ya bidhaa za kilimo hai.

Mwanga anasema katika kuhakikisha dhamira yao ya kubadilisha mitazamo ya watanzania kutumia bidhaa za kilimo hai wamekuwa wakilima katika shamba lao lililopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

“Mkuranga tuna mashamba matatu yenye ukubwa tofauti ambapo tunalima mazao mchanganyiko yakiwemo mbogamboga na soko lipo la uhakika, hasa nyanya, bilinganya, karoti na mengine,” anasema.

Naye Meneja wa Duka la Kampuni ya I am Organic, Norine Kweka anasema kuwa bidhaa za kilimo hai zina soko la uhakika, hivyo kuwataka wakulima waongeze kasi ya uzalishaji.

“Hapa kwetu tunauza matunda, nyanya, karoti, ndizi mbivu, viazi ulaya, vitunguu na mbogamboga nyingine muhimu,” anasema.

Kweka anasema pia mchele, mafuta ya alizeti, mbegu za alizeti, unga, njugu mawe, korosho na nyingine wakulima walime na kuwapelekea dukani kwako Masaki.

Kweka anasema matamanio yao ni kuona watanzania wanakula bidhaa za kilimo hai kwa kuwa zina faida nyingi kiafya kulingana na kuwa hazina dawa kama ilivyo kwenye mazao mengine.

Mmiliki wa Glen Farm Shop na msimamizi wa duka la mazao ya kilimo hai MESULA mkoani Arusha Bw. Glen Tells anasema soko la bidhaa za kilimo ikolojia hai ni kubwa kwani kwa sasa upatikanaji wa bidhaa za kilimo hai haufiki hata nusu ya mahitaji.

Anasema mipango yake ni kuendelea kushirikiana na mashirika na wakulima ambao wanalima mazao kwa njia ya kilimo ikolojia hai ili kuhakikisha wanakidhi hitaji la soko.

“Kusema kweli soko la bidhaa za kilimo hai hapa Arusha lipo, kwa sasa tunachopata hakifiki hata nusu ya mahitaji, hivyo nitumie nafasi hii kuwahamasisha wakulima kulima kwa uhakika wa soko,” anasema.

Glen anasema juhudi zinazofanywa na mashirika mbalimbali kama Shirika la Kilimo Endelevu Tanazania kupitia Jarida la Mkulima Mbunifu, Shirika la Islands of Peace (IDP), MVIWAA, TABIO, PELUM kwa kutaja machache, zinapaswa kuungwa mkono na wadau wengine ili kuhakikisha bidhaa za kilimo ikolojia hai zinapatikana muda wote.

Mfanyabiashara na mkulima huyo anasema wakati wa mvua nyingi wamekuwa wakipata bidhaa nyingi na zenye ubora, ila changamoto kubwa ipo wakati wa kiangazi.

Amesema atatumia jarida la Mkulima Mbunifu kuangalia mahali pa kupata bidhaa za kilimo hai za vipando na mifugo kwani zina soko la uhakika.

Anasema asilimia 70 ya bidhaa anazouza anatoa shambani kwake na wakulima wakichangia asilimia 30, hivyo kuwataka waongeze kasi kwenye kilimo hicho.

Glen anasema kutokana na uhaba wa bidhaa bei imekuwa kubwa, hivyo kusababisha watu wenye uwezo na wasomi kuwa ndio wateja wao wakubwa.

Aidha, mkulima huyo amewataka wakulima watunze udongo, ili waweze kuzalisha mazao bora na salama kwa wingi lakini pia kulima kilimo mseto kinachohusisha miti ya matunda na mazao mengine, kwani kinaongeza uzalishaji.

Anaishauri serikali itoe kipaumbele kwenye kilimo hai hasa kwa kuweka mkazo katika elimu ya utunzaji udongo ili kuwezesha viumbe hai vinavyosaidia ukuaji wa mimea kuwepo.

Kilimo ikolojia ni njia ya kilimo inayolenga kuhifadhi mazingira, kuhimiza uendelevu, na kukuza ustawi wa jamii kwa kuzingatia mifumo ya ikolojia na utamaduni wa eneo husika. Ni mfumo ambao unazingatia uhusiano wa karibu kati ya mimea, wanyama, binadamu, na mazingira yao, na kujaribu kuiga mifumo ya asili ili kudumisha bioanuai.

“Kusema kweli soko la bidhaa za kilimo hai hapa Arusha lipo, kwa sasa tunachopata hakifiki hata nusu ya mahitaji, hivyo nitumie nafasi hii kuwahamasisha wakulima kulima kwa uhakika wa soko,” anasema.

Glen anasema juhudi zinazofanywa na mashirika mbalimbali kama Shirika la Kilimo Endelevu Tanazania kupitia Jarida la Mkulima Mbunifu, Shirika la Islands of Peace (IDP), MVIWAA, TABIO, PELUM kwa kutaja machache, zinapaswa kuungwa mkono na wadau wengine ili kuhakikisha bidhaa za kilimo ikolojia hai zinapatikana muda wote.

Mfanyabiashara na mkulima huyo anasema wakati wa mvua nyingi wamekuwa wakipata bidhaa nyingi na zenye ubora, ila changamoto kubwa ipo wakati wa kiangazi.

Amesema atatumia jarida la Mkulima Mbunifu kuangalia mahali pa kupata bidhaa za kilimo hai za vipando na mifugo kwani zina soko la uhakika.

Anasema asilimia 70 ya bidhaa anazouza anatoa shambani kwake na wakulima wakichangia asilimia 30, hivyo kuwataka waongeze kasi kwenye kilimo hicho.

Glen anasema kutokana na uhaba wa bidhaa bei imekuwa kubwa, hivyo kusababisha watu wenye uwezo na wasomi kuwa ndio wateja wao wakubwa.

Aidha, mkulima huyo amewataka wakulima watunze udongo, ili waweze kuzalisha mazao bora na salama kwa wingi lakini pia kulima kilimo mseto kinachohusisha miti ya matunda na mazao mengine, kwani kinaongeza uzalishaji.

Anaishauri serikali itoe kipaumbele kwenye kilimo hai hasa kwa kuweka mkazo katika elimu ya utunzaji udongo ili kuwezesha viumbe hai vinavyosaidia ukuaji wa mimea kuwepo.

Kilimo ikolojia ni njia ya kilimo inayolenga kuhifadhi mazingira, kuhimiza uendelevu, na kukuza ustawi wa jamii kwa kuzingatia mifumo ya ikolojia na utamaduni wa eneo husika. Ni mfumo ambao unazingatia uhusiano wa karibu kati ya mimea, wanyama, binadamu, na mazingira yao, na kujaribu kuiga mifumo ya asili ili kudumisha bioanuai

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *