Jina langu ni Bruno Edward, mkulima kutoka mtaa wa Maheve, mkoa wa Njombe. Mimi ni msomaji wa gazeti la Mkulima Mbunifu ambalo nililipata kutoka kwa jirani yangu ambae anapokea majarida kutoka shirika la CARITAS, jimboni katoliki.
Mimi ni mkulima wa parachichi. Niliona makala ya kilimo cha parachichi katika gazeti, nikavutiwa kusoma kwa umakini zaidi. Nilianza kilimo nikifanya kazi kama msimamizi wa shamba katika shuke ya St. Benedict. Mwaka 2017, nikaamua kuanza upandaji wa miti ya matunda kama maua tu nyumbani katika eneo ndogo. Kati ya hio miche 39 ya kwanza, nilikua na maembe, apple, parachichi na peaches.
Kwa nini parachichi
Nilisoma kwamba kuna uhitaji wa parachichi. Nikaamua kujikita katika kilimo cha parachichi. Watu walinibeza na kuniambia mambo ni yale yale, kwamba ningelima mazao ya kawaida kama vile pareto na chai, ambayo wakati huo yalikuwa yanayumbayumba. Lakini sikusita kuendelea na kilimo cha parachichi. Nilisoma gazeti na kufanya kilimo hiki kwa lengo la kuuza.
Ninafanya kilimo hiki kwa kutumia mbolea za wanyama na katika tuta ninaotesha mbogamboga ambayo inanisaidia kwa chakula nyumbani, pia kwa vijana wanaonisaidia shambani.
Mafanikio
Nimeona mafanikio mengi. Nilipoanza, nilikuwa ninauza parachichi debe moja (kilo 20) kwa TShs 5,000 – 6,000. Baada ya miaka 6, nilipata soko la mkataba. Sasa, ninauza kilo 1 kwa TSh 1,500 – 2,000. Kupitia kilimo hcha parachichi, ninasomesha watoto wangu shule na uchumi wangu umeimarika. Pia, ninamiliki nyumba 4 za kukodisha na magari 2; 1 ya mizigo na lingine la kutembelea.
Ushauri wangu
Ninashauri wakulima wasiwe wanapuuza vitu. Kwa mfano, magazeti kama ya Mkulima Mbunifu yanasaidia sana na huwezi kupata elimu ya bure kama hii. Zaidi, ni muhimu kutokukata tama. Ni vema kuelewa na kufanyia majaribio yaliyomo kwenye jarida ili uweze kufanikiwa.
Nimejifunza kwamba kilimo cha parachichi ni ni mradi wa muda mrefu, ambao unahitaji gharama kubwa za awali wakati wa kupanda, ikifuatiwa na kusubiri kwa miaka 3-5 ili miti ianze kuzalisha. Hivyo, mkulima lazima awe na subira. Ili kupata matunda mazuri, ni muhimu kufanya tathmini kamili kabla ya kuanza na kudumisha shamba lenye afya ambalo hutoa mavuno ya juu kwa miaka mingi.