Nyuki ni wadudu wadogo lakini ni wadudu wenye uwezo wa kutengeneza mazao ya chakula na biashara kama asali na nta. Ufugaji wa nyuki pamoja na kumpatia mfugaji pato lakini pia nyuki husaidia katika kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Baadhi ya wafugaji wa nyuki huwa na matamanio ya kupata faida kubwa kutokana na kazi hii lakini kwa kujua au kutokujua kuna baadhi ya makosa wanayofanya na kuperekea kutofikia ndoto zao katika kazi ya ufugaji wa nyuki.
Katika makala hii nitagusia baadhi ya makosa kumi yanayofanywa na wafugaji wa nyuki wadogo na namna ya kukabiliana nayo.
- Kufuga nyuki kama mradi wa ziada na kuutelekeza
Wafugaji wengi wa nyuki wadogo wamekua wakifuga kwa fahari ya kuwa na mizinga na kuona ni ziada tu, hata wakati mwingine hupita miezi miaka wasikague wala kuhangaika kujua nini kinaendelea katika mizinga
Hili ni kosa kubwa sana kwani nyuki wadogo huhitaji usimamizi wa karibu kujua uendelevu wao, kuweka ukaribu na manzuki yako huwafanya nyuki kuanza kuelewa kuwa wanapendwa na pia huboresha tabia yao kiakili.
- Kutokufahamu njia za kudhibiti wadudu vamizi
Hii huchangiwa na uelewa mdogo pia usimamizi mdogo wa manzuki yako, nyuki wadogo wanaathiriwa sana na wadudu wakiwemo siafu, sisimizi, buibui, vyura, nyigu na wengioneo, elimu inahitajika ikiwa ni mkazo wa elimu ya vitendo kwa wasimamizi juu ya kufahamu njia thabiti za udhibiti wa wadudu vamizi katika manzuki.
- Kushindwa kufahamu namna ya kulisha makundi ya nyuki wadogo baada ya kuyagawanya
Ni wazi kuwa unaweza kuendeleza makundi ya nyuki wadogo kwa kuyagawanya njia hii ni rahisi ila wengi wameshindwa kuijua kwa sababu njia bora ya kuwalisha nyuki wakati wa kugawanya makundi.
Kitendo cha ugawanyaji wa makundi ya nyuki ni kitendo cha kibaologia ambacho huhitaji mfugaji kujua kuwa ugawanyaji wa kundi utapelekea msongo wa mawazo na mshituko kwa kundi la nyuki hivyo basi unahitaji kugawanya kundi la nyuki na kuhakikisha wanapata chakula safi ndani ya mzinga ambacho ni lazima mfugaji akiandae.
Hapa mara nyingi unga wa ugali, asali au sukari huweza kutumika, mfugaji atalazimika kuweka maji katika mzinga mpya kwa kutumia kizibo cha kopo la maji na kukiweka muwa ulitafunwa ndani yake kisha kuweka maji.
- kugawanya kundi la nyuki na kuzivunja seli zenye majana
Ikiwa mfugaji atagawanya kundi kwa kuvunja seli za majana anapelekea kuoza na kuzaliwa kwa viluilui wadogo weupe ambao huwashambulia nyuki wadogo na kuliangamiza kundi
Hii hutokea pia pale ambapo mfugaji hugawanya kundi kubwa na kuliweka kwenye mzinga mdogo hii hufanya kubana kundi na kulifanya lishindwe kujijenga kwa ufasaha hivyo seli za majana huoza na kutoa viluilui waharibifu.
- Kushindwa kutambua ni kundi lipi hufaa kugawanywa
Ugawanyaji wa makundi ya nyuki wadogo huhitaji umakini wa kipekee sana, si kila kundi huweza kugawanyika kumbuka ugawanyaji wa makundi ya nyuki huzingatia sana makundi yaliyojijenga vizuri makubwa, yenye nyuki wa kutosha na waliotengeneza chakula cha kutosha hii hurahisisha kujua kundi unaloenda kuligawanya ni kundi lenye afya na lenye hulka ya uchapakazi.
- Kushindwa kutambua mahali sahihi pakuweka mizinga
Mizinga ya nyuki wadogo huhitaji uangalizi wa karibu na mazingira rafiki, si kila mahali hufaa kuweka mzinga ya nyuki katika nyumba yako eneo lenye kuingiliwa na siafu, sisimizi, kukaliwa sana na nyigu halifai kuweka mizinga ya nyuki wadogo.
Uusiweke mizinga karibu na jiko au kitu chochote kinachotoa moshi au joto kali kwani huweza kuathiri joto la ndani ya mzinga hivyo kupelekea kulainika kwa masega na kumwaga asali, mizinga isiwekwe mahali penye upepo mkali kwani hii hupelekea kuanguka kwa chavua nyingi zinazoletwa kwenye mzinga hivyo kupelekea kukosekana kwa chakula cha kutosha hivyo kusababisha makundi ya nyuki kuhama na kutafuta sehemu tulivu
Epuka kuweka mzinga kando na bati linalovuja kwani kuingia kwa maji katika mzinga hupelekea ukungu na baadae uozo wenye kuathiri kundi la nyuki.
- Kushindwa kutambua msimu bora wa kufanya ugawanyaji wa makundi
Ni wazi kuwa wakati wa neema ya chakula viumbe vyote huweza kuzaliana hivyo basi hata nyuki wadogo mfugaji atambue msimu wa kuwagawanya ni wakati wa chavua za kutosha msimu ambao maua yapo ya kutosha kila mahali.
Katika msimu huu makundi yatagawanyika na kutoa matokeo makubwa ambayo yataambana na urahisi wa kupata chavua na kuendeleza masega kutengeza asali kama akiba ya chakula cha kutosha.
- Kutozingatia kanuni za usafi
Nyuki ni mdudu anayezingatia sana kanuni za usafi ni wazi kuwa ukifungua mzinga wa nyuki utaona namna usafi ulivyozingatiwa basi wakati wa kufikiri kugawanya makundi ya nyuki lazima usafi wa mfugaji uwe wa hali ya juu, mikono ioshwe vizuri kwa sabuni na kuoshwa maji mengi kuondoa harufu na kukaushwa vizuri.
Kifaa chochote kitakachotumia ikiwa ni hive tool (kisu cha kufungulia mzinga) au mzinga wenyewe vya faa kuwa safi kweli kwani la sivyo ni rahisi kueneza magonjwa katika kundi la nyuki.
- Kushindwa kuliweka kundi jipya kama lilivyokuwa kwenye mzinga mama
Ni wazi kuwa kundi la nyuki wadogo hujenga nyumba yake kwa kujishikiza kwenye magome au magogo kwa nyuki wa kwenye magogo na miamba au mizizi fulani kwa wale nyuki wa chini hivyo basi mazingira yale lazima yawekwe.
Vilevile katika mzinga, mzinga mpya ikiwa ni pamoja na kulifanya kundi lining’inie katika mzinga mpya na gundi yake ikipakwa pembezoni mwa miimo ya mzinga mpya zingatia sana harufu kuendana na mzinga mama, kuning’inizwa kwa kundi hili katika mzinga mpya hufanyika kwa kukata vijiti viwili na kuweka chini ndani ya mzinga na kundi la nyuki (nyumba) kuwekwa juu katika vijiti hivyo na pia kushikiza nyumba juu yake, baada ya zoezi hili resini ipakwe katika mdomo wa kuingilia nyuki huku sehemu ya masega ya asali na chavua vikiwekwa sambamba.
- Kutokufahamu Rangi inayopakwa katika mizinga ya nyuki wadogo
Ni wazi kuwa uzuri wa mzinga huchangiwa na rangi inayopakwa lakini sio kila rangi hufaa kupakwa kwenye mzinga kwani rangi za mafuta na harufu kali huwa sio rafiki kwa nyuki katika mzinga.
Rangi katika mizinga ya nyuki wadogo baada ya kutengenezwa kwa mizinga ni vema ukapaka rangi ya maji na ikauke vizuri kwani harufu ya rangi ya mafuta huweza kukaa muda mrefu bila kupoteza harufu yake na hivyo kutokuwa rafiki kwa nyuki wadogo kuweza kuzoea mzinga
Hitimisho
Ili kupata mazao ya nyuki kwa wingi ni lazima manzuki ituzwe kwa kuzingatia usafi na usalama wa makundi yote, pia ni muhimu kutambua maendeleo ya kila mzinga kwa kufanya ukaguzi ili kubaini maendeleo na matatizo yanayosumbua na kudhoofisha kundi hii huperekea kupata mazao kwa wingi, kukaa na makundi yanayoaminika na kwa muda mrefu.
Kwa maelezo zaidi kuhusu makala hii wasiliana na Dauni Ngosengwa Manongi, Mtalaamu wa kilimo Ikolojia na Nyuki Mradi wa wadudu wachavushaji kwa simu namba 0629661063