Uelewa wa mahitaji ya mimea humwezesha mkulima kuchukua hatua kuimarisha udongo ili kulisha mimea na kuongeza mavuno.
Katika kilimo, rutuba kwenye udongo na upatikanaji wa maji ni mambo muhimu ya kuzingatia kwani huweza kuathiri uzalishaji, usalama wa chakula, na wa mazingira.
Hivyo basi, mkulima anapotunza udongo anatarajia kwamba udongo huo utaweza kulisha mimea na kuzalisha mimea, inayoweza kustahimili magonjwa, athari za kimazingira kama ukame, na kuleta mavuno mengi naya hali ya juu.
Uzalishaji wa mazao kwa njia za asili uhakikisha kunakuwepo uzalishaji wa kutosha kwa kutumia malighafi zinazopatikana shambani na kwenye mazingira jirani; hii ikiwa ni pamoja na matandazo, mboji na bila kutifua udongo mara kwa mara, na kupunguza uhitaji wa pembejeo za ziada ambazo mara nyingi zinatumika ipasavyo ama kwa wingi na kuhatarisha afya ya watumiaji wa mazao ya kilimo.
Ongezeko la malighafi za asili husaidia kuimarisha udongo na kufanya kuwepo kwa virutubisho vya kutosha.
Athari kwa udongo
Katika kilimo cha kawaida, udongo hulimwa mara kwa mara jambo linalosababisha uharibifu wa muundo wa udongo na uwiano wa virutubisho. Virutubisho vinapoongezwa kwa kutumia mbolea za chumvi chumvi, hasa kwa viwango visivyofaa, muundo wa udongo unabadilika, rutuba nayo inapungua, uwezo wa udongo kuhifadhi maji pamoja na viumbe hai hupungua.
Hii inapofanyika msimu baada ya msimu, uwezo wa udongo kusaidia ukuaji wa mimea huathiriwa kabisa. Mimea inashindwa kustahilimi uvamizi wa magonjwa na wadudu waharibifu, na mavuno yanapungua msimu hadi ya msimu. Nayo mapato ya mkulima yanadorora kabisa!
Elewa rutuba ya udongo
Rutuba ya udongo hutengenezwa na vitu vitatu muhimu ambavyo ni uasilia wa kibayolojia, kikemia na kifizikia. Kati ya hayo, utunzaji wa udongo unategemea kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kibayolojia.
Viumbe hai wana mchango mkubwa sana katika kuendeleza rutuba ya udongo. Kazi yao kubwa ni kumeng’enya mabaki ya mimea, wanyama na viumbe hai wengine. Mchakato huu husababisha uwepo wa virutubisho, na hewa ya kaboni, ambavyo kwa pamoja hutengeneza rutuba kwenye udongo. Njia rahisi ya kutambua baiyolojia na ufanyaji kazi wa udongo ni kwa kuangalia uwepo wa nyungunyungu (earthworms).
Kujua muundo wa udongo husaidia kuweka usawa kati ya upitishaji wa hewa safi, umwagiliaji na ushamirishaji wa mizizi.
Pembejeo za kilimo hai pamoja na mbinu za kilimo zinazosaidia katika kuzuia kusumbuliwa kwa udongo na kusawazisha upatikanaji wa viumbe hai zinaweza kutumiwa ili kuimarisha udongo na kulinda ardhi.
Udongo wenye rutuba hauwezi kugandamana, hasa wakati wa mvua nyingi, ama kupasuka-pasuka wakati wa kiangazi, una harufu nzuri, una viumbe hai ama unaonyesha uwepo wa viumbe hawa, na mimea huonekana yenye afya.
Vyanzo vinavyopatikana shambani
Mboji
Mboji hasa inayotengenezwa kwa kutumia kinyesi cha wanyama, inaweza kuwa chanzo kizuri cha viumbe wadogo kwenye udongo na virutubisho vyenye gharama ndogo. Unapotumia mboji, changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa imeozavizuri na namna ya kuitumia kwa usahihi.
Ikiwa mchanganyiko uliotumika utengeneza mboji ni ya ubora wa chini, basi mboji hiyo itakuwa na ubora wa chini pia. Hifadhi mboji kwenye kivuli ipigwe na jua au mvua, kwa kuwa hali hii inaweza kusababisha kupotea kwa virutubisho.
Inashauriwa kwamba mboji itumike mara kwa mara ili kuweza kuongeza nitrojeni na malighafi zinazo oza kwenye udongo.
Samadi
Mchanganyiko wa samadi inayotokana na mifugo; ikiwa ni pamoja na ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku n.k inaweza kuwa na uwiano mzuri wa virutubisho vya nitrojeni na aina nyingine. Changamoto kubwa ni upatikanaji wa samadi kwa viwango vingi na kwa ubora wa hali ya juu wakati wote. Ozesha samadi kabla ya kutumia, hasa kwenye mbogamboga ili kupunguza madhara kwenye vyakula.
Mimea inayofunika udongo
Mimea inayotambaa huongeza na kushika virutubisho kwenye udongo, kuongeza malighafi zinazooza kwenye udongo, kuzuia madini (hasa ya naitriti kuzama kwenye udongo), virutubisho kutiririshwa, na mmomonyoko wa udongo. Jambo la muhimu hapa ni kuwa udongo umefunikwa ili kuzuia uharibifu. Inashauriwa kutumia mimea jamii ya mikunde zaidi kwa kuwa husaidia kuchukuwa nitrojeni inayopatikana hewani na kuongeza kwenye udongo. Kwenye maeneo yenye mashamba madogo, panda mikunde inayoweza kutumika kama chakula cha wanadamu au mifugo.
Pia, katika maeneo panapopandwa nyasi ya malisho ya mifugo, inashauriwa kuchanganya mimea jamii ya mikunde na nyasi kwa kuwa nyasi hutumia nitrojeni nyingi sana kutoka kwenye udongo. Hivyo, mikunde husaidia kurudisha nitrojeni na kusawazisha mtiririko mzima wa upatikanaji wa nitrojeni kwenye udongo.
Kumbuka malengo muhimu
- Kuongeza kiasi ya malighafi zinazo oza kwenye udongo
- Kujenga uwepo wa uhai wa viumbe hai kwenye udongo
- Kuwezesha upatikanaji wa madini muhimu; nitrojeni, potasiamu n.k
- Kuboresha muundo wa udongo
- Kuongeza uwezo wa uhifadhi wa maji
- Kujenga mazingira ya udongo wenye uwiano
- Kufifisha magonjwa ya mazao
Hii inafanya udongo kuwa hai, kuwa na mazingira ya udongo wenye uwiano, na kufifisha magonjwa na wadudu waharibifu kwa mazao, na yenye uwezo wa kulisha mimea ipasavyo.
Tutaendelea kukuletea makala zaidi jinsi unavyoweza kuboresha rutuba ya udongo wako ili kuimarisha kilimo hai katika shamba lako. Zaidi ni kuongeza uelewa wako kwa sababu unapojua na kufahama lengo lako basi utakuwa makini kuchukua hatua zinazofaa