Kwa muda mwingi nimekuwa nikisikia kuhusu kilimo hifadhi, lakini sielewi na natamani kufahamu. Mnaweza kunieleza kwa ufupi ni nini maana yake na kinafanyikaje?. Shukuru, Msomaji MkM
Hili ni swali muhimu sana na ambalo bila shaka wakulima wengi wamekuwa wakiuliza na kujiuliza pia. Ni muhimu kufahamu na kufanya kilimo hifadhi kwani itasaidia katika uhifadhi wa mazingira, ardhi na uzalishaji wa mazao mengi zaidi kwa njia salama.
Kilimo hifadhi ni nini?
Hii ni aina ya kilimo ambacho hufanyika kwa kufunika ardhi kwa kutumia masalia ya mazao, au kwa kupanda mazao yanayofunika ardhi hasa jamii ya mikunde kama vile maharagwe, ngwara na kunde huku kikizingatia hasa kutosumbua ardhi.
Pia kilimo hifadhi kinazingatia mzunguko wa mazao kama vile mahindi na maharagwe katika misimu tofauti.
Kanuni za kilimo hifadhi
Kilimo Hifadhi kina kanuni tatu muhimu zinazosaidia kuboresha uzalishaji wa chakula na kutunza udongo wenye afya. Ni kilimo mbadala unaozuia kufyeka na kuchoma, ambapo kwa kufanya hivyo hupunguza rutuba katika udongo na kuchangia kuharibu misitu. Kilimo hifadhi huzingatia:
- Kutosumbua ardhi
- Kufunika ardhi
- Kupanda mazao mchanganyiko
Kutosumbua udongo/ardhi
Mashamba yasiyosumbuliwa yanatunza mboji, yanalinda muundo wa asili wa udongo na kutunza afya ya udongo. Hii inaboresha rutuba ya udongo na uzalishaji.
- Udongo haugandamizwi kama ilivyo wakati ardhi ikipaliliwa.
- Mboji katika udongo inatunzwa.
- Udongo unabaki shambani na hauchukuliwi na maji ya mvua ikinyesha.
- Muda haupotei katika upaliliaji.
Kufunika ardhi
Mabaki ya mazao au mazao funika yanatunza udongo katika shamba na kuhifadhi maji na virutubisho kwa ukuaji wa mazao.
- Kufunika udongo kunahifadhi unyevu unyevu kwenye udongo na kupunguza maji kupotea kutokana na joto wakati wa jua kali.
- Mabaki ya mazao yanaoza na kuweka mboji kwenye udongo.
- Udongo unahifadhiwa na hauchukuliwi na maji wakati wa mvua.
- Magugu ni machache kwa sababu hayawezi kukua wakati udongo umefunikwa.
Kupanda mazao mchanganyiko
Mazao mchanganyiko huzalisha mavuno zaidi na husaidia ikiwa zao moja litatoa mavuno haba basi zao lingine litasaidia kufidia.
Kupanda mazao jamii ya mikunde kabla au pamoja na zao kuu ni vizuri kwa kuboresha afya ya udongo na pia kupata mazao ya mikunde yenye virutubisho na ladha nzuri.
- Mazao mchanganyiko huongeza uzalishaji.
- Mimea jamii ya mikunde (maharagwe, kunde, mbaazi) hurutubisha udongo kwa naitrojeni.
• Hudhibiti magugu na magonjwa ya mazao.
Ni nini faida za kilimo hifadhi?
- Hupunguza mmomonyoko wa udongo.
- Huboresha udongo kwa kusaidia kuhifadhi rutuba kutokana na muozo wa masalia ya mimea yaliyobaki shambani.
- Husaidia kuhifadhi maji kwenye ardhi.
- Hupunguza gharama za uzalishaji.
- Hutumia muda mchache shambani na nguvu kazi kidogo.
Kwa nini wakulima wajiunge na kilimo hifadhi?
- Hii itasaidia walime mashamba yaleyale bila kubadili na kuanzisha mashamba mapya
- Itawasaidia wazalishe chakula zaidi katika mashamba yaleyale
• Itasaidia kuhakikisha kuwa mazao yana udongo, maji na virutubisho vya kutosha na kuhakikisha kuwa udongo haumomonyoki - Itasaidia kuboresha rutuba kwenye udongo na kupata mavuno mengi na ya uhakika.
• Itasaidia kupunguza nguvu kazi na pia kupunguza na kuepuka matumizi ya mbolea za viwandani
Kilimo hifadhi kinapunguzaje mabadiliko ya tabia nchi na athari zake
- Kilimo hifadhi kinasaidia kuongeza na kutunza unyevuunyevu kwenye udongo na kutumia vizuri maji yaliyopo. Hii inapunguza uwezekano wa hatari ya kuharibika mazao wakati wa mvua haba au mvua isipokuwepo.
- Kilimo hifadhi kinaongeza kaboni na mboji kwenye udongo na hivyo kuongeza rutuba kwenye udongo.
- Kwa kuepuka kupalilia na kuchoma moto mashamba, hewa ukaa (gesi chafu) zinapunguzwa hewani.