Ni ukweli usiopingika kuwa, wakulima wengi kwasasa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali jambo ambalo huweza kutatuliwa kwa kutumia njia mbalimbali na matumizi sahihi ya mbolea za asili ikiwemo samadi itokanayo na kinyesi cha popo.
Popo hupatikana katika maeneo mbalimbali kama vile kwenye mapagala, miti, mapango au kwa kujenga banda na kuliegesha shambani kisha popo kuingia na kufanya makazi, na baadaye kutoa kinyesi chao ambacho baadaye mkulima anaweza kukusanya kwa ajili ya matumizi ya kilimo.
Cleophace Mwombeck toka Kijiji cha Vianzi [Morogoro] ni mtaalamu wa kutengeneza mbolea inayotokana na samadi ya popo ujuzi anaosema aliupata miaka kadhaa iliyo pita baada ya kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa ajili ya mazao yake.
Jinsi ya kuandaa/kutengeneza
Kama ilivyo kwa mbolea zingine za asii zinazotumika katika uzalishaji wa mazao mbalimbali, kuna hatua ambazo ni lazima kuzifuata ili kuweza kupata mbolea bora na yenye tija kwa mkulima.
Ili kupata mbolea bora itokanayo na popo huna budi kufaya yafuatayo;
- Chukua samadi ya popo kiroba kimoja ambacho kitakuwa na ujazo wa kilogramu 25.
- Andaa chombo chenye ujazo wa maji kiasi cha lita 200 [yaani pipa].
- Chukua samadi uliyoweka kwenye kiroba kisho dumbukiza kwenye pipa lako.
- Mimina maji mpaka kwenye ujazo wa pipa lako.
- Baada ya hapo funika mbolea hiyo kwa kitu ambacho hakiwezeshi hewa kutoka, lengo ni kulinda virutubisho vilivyomo kwenye mbolea visiondoke.
- Acha kwa muda wa siku tatu ikiwa imefunikwa.
- Siku ya tatu funua na anza kuikoroga na utakuwa unafanya hivyo kila baada ya siku tatu, kufunua, kukoroga na kisha kufunika. Utafanya hivyo kwa muda wa siku 21
Nini hufuata baada ya siku 21
Baada ya siku 21 andaa vyombo vya kuhifadhia mbolea yako vyenye ujazo wa lita 600 ujazo huo ni sawa na mapipa matatu.
Chukua maji lita 400 sawa na mapipa mawili, kisha changanya na mbolea hiyo iliyokuwa imeandaliwa kwa siku 21.
Lengo ni kutaka kupunguza nguvu iliyomo kwenye mbolea ili isije ikaleta madhara kwenye ardhi na kuunguza mazao pia.
Ikishachanganywa kwenye lita 400 na kukoroga vizuri mbolea yako itakuwa tayari kwa ajili kutumika shambani, na unaweza kuiweka kwenye vyombo vidogo vidogo ambavyo itakuwa ni rahisi kubeba wakati wa kupeleka mbolea shambani
Jinsi ya kutumia
Kila mmea utaunywesha mbolea kwa kipimo cha robo ya kikombe kidogo cha chai na mbolea hii hutumika wakati mmea tayari umefikisha siku 21 yaani wiki tatu toka kuoteshwa.
Mbolea hii huweza kutumika kwa mazao ya aina mbalimbali yakiwemo ya mboga na matunda, mazao ya nafaka na mazao mengine yale ya muda mrefu (ya kudumu)
Faida ya mbolea hii
Mwombeck anasema kuwa “tangu nilipoanza kuitumia mbolea hii nimepata mafanikio makubwa katika kuongeza tija ya uzalishaji, lakini si tu kwangu bali hata wakulima wenzangu ambao nimewafundisha wamekuwa wakitoa shuhuda za ufasini wa mbolea ya popo kwenye mazao yao’’.
‘’Nimeweza kupunguza utegemezi wa mbolea, nimekuwa huru na ninaweza kuandaa mashamba yangu wakati wowote kwa kuwa sina changamoto tena ya mbolea na mbolea hii inaweza kudumu katika ardhi kwa takribani miaka kumi’’ aliongeza.
Bw. Mwombeck anaeleza kuwa mbolea ya popo imekuwa msaada mkubwa sana kwake hasa wakati wa mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa inaweza kuufanya mmea na udongo ukawa na unyevu kwa muda mrefu na hivyo kusaidia mazao yasiathirike kirahisi.
‘’Kwa maeneo mengine mbolea ya popo imekuwa na soko kubwa sana na inahitajika kwa kiwango kikubwa mfano kwa Zanzibar kilogram moja ya bidhaa hii inauzwa sh. 1500″ alisema
Wito kwa serikali
‘’Naiomba serikali ijaribu kuunga mkono jitihada za wakulima wadogo wa ambao wanajaribu kuja na teknolojia mbalimbali na rahisi za kilimo hasa pembejeo za asili’’ alisema.
Bw. Mwombeck anasema kuwa, serikali kama itatenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kufanya tafiti za mbolea za asili inaweza kumsaidia mkulima ambaye kila mwaka ana uhitaji mkubwa wa mbolea kwa ajili ya kuzalisha.
Kwa maelezo zaidi kuhusiana na mbolea ya popo wasiliana na Bw. Mwombeck kwa simu namba 0768391947
Nina gunia tano za mbolea ya mavi ya popo, nahitaji mteja. 0764090291
Viwango vya virubisho NPK vikoje kwenye Mbolea ya popo?
Nina mbolea ya popo nahitaji mteja