Siku za hivi karibuni, mradi wa Mkulima Mbunifu uliratibu na kuendesha mafunzo ya kilimo hai kwa waandishi wa habari nchini Tanzania.
Mafunzo hayo ya siku tatu yalifanyika katika shamba la kilimo hai SJS- St Joseph Sustainable Organic Farm lililopo katika kijiji cha Kwanyange Wilaya ya Mwanga.
Mafunzo haya yalifadhiliwa na shirika la Biovision (Bv) Foundation lililopo Switzerland.
Katika mafunzo hayo Austin Makwaiya Makani muwezeshaji akishirikiana na wakufunzi wengine Fredrick Ochieng mratibu wa programu ya mawasiliano Biovision Africa Trust (BvAT) kutoka Nairobi ambapo Mkulima Mbunifu inaratibiwa kiufundi, na Ayubu S. Nnko aliyekua meneja mradi wa Mkulima Mbunifu, Mtaalamu wa kilimo Bw. Jonathan Nalubikya kutoka Shirika la Kilimo endelevu Tanzania (SAT). Hayo yote yalifanikiwa kwa usimamizi wa meneja wa mradi na mhariri mkuu wa jarida la Mkulima Mbunifu (Erica Rugabandana) pamoja na wafanyakazi wenzake Gabriela John na Flora Laanyuni.
Jumla ya waandishi 15 kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania walialikwa na kuhudhuria mafunzo hayo yaliyolenga kufundisha jinsi ya kuandika taarifa elekezi kwa ajili ya kuchapishwa katika Jarida la Mkulima Mbunifu.
Jarida hili limewalenga wakulima wadogo wadogo nchini Tanzania ambao ndio wazalishaji wakuu wa chakula nchini Tanzania. Jarida hili hupokea makala kutoka kwa waandishi mbalimbali nchini Tanzania, pia wataalamu wa elimu ya kilimo hai.
Mbinu mbalimbali za kufanya kilimo hai, uchakataji wa mazao na habari za mafanikio, huchapishwa kumsaidia mkulima kujifunza na kutekeleza ili kufanya kilimo endelevu na chenye tija.
Kilimo hai kina faida nyingi kwa kuwa hakihusishi matumizi yoyote ya kemikali za viwandani, kinahakikisha afya ya binadamu, wanyama, mazingira na mimea.
Kwa kutekeleza kilimo hai mkulima ataboresha uchumi, afya na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.