Mkulima Mbunifu hutembelea wakulima wa kilimo hai popote walipo kujifunza na kunukuu taarifa zao za mafanikio katika utekelezaji wa kilimo hai kwa manufaa ya jamii na wakulima.
Pamoja na kuinufaisha jamii kwa mapana, pia ni fursa kwa mkulima aliefikiwa na MkM kujulikana pamoja na kutangaza bidhaa anazozalisha.
Katika Makala hii, tutajifunza kupitia mkulima mmoja mkoani Arusha, katika wilaya ya Karatu kata ya Mbulumbulu, kijiji cha Slaamo.
Mama Tajieli Paulo (54), ni mkulima na mfugaji ambae ana familia ya watoto watano. Mkulima huyu anajishughulisha na kuzalisha mbogamboga aina ya saro, sukuma wiki na mnafu, kwani mazao hayo huyatumia nyumbani na pia kufanya biashara. Mbali na mazao hayo, pia anajishughulisha na kilimo cha migomba, miwa, mihogo na viazi lishe.
Alianza lini kilimo hai
Tajieli alikua mkulima wa kilimo cha kawaida hadi mwaka 2017 alipojiunga katika kikundi cha kilimo chini ya mradi wa Kilimo Endelevu. Kupitia mradi huo alijifunza kuhusu kilimo cha kiikolojia, ambacho kimempa furasa ya kuelewa ni jinsi gani anaweza kufanya kilimo hai akaboresha uzalishaji na afya kwa familia yake.
Pamoja na kilimo, anafuga mbuzi wa maziwa na kuku, mbolea pamoja na mkojo kutoka kwa wanyama hawa imekua tegemezi kwake kwaajili ya shambani ametumia kurutubisha udongo ili kuzalisha mazao yenye tija .
Majani na mabaki ya mazao shambani huyatumia kulishia mifugo. Hii inadhihirisha ni kwa namna gani mambo haya yanategemeana bila kuhitaji gharama au nyongeza kutoka nje.
Kwanini aliamua kufanya kilimo hai
Tajieli anashuhudia kuwa kilimo hai kinalipa! Anaelezea kuwa, haingii gharama kubwa kama awali kulinganisha na faida anayopata.
Anaelezea, kilimo hiki kimenisaidia kuboresha afya ya familia yangu na mimi mwenyewe kwasababau sasa ninauhakika na ninazalisha mazao salama. Pia mazao haya yamenisaidia kwani nimekua maarufu na mboga yangu inanunuliwa kwa wingi kwakuwa inavutia kwa rangi, na pia watu huniambia ladha yake ni halisi na nzuri. Hapa kijijini watu wamekua wakifata mboga hizo nyumbani kabla sijapeleka sokoni.
Faida ya kilimo hai kiuchumi
“Ninapata faida kwani kwa siku moja kupitia bustani yangu naweza kuuza mpaka shilingi elfu kumi (10,000/- shilingi za kitanzania). Fungu la saro lenye majani /matawi 10 huuza kwa shilingi 200/- za Tanzania. Wateja wangu ni jamii inayonizunguka. Wanapenda mboga ya saro, sukuma na pia Mnavu. Mazao haya yamenisaidia kuongeza kipato ambacho kinanisaidia kujikimu kimaisha na familia yangu” anasema.
Tajieli anapata faida katika mifugo yake, mbali na mbolea na maziwa ya mbuzi, anauza kuku pindi wakiwa wengi huwapunguza kwa kupeleka sokoni. Jogoo mmoja anamuuza hadi shilingi elfu kumi na tano 15,000/- wakati mtetea atamuuza kuanzia elfu saba hadi elfu kumi 7,000 -10,000/- inategemeana na ukubwa. “Hata hivyo watu wameshtuka kuhusu matumizi ya dawa zenye sumu kwenye mboga ndio maana wengi wanakuja kwangu pia kuhakiki shambani” anaongeza Tajieli.
Anawasaidiaje wengine kujifunza kilimo hai
Jamii na majirani wamekua wakienda katika shamba la mkulima huyu kujifunza na wao kujaribisha katika viunga vya nyumba zao.
Kuna maswali mengi kuwa ni jinsi gani ameweza kushindana na wadudu na magonjwa ya mimea kama mnafu na kimamba. Amekua akiwajibu maranyingi kuwa amepulizia kiuatilifu salama chenye mchanganyiko wa Mwarobaini, alizeti pori na kitunguu saumu na wakati mwingine pilipili kichaa. Wadudu wengi wanachukia harufu na hawapendi pilipili.
Kuhusu Mkulima Mbunifu
Kikundi chetu kinapokea jarida la Mkulima Mbunifu kupitia mradi wa kilimo endelevu, ninalipenda sana jarida hili kwani limesheheni taarifa nyingi za kilimo hai. Sisi husoma kwa kupokezana na mtu kama ana swali huwauliza wataalamu wetu wa kilimo endelevu. Tunaomba tuendelee kupokea jarida hili bila kukosa.
Ushauri wake
Ninachoweza kuwashauri wakulima wenzangu ni kwamba tusiwe na tamaa ya kutaka mazao ya haraka kwa kutumia dawa za kemikali. Afya kwanza, hivyo wazalishe mazao kwa mbinu za kilimo hai.