Ni kwa namna gani udongo unaweza kufunikwa wakati wote, wakati shughuli nyingine zinaendelea kwenye udongo huo huo?
Hili ni swali muhimu wanalojiuliza wakulima wengi. Hii inategemeana na utunzaji na aina ya shughuli zinazofanyika kwenye udongo huo, na kama shughuli zenyewe zinafanyika kwa kutumia mikono au mashine. Moja ya shughuli ambazo zinasumbua udongo kwa kiasi kikubwa ni kulima kwa kutumia plau. Na pia inategemea na uelewa, tunaposema kufunika udongo.
Uelewa wa sababu ya kufunika udongo ni muhimu sana. Baada ya kufanya mambo yote tunafunika udongo ili kuzuia mmomonyoko, virutubisho kutoweka, kukauka, kupasuka na mengineyo.
Hili linaweza kufanyika kwa njia mbalimbali
- Kwa kutumia mimea inayotambaa, ambayo mara nyingi huwa tunaipanda.
- Kwa kutumia matandazo, ambayo yanaweza kuwekwa chini ya shina la mimea au kutandazwa kwenye ardhi ambayo bado haijalimwa.
- Kuweka kivuli kwa kutumia turubai.
- Kivuli cha miti. Kila njia inatofautiana kulingana na mahitaji na uwezo wa mkulima. Katika hali kama hii mkulima anaweza kuacha kabisa kutifua udongo, ambapo katika sehemu kama hiyo udongo ubaki ukiwa umefunikwa siku zote kutokana na mabaki ya mazao yaliyovunwa kabla ya kupanda mengine.
Kulima kwa jembe la kukokotwa na wanyama
Sehemu ambayo ardhi imelimwa kwa kutumia plau matandazo huondolewa au kusogezwa. Hata hivyo, inapendekezwa kufunika udongo mara moja, ili kuepusha mmomonyoko, au upotevu wa virutubisho pamoja na udongo kukauka. Wakulima walio wengi katika nchi zinazoendelea wanageukia kulima sehemu ambayo ilikuwa haitifuliwi, ambapo wanatumia trekta, plau na hata kupanda kwa kutumia harrow. Hii inasemekana kuwa inarahisisha kazi ikiwa ni pamoja na kupata mavuno mengi.
Ardhi isiyolimwa/tifuliwa
Ardhi isiyotifuliwa hupunguza gharama, kulinda udongo, pamoja na kuongeza mavuno. Magugu hufifishwa, hivyo hupunguza gharama za kupalilia; rutuba ya udongo huongezeka, hivyo kuwa na mazao yenye afya, viumbe hai kwenye udongo huongezeka na hivyo kujenga muundo mzuri zaidi wa tabaka za udongo, ambao una uwezo wa kukabiliana kwa kiasi kikubwa na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Uzalishaji wa mazao unatuhitaji kuweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi. Kuulinda udongo ambao ni rahisi kuharibiwa ni lazima.
Punguza kuutifua udongo, zuia magugu
Kila gramu moja ya udongo ina mamilioni ya mbegu za magugu. Ili mbegu iote inahitaji kupata mwanga na jua. Kulima inasaidia kugeuza mbegu zilizokuwa zimefukiwa kwenye udongo kuwa juu na hivyo kuzifanya ziote. Hivyo kutifua udongo husaidia kuongeza magugu shambani.
Kwa upande mwingine, kuweka matandazo shambani husaidia kuzuia mwanga kufikia ardhi, hivyo kuzuia magugu kuota. Kuacha kulima huku ukifunika udongo kwa matandazo, husaidia kuzuia magugu hivyo kuondoa gharama ya muda na nguvu kazi ya kufanya palizi, na kuwa na udongo wenye afya.
Muhimu: Kulima huharibu viumbe hai wadogo waliopo kwenye udongo ambao wana faida kwa ufanisi wa udongo.
Kulima huharibu viumbe hai waliomo kwenye udongo
Kutifua udongo ni sawa na kioski kilichoharibiwa. Wateja watakuja wakati wa mahitaji, lakini kwa bahati mbaya biashara ilishaharibiwa na haiwezekani kupata mahitaji kutoka kwenye hicho kioski. Aina tofauti ya viumbe hai muhimu huishi katika matabaka tofauti ya udongo. Tunapotifua udongo si tu kuwa tunaweka mbegu za magugu juu na kuzifanya ziote, lakini pia tunaharibu hali ya viumbe hai walio muhimu kwenye udongo. Matokeo yake ni kuwa udongo utahitaji kuboreshwa kabla ya kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
Udongo uliokauka unaweza kuhitaji kutifuliwa kidogo ili kuruhusu hewa kuingia, lakini hatua hii pia inaweza kuachiwa viumbe hai wadogo kwenye udongo kuifanya. Kunyunyizia kemikali kwenye mimea huuwa wadudu muhimu kwenye udongo na hivyo kusababisha gharama isiyohitajika kwa mkulima. Mkulima mzuri hujenga mazingira mazuri ya hawa wadudu kuendelea kuwepo kwenye udongo.
Udongo na mazao
Inafaa wakulima kutunza na kuhifadhi udongo, wakati anapanda mazao. Tukiutunza udongo vizuri, mazao pia yatakuwa na hali nzuri. Tusipouweka udongo katika hali nzuri, ni dhahiri pia mazao yetu yatakuwa na hali mbaya.
Mboji huboresha rutuba ya udongo
Utengenezaji wa mboji unahitaji nguvu kazi kubwa. Maandalizi yanahitaji muda, na mbolea inakuwa rundo, jambo ambalo linasababisha usafirishaji na matumizi kuwa magumu. Bado ukiwa kama mkulima mdogo, ni lazima uthamini ubora na faida zinazopatikana kutokana na mboji kwa kuwa ina virutubisho vingi ambavyo huwepo kwenye ardhi na baadaye kuchukuliwa na mimea kwa matumizi yake.
Lakini faida kubwa ya mboji ni kuongeza kiasi cha malighafi za asili zinazooza kwenye udongo, ambazo huboresha muundo wa udongo, uwezo wa kuhifadhi maji, na kusaidia viumbe hai waliomo kwenye udongo kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya mizizi ya mimea. Malighafi zinazooza husaidia kupunguza asidi kwenye udongo, jambo ambalo husababishwa na matumizi ya mbolea zisizo za asili mara kwa mara.
Endapo mboji itatumika mfululizo miaka mitatu, huweza kujenga rutuba ya udongo kiasi kwamba mkulima atahitaji kuongeza kiasi kidogo sana cha mbolea ili kuimarisha rutuba kwenye udongo. Mkulima anaweza kuandaa mboji kiasi kingi awezavyo kutegemeana na upatikanaji wa malighafi zinazohitajika kwa kazi hiyo.