Maji ni uhai na bila maji, vitu vilivyo hai duniani haviwezi kuishi. Binadamu, mimea na wanyama wanahitaji maji safi ili kuwa na afya nzuri hivyo tunapaswa kuhakikisha tunatumia maji safi ya kunywa, kupika na hata kwa wanyama na mazao.
Imekuwa kawaida kuona watu wakitembea na chupa za maji ya kunywa. Mbali na hali ya hewa kuwa na joto, umewahi kujiuliza faida ya maji katika mwili wa mwanadamu ni ipi? Kweli, maji huchangia kati ya 50-75% ya uzito wa mwili wako na ni ya muhimu, na kwa sababu hii imeitwa chanzo cha maisha.
Mtu mwenye afya ya kawaida anaweza kuishi hadi wiki 3 bila chakula lakini siku 3 hadi 4 tu bila maji. Hii ni kwa sababu mwili hauwezi kuhifadhi maji na unaendelea kupoteza maji iliyo kwenye seli zake kupitia mmeng’enyo wa chakula, kupumua na kutokwa jasho. Hivyo, ni muhimu kurudisha maji mwilini, kwa kunywa maji safi.
Kwa matumizi ya binadamu, maji yanapatikana katika aina mbili: maji ya kawaida tunayokunywa na ile iliyo ndani ya chakula na ambayo mwili inapata tunapotumia chakula.
Kiasi cha maji katika vyakula
Ingawa inashauriwa sana kunywa na kutumia maji ya kawaida, bado asilimia 20 ya maji inayotumiwa na miili yetu kila siku hutoka kwenye vyakula ambavyo tunakula. Ikiwa mtu hajisikii kunywa maji, bado anaweza kupata maji kupitia vyakula vyenye asilimia kubwa ya maji.
Katika orodha hii ya vyakula ni matango ambayo yana karibu 96.7% ya maji, nyanya (94.5%), pilipili hoho (93.9%), cauliflower (92.1%), tikiti maji (91.5%), spinach (91.4%), strawberry (91.0) %), brokoli (90.78) na karoti 90%.
Mahitaji ya maji kwa makundi tofauti
Inashauriwa mtu mzima kutumia glasi 8 za maji ambazo ni sawa na lita 2 kila siku, lakini kiwango cha matumizi ya maji kinategemea mambo kama vile umri, jinsia na afya ya mwili kwa ujumla.
Mwili ukiwa hali ya juu kiafya, unywaji wa kila siku unaopendekezwa kwa makundi tofauti ni kama ilivyoorodheshwa hapa chini;
Kundi | Umri | Kiasi ya maji kwa siku (mili-Lita) | |
Watoto wachanga | Miezi 0 – 6 | 680 kupitia maziwa ya mama | |
Miezi 6 – 12 | 800 – 1,000 | ||
Watoto | Mwaka 1-2 | 1,100 – 1,200 | |
Miaka 2-3 | 1,300 | ||
Miaka 4-8 | 1,600 | ||
Miaka 9-13 | Wavulana | 2,100 | |
Wasichana | 1,900 | ||
Zaidi ya miaka 14 | Sawa na watu wazima | ||
Watu wazima | Wanawake | 2,500 | |
Wanaume | 2,000 | ||
Waja wazito | 2,800 | ||
Wanaonyonyesha | 3,100 – 3,200 | ||
Wakongwe | Sawa na watu wazima |
Wakati wa kunywa maji
Watu wanaoishi maisha ya kukaa tu (katika miji, makazi duni na makazi mengine), wale wanaoishi katika maeneo baridi na wale wanaotumia vyakula vyenye maji mengi wanaweza kunywa maji kidogo.
Watu walio na hali zifuatazo watahitaji kunywa maji mengi kwa siku;
- Wanaokula chakula chenye protini nyingi.
- Wanaofanya mazoezi ya mwili.
- Walio kwenye sehemu za joto.
- Mama wajawazito / wanaonyonyesha (mili-lita 750 – 1,000 kila siku kutokana na mahitaji ya kimsingi ya mwili).
- Wanaotapika au wenye kuharisha.
- Wanaokula chakula chenye nyuzi nyingi kwani inasaidia kuzuia kuvimbiwa.
Faida za kiafya za maji
Faida za kiafya za maji kwa mwili ni nyingi na ni pamoja na;
- Udhibiti wa joto la mwili kwani maji ambayo huhifadhiwa kati ya tabaka za mwili na ngozi huja juu ya ngozi, hubeba joto kutoka ndani ya mwili na husaidia kuipoza.
- Inalinda tishu, uti wa mgongo na viungo. Maji yanahusika katika utengenezaji wa homoni na mishipa ambayo ni muhimu kwa muundo na utendaji wa ubongo.
- Husaidia katika utoaji wa uchafu mwilini. Maji yanahitajika katika kutoa jasho, mkojo na kuondoa kinyesi ambayo yote ni sehemu ya michakato ya kutoa uchafu.
- Husaidia katika kunyonya virutubisho. Maji husaidia katika ufyonzwaji wa virutubisho na madini yanayopatikana kwenye chakula na kuyafanya yaweze kufikia sehemu tofauti za mwili.
- Husaidia katika kupunguza uzito. Maji yanaweza kusaidia kupunguza uzito wakati yanatumiwa badala ya juisi na soda. Mkakati mwingine ambao husaidia kupunguza uzito ni ule wa kuunywa maji mengi kabla ya kula. Hii husaidia kuzuia kula kupita kiasi kwa kuleta hisia ya kushiba.
- Husaidia kuzuia kuvimbiwa. Wakati mwili unapata maji ya kutosha, uwezekano wa kuvimbiwa huwa mdogo kwani maji huwezesha urahisi wa kutolewa kwa kinyesi kutoka kwenye utumbo mkubwa (koloni) na kupunguza uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.
- Maji hutumika katika kuunda mate. Mate husaidia kusaga chakula na huweka unyevu kwenye kinywa, pua, na macho. Hii inazuia msuguano na uharibifu. Maji ya kunywa pia huweka kinywa safi. Ikitumiwa badala ya vinywaji vyenye utamu basi inapunguza kuoza kwa meno.
- Maji huboresha mzunguko wa oksijeni mwilini. Maji yanajumuisha hidrojeni na oksijeni na wingi wake mwilini husaidia katika mzunguko wa oksijeni kupitia damu ambayo ni asilimia 90 ya maji.
- Maji hutumika katika usafirishaji wa virutubisho katika mwili wote wa binadamu.
- Maji ni muhimu katika kupambana na magonjwa. Maji huongeza oksijeni kwenye damu na kutoa sumu. Pia, husaidia viungo kama macho na mdomo kubaki na unyevu na kutoa uchafu ambao unaweza kusababisha maambukizi.
- Inaboresha utendaji wa mwili. Upungufu wa maji mwilini unaweza kusababisha uchovu, kupungua kwa motisha, na mabadiliko ya mhemko. Kwa hivyo, matumizi ya kiwango cha kutosha cha maji ni muhimu sana kuboresha viwango vya nguvu mwilini.
- Maji huzuia uharibifu wa figo. Mwili usipopata maji ya kutosha kuna uwezekano wa kusababisha mawe ya figo, na shida zingine.
Muhimu: Hakikisha mwili wako unapata maji ya kutosha yaliyo safi na salama kila siku.