Ni muhimu kujua baadhi ya mambo ambayo husababisha maziwa kuharibika ili uweze kuzuia hasara zisizokuwa za lazima. Maziwa yana virutubisho vingi sana. Kwa sababu hiyo, bakteria waharibifu huweza kukua kwa haraka kwenye maziwa.
Kwa wasafirishaji wa maziwa, nii muhimu kufahamu vyema jinsi maziwa yanavyoweza kuharibika haraka kama hayatatumika na kuhifadhiwa vizuri au hayatasafirishwa kwa haraka. Ni muhimu kuwa na uelewa wa kutosha juu ya misingi bora wakati wa kusafirisha maziwa na kwenda kuyauza kwa wateja.
Vyombo vinavyoruhusiwa kwa kutunzia maziwa
Ni muhimu kuhakikisha maziwa yanakuwa bora wakati wa kutunza na kusafirisha ili kupunguza upotevu na uharibifu:
- Vyombo vyote vya kutunzia maziwa vinatakiwa kuwa safi na vimetengenezwa kwa kutumia aluminiamu, chuma kisichopata kutu na plastiki maalum. Vyombo hivi ni rahisi kusafisha.
- Mahali pa kuhifadhia maziwa panatakiwa kuwa safi, pasipokuwa na wadudu.
Pawe na hewa na mwanga wa kutosha na ambapo vumbi, mionzi ya jua na mvua haingii.
- Maziwa yasihifadhiwe katika chumba kimoja na mazao ya kilimo (k.m. kabichi, vitunguu, pumba, n.k) au kemikali kama vile rangi au mafuta ya taa ambavyo hutoa harufu.
- Safirisha maziwa haraka iwezekanavyo.
- Uchelewaji katika kusafirisha maziwa kwenda kituo cha kukusanyia au kiwandani kutasababisha maziwa yaliyokuwa mazuri kuharibika. Maziwa yasafirishwe kwenda kituoni au kiwandani kabla ya saa 3 baada ya kukamuliwa.
Vyombo vinavyoruhusiwa kwa kusafirishia maziwa
Vyombo vinavyoruhusiwa kusafirishia maziwa kiasi kidogo cha maziwa ni alumini, chuma kisichopata kutu na plastiki maalum. Aina ya vyombo hivi inakubalika katika uhifadhi wa maziwa ya kunywa pia ni imara na rahisi kufanyiwa usafi kwa kuosha kwa maji moto na kufukizwa. Chombo cha kusafirishia maziwa kiwe na mfuniko unaofunga vizuri kuzuia maziwa kuchafuka na kumwagika.
Usafirishaji wakiasi kikubwa cha maziwa unahitaji matenki makubwa maalum yanayohifadhi ubaridi. Matenki haya ni ghali na yanahitaji vifaa vingine zaidi kama pampu ambavyo pia inabidi visafishwe kwa njia maalum.
Usafi wa vyombo vya kusafirishia maziwa
- Vyombo vya kusafirishia maziwa havinabudi kusafishwa ipasavyo kwa sababu maziwa huweka mazingira mazuri kwa bakteria kuongezeka haraka.
- Vyombo vioshwe kwa sabuni na dawa ambayo haiharibu vyombo.
- Kuosha na kufukiza ni muhimu kufanywa kwa pamoja; kwani njia moja pekee haitoshelezi malengo ya usafi, ambayo ni kuondoa mabaki yote ya maziwa.
Kwa maelezo zaidi, rejea mwongozo wa kufundisha wasafirishaji wa maziwa Afrika Mashariki. ASARECA, 2006