Nchini Tanzania, kilimo si kazi tu, ni sehemu ya maisha ya kila siku. Kilimo kinatoa ajira kwa takribani asilimia 80 ya Watanzania na kuchangia takribani asilimia 30 ya pato la taifa. Kiasi kikubwa cha chakula chetu kinazalishwa na wakulima wadogo. Hata hivyo, licha ya mchango wao mkubwa, wakulima hawa hukumbwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na udongo kupoteza rutuba, hali ya hewa isiyotabirika, bei zisizo na uhakika sokoni, na ukosefu wa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu kilimo.

Hii ni moja ya sababu kubwa ya Mkulima Mbunifu (MkM), kutafuta suluhisho kwa maswala yanayowakumba wakulima wadogo, kuwapa maarifa ya kilimo ili kupanua uzalishaji na kuinua hali ya maisha.
Mradi wa MkM unatoa maarifa ya kilimo yanayofanya kazi, na hili limethibitishwa na wakulima wanufaika wa mradi huu. Wakulima hawa wanatoa ushuhuda wa kuongezeka kwa mavuno na mapato, kukidhi mahitaji ya chakula safi na salama kwa familia, na kuboreshwa kwa mazingira kupitia mbinu sahihi na endelevu shambani.




