- Kilimo, Udongo

Matumizi ya mabaki ya mimea na wanyama katika kurutubisha udongo na kupelekea uzalishaji bora wa mazao

Sambaza chapisho hili

Je, unafahamu kuwa unatakiwa kujua sifa za udongo ulio katika shamba lako na changamoto zake? Je, udongo una upungufu wa naitrojeni? Je, una upungufu wa fosiforasi? Je, kuna uwepo wa mabaki ya miti au wanyama ya kutosha?

Ikiwezekana, udongo huo upimwe na mtaalamu au afisa kilimo ili kuonyesha kwa usahihi udongo una mapungufu ya virutubishi vipi na nini kifanyike ili kuweza kurejesha.

Ni muhimu kufahamu kanuni hizi za msingi

Ikiwa mimea ina majani ya rangi ya njano, basi kuna uwezekano kuwa udongo wako una upungufu wa naitrojeni hivyo unapaswa kuongeza kupitia kwenye mbolea ya mabaki ya majani/miti au malisho ya wanyama.

Ikiwa mimea ina rangi ya zambarau, kuna uwezekano kuwa udeongo una upungufu wa fosiforas hivyo unatakiwa kuongeza mbolea ya mabaki ya miti na wanyama iliyo na fosiforas nyingi kama vile majani ya mashina ya mualizeti nk.

MUHIMU: Ifahamike kwamba majani ya mimea huweza kuwa na rangi ya manjano au zambarau kwasababu ya kujaa maji, kushindana na magugu, magonjwa au kwasababu nyinginezo hivyo ni muhimu kuonana na mshauri au mtaalamu wa kilimo mara kwa mara na kwa uchunguzi zaidi.

Mbolea za mabaki

Wakulima wana vyanzo mbalimbali vya mbolea inayotokana na mabaki wanayotumia katika kuhakikisha udongo unadumisha rutuba yake. Vyanzo hivi hutokana na aidha mimea wanayokuza, samadi, miti iliyooteshwa, magugu yanayopatikana katika ukingo wa mashamba nk.

  1. Mimea

Njia bora ya kutumia mabaki ya mimea hutegemea aina ya chembechembe inayopatikana katika mabaki hayo. Mimea huwa na chembechembe za aina tatu ambazo huifanya iwe mbolea nzuri nazo ni naitrojeni, lignin na phenol.

Naitrojeni

Mimea yote huhitaji naitrojeni ili kukua. Mimea hupata naitrojeni kutoka kwenye udongo na huhifadhi katika matawi, mashina na mizizi.

Kuna aina ya mimea inayopata naitrojeni kwa urahisi ama kutoka kwenye udongo au kwenye hewa na kuna aina nyingine ya mimea isiyoweza kupata naitrojeni hiyo kwa urahisi. Kwa mfano; mualizeti una uwezo mkubwa wa kupata naitrojeni kutoka kwenye hewa lakini mhindi hauna uwezo huo.

Mimea kama jamii ya mikunde hujitengenezea naitrojeni kutoka katika hewa. Maharage, choroko ni moja ya mimea yenye mbolea nzuri sana ya naitrojeni n ani mimea mizuri kupandwa katikakati ya mimea mingine kwani huongeza naitrojeni kwa wingi kwenye udongo na pia huhifadhi katika mashina na majani yake.

Kwa ujumla unaweza kutambua ikiwa mmea una naitrojeni ya kutosha kutokana na rangi ya majani yake. Ikiwa kuna majani ya kijani iliyokolea basi mmea una naitrojeni ya kutosha na ikiwa majani ni ya rangi ya njano basi kuna upungufu wa naitrojeni.

Mabaki ya mimea ya rangi ya kijani huwa mbolea nzuri sana huku ya rangi ya njano ikiwa ni mbolea hafifu/ duni.

Lignini

Hii ni chembechembe katika mmea zinazoufanya uoze kwa haraka. Kuna mimea ambayo inaponyauka inaoza kwa haraka na kuingiza virutubishi vyake kwenye udongo katika kipindi cha siku chache. Mimea mingine huoza polepole na kwa hivyo virutubishi vyake hutolewa taratibu. Kwa ujumla, mimea inayooza kwa haraka huwa mbolea nzuri ya mabakii kwasababu mazao huwezxa kutumia virutubishi vyake mapema sana.

Mimea yenye mashina makubwa huwa na lignini. Ijapokuwa mimea yote huwa na lignini lakini mimea ambayo mabaki yake huoza taratibu huwa na lignini nyingi. Mimea hii haiwi mbolea nzuri ya mabaki na mara nyingi mimea hii ni ile iliyokomaa sana.

Ili kufahamu kama mimea ina lignini nyingi, unaweza kuchukua jani na kulichana katikati kwa kutumia vidole vyako, ikichanika kwa urahisi basi lignini yake ni kidogo na likiwa halichaniki kwa urahisi basi mimea hiyo ina lignini nyingi.

Phenol

Hii ni chembechembe katika mmea zinazoufanya uoze polepole. Mmea ulio na phenol hauwi mbolea nzuri ya mabaki. Unaweza kufahamu kama mmea una phenol nyingi kwa kuuonja na ukiwa na ladha ya uchungu basi unawezekana una phenol nyingi na hautakuwa mmea mzuri wa mbolea ya mabaki.

Sehemu tofauti za mmea huweza kuwa na kiwango tofauti za chembechembe hizi kwa mfano mashina yanaweza kuwa na chembechembe hizi lakini majani yakawa hayana hivyo majani yatafaa kuwa mbolea ya mabaki.

Mara nyingi chembechembe hizi hutegemea mahali mmea ulipopandwa mfano mmea uliopandwa mahali penye uvuguvugu, mvua ya kutosha na udongo wenye rutuba utakuwa na kiwango tofauti cha chembechembe hizi ukilinganisha na mmea huo huo ukipandwa mahali pakavu na penye udongo usiokuwa na rutuba.

Ubora wa samadi ya wanyama hutegemea zaidi kile kilicholiwa na mnyama. Ikiwa wamelishwa chakula duni au nyasi zilizomea katika udongo usio na rutuba, basi samadi yao pia itakuwa na ubora duni.

Ikiwa wanyama wamelishwa chakula kizuri basi samadi pia itakuwa bora na iliyojaa virutubisho.

  1. Samadi toka kwa wanyama

Samadi huhitaji kupevuka kwa majuma au miezi kadhaa kabla ya kuwa tayari kutumiwa mashambani kama mbolea. Hata hivyo kiwango cha naitrojeni kilichomo katika samadi hiyo hupungua muda unavyopita kwa kupotelea hewani au kufagiliwa mbali na maji ya mvua.

Ili kuzuia hili kutokea, unashauriwa kuiweka samadi katika shimo, au pipa iliyofunikwa kabla ya kupeleka na kuitandaza shambani.

Samadi iliyochanganywa na mkojo kwa mfano ikiwekwa katika shimo ambamo kuna tope laini huwa na kiasi kikubwa cha naitrojeni kuliko samadi yenyewe.

Hata hivyo, naitrojeni iliyo katika mkojo hupotea kwa urahisi hivyo funika shimo hilo la tope ili kuzuia upotevu huu. Hata kama samadi ipo katika hali duni, bado inakuwa mbolea nzuri hivyo unapaswa kuitumia.

Kwa ujumla, samadi ya nguruwe na kuku huwa bora zaidi kuliko ya ng’ombe na mbuzi lakini unaweza kuitumia samadi ya ng’ombe kwa kuichanganya na samadi ya wanyama wengine.

Namna ya kutumia mabaki ya mimea na samadi ya wanyama

Wakulima huweza kuchagua njia ya matumizi ya mabaki ya mazao mbalimbali kwa kufanya yafuatayo;

  • Kuchagua mabaki kutoka katika aina tofauti ya mimea kama vile miti na masalia ya mazao.
  • Kuchagua mabaki ya mimea kutoka sehemu mbalimbali ndani ya shamba au nje ya shamba.
  • Kutumia mabaki moja kwa moja shambani au kuyarundika na kuzalisha mbolea kisha kutumia.
  • Kuchanganya mabaki ya mimea ya aina mbalimbali kwa pamoja.
  • Kuweka mabaki ya mimea juu ya udongo kama matandazo au kuchanganya na udongo wakati wa kulima shamba.
  • Kuweka mabaki juu ya shamba na kuacha kabla ya kulima.
  • Kutumia mabaki kama mbolea kwa mazao yanayohitaji virutubishi kwa wingi kama vile mboga au mazao makuu kama mahindi.
  • Mara baada ya kufahamu ubora wa mabaki unayohitaji kutumia ni lazima sasa uamue jinsi ya kuyatumia kutegemeana na aina ya mabaki kama miti.
  • Unaweza kuchanganya mabaki yayo katika udongo na ukatumia kama mboji au ukaweka juu ya udongo kama matandazo.
  • Ni vizuri kutumia mabaki yaliyobora moja kwa moja kama mbolea katika udongo na kwa aina nyingine ya mabaki kama mabua ya mahindi ni bora yatengenezwe mboji kwanza au yachanganywe na mbolea kabla ya kuwekwa shambani.
  • Aina nyingine ya mabaki kama vile mashina na matawi hayawezi kuwa mboji kwasababu ina uwingi wa mitimiti hivyo ni muhimu kutumika kama kizinga mmomonyoko wa udongo na kusaidia kuhifadhi unyevu wa ardhi.
  • Ikiwa kuna mabaki yenye ubora na yaliyo duni, ni vyema kuchanganya kabla ya kuweka shambani. Changanya mabaki ya mimea na mabaki ya wanyama ili kuweza kustawisha rutuba ya udongo.

Makala hii imenukuliwa katika kitabu cha mwongozo wa nyanjani wa kilimo cha kujitosheleza kwa Afrika ya Mashariki na Kusini.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *