Napenda kuchangia kipengele cha matumizi ya mbolea za asili toka Jarida la mkulima mbunifu toleo la 3 Novemba 11 na Moduli ya 11.
- Kusanya mifupa, pembe au kwato kutoka kwenye bucha, hotelini, machinjio, mabandani na nyumbani kwako.
- Rundika kisha choma moto. Kwa kawaida mifupa huwaka kwa urahisi sana na kwa muda mfupi.
- Baada ya kuungua, acha mifupa, pembe au kwato zipoe.
- Ponda ponda malighafi hiyo kwa kuweka kwenye gunia au mfuko, kisha unapigapiga na fimbo nzito au kutwanga kwenye kinu hadi iwe laini kama unga wa kawaida tayari kwa kutumia.
Mbolea hii ina madini mengi ya chokaa na fosiforasi ni nzuri kwa ukuaji wa mimea.
Jinsi ya kutumia
Wakati wa kupanda mimea ya aina yoyote, tumia kizibo cha soda au bia.
Fukua sehemu ambayo mche utapandikizwa kisha tia mbolea hii kifuniko 1 na uchanganye na udongo ndipo upande mche.
Endapo unapanda mbegu za aina yoyote, inabidi kuchimba shimo la kupanda, weka mbolea halafu funika mbolea na udongo kisha weka mbegu na ufunike kwa udongo.
Kupanda miche ya matunda au miti ya aina mbalimbali ni kama upandaji wa miche ya mboga isipokuwa kiasi ni vifuniko 3 – 4 vya soda.
Nawatakia wasomaji wenzangu matumizi mema ya mbolea za asili na muendelee kufuatilia mada mbalimbali za MkM.
Sista Veronica Mdendemi OSB. Ofisi ya Caritas, Njombe. Simu: 0768093854