- Binadamu, Kilimo, Kilimo Biashara

Kilimo ikolojia kimeniongezea tija katika uzalishaji

Sambaza chapisho hili

Mbegu bora ya asili huchangia pakubwa katika usalama wa chakula na lishe kwa familia na jamii kwa ujumla. Hii inaambatana na matumizi ya mbinu bora za kilimo endelevu ili kumhakikishia mkulima uzalishaji wa juu nyakati zote na kwa muda mrefu.

“Kabla ya kushiriki katika mradi wa CROPS4HD (Mazao yenye afya yasiyopewa kipaumbele), Mama Regina Mrope, kutoka Kijiji cha Mpindimbi, Masasi, Mkoani Mtwara, alikumbana na changamoto nyingi katika uzalishaji. Alikuwa akifanya kilimo cha mazoea akizalisha mazao ya asili yasiyotoa mavuno mengi huku akikosa mbegu bora na kutumia mbinu finyu za kilimo.

Hata hivyo, maisha ya Mama Regina yalibadilika baada ya kuwa moja ya wanufaika wa mradi wa CROPS4HD, ambao ulilenga katika utafiti na maendeleo, ikiwemo mbegu za mikunde ya Bambara kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Badala ya kutegemea mbegu bora pekee, mradi huu ulilenga mbegu ambazo zimezoleka kwa wakulima na huendana na mazingira ya kila eneo. Mradi ulimpa Mama Regina mafunzo na rasilimali za jinsi ya kusimamia na kuzalisha mbegu hizi za asili kwa ubora zaidi, ikiwemo njugu Myeupe-1, Tanbam, Mnyao mkubwa, Nalbam 4, njugu nnyeupe-2, Ifunda, na Bahi nyeupe.

Mama Regina anasema kuwa mafunzo haya yalimsaidia kupata ujuzi mpya katika uteuzi na uchaguzi wa mbegu, kuzalisha mbegu, na mbinu bora za kilimo endelevu. Kwa kutumia ujuzi huu, aliboresha kilimo katika shamba lake na kuwa msimamizi wa mbegu katika jamii yake. Moja ya majukumu yake ni kuhakikisha mbegu hizi za kipekee zinahifadhiwa na zinapatikana kwa wakulima wengine.

Mafanikio ya bahi nyeupe

Miongoni mwa aina za mbegu alizotumia ni Bahi nyeupe ambayo ni nzuri kwa ladha na ina uwezo wa kustahimili mazingira mbalimbali. Aina hii ya mbegu ilifanya vizuri katika ardhi yake na kuleta mavuno mengi. Kwa sasa, mbegu hii ni maarufu kwa matumizi mbalimbali kama kupika ugali, chapati, na kuongezea ladha kwa mchele.

Mama Regina alifanikiwa kuuza yake ya ziada na kupata kipato cha ziada. Kwa mara ya kwanza, Mama Regina alipata fursa ya kipekee kuwekeza katika maendeleo ya shamba lake na kuboresha hali ya maisha ya familia yake kupitia faida hii ya kifedha.

Baada ya kuuza mazao yake Mama Regina alitumia kipato kupanua shughuli zake za kilimo kwa kununua ekari moja ya ardhi (shamba) ambayo amepanga kuitumia kwa kilimo cha mbegu za njugu na ulezi. Kuongezeka kwa eneo la shamba, kutamwezesha kulima mazao mengi kwa manufaa ya familia yake na kwa ajili ya kusambaza mbegu bora kwa jamii yake. Hii itasaidia kuongeza usalama wa chakula katika kijiji chake.

Baadaye, Mama Regina alipata nafasi ya kushiriki katika maonyesho ya chakula na mbegu (Siku ya Chakula Duniani) yaliyofanyika Kigoma na Bukoba. Maonyesho haya yalikuwa fursa muhimu kwa Mama Regina kuungana na wakulima kutoka mikoa mengine, kubadilishana maarifa na kuonyesha mbegu zao. Katika maonyesho haya, aliweza kuuza mbegu zake na kubadilishana mbegu na wakulima wengine, jambo ambalo lilipanua mtandao wake na kumjengea kujiamini zaidi.

Aidha, Mama Regina amekuwa msimamizi wa benki ya mbegu ya jamii, ambapo ana jukumu la kuhakikisha kuwa mbegu bora na za asili zinapatikana kwa wakulima wa Mpindimbi. Kwa kushirikiana na wakulima wengine, mama huyu ameweza kusaidia kuboresha mbinu za kilimo na kuongeza uzalishaji, hivyo kusaidia familia nyingi kuwa na chakula cha kutosha na cha lishe ya juu.

Malengo ya siku za usoni

Mama Regina anaangalia mbele na kujikaza akiwa na matumaini ya mafanikio makubwa zaidi. Anapanga kuendelea kuzalisha zaidi mbegu za njugu mawe, kwa manufaa ya familia na jamii kwa ujumla. Kama kiongozi katika kilimo endelevu, bado anajitolea kutunza maarifa ya kilimo cha asili na kuyapitisha kwa wakulima wenzake na vizazi vijavyo.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *