Ni wazi kuwa wakulima wengine wamevuna nafaka mbalimbali kama vile maharage na mahindi katika msimu huu wa mavuno hivyo wasipokuwa makini na kuhifadhi kwa usahihi mavuno yote yatapotea kwa kuharibiwa na wadudu, panya, au hata ukungu unaotokana na unyevu.
Ili kuepukana na hasara ni muhimu kuhakikisha unahifadhi mazao yako katika njia salama kama unavyoshauriwa na Mkulima Mbunifu au wataalamu wa kilimo.
Kabla ya kuhifadhi hakikisha mazao yako yamekauka vizuri kwa kung’ata punji ambayo huwa ngumu na hukatika kwa mlio mkali, kumimina kwenye chombo au sakafu, ambapo hutoa mlio mkali kama wa kuumiza sikio, kutumia chumvi yaani kuchanganya mahindi na chumvi kiasi kisha mimina kwenye jagi la kioo, na kama chumvi itang’ang’ania kwenye punje basi hazijakauka au kutumia kipima unyevu ambacho huonyesha unyevu wa asilima 13.5.
Kutayarisha nafaka kabla ya kuyahifadhi
Kabla ya kuweka nafaka kwenye vifungashio au kuhifadhi ghalani, inabidi kuchukua tahadhari ya kuzuia uharibifu utokanao na wadudu au wanyama kama panya ndani ya ghala.
Hakikisha ghala la kuhifadhia nafaka ni safi, lisilovuja na ikibidi changanya mahindi na viuwadudu.
Viuwadudu hivyo vinaweza kuwa vya asili vinavyotokana na mimea kwa mfano mwarobaini au pareto. Aidha ni muhimu kutenga kiasi cha nafaka itakayotumika kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu baada ya kuvuna. Hii ni kwasababu katika kipindi hiki, mashambulizi ya wadudu huwa ni ya kiwango cha chini sana.
Kuchanganya kiuwadudu na nafaka
Wakati wa kuchanganya kiuwadudu na nafaka ni muhimu kuandaa vifaa kama vile, turubai isiyokuwa na matundu, sakafu safi ya sementi, debe la kupimia nafaka, beleshi au koleo, dawa ya kuhifadhia na kifaa au kitambaa safi cha kufunika pua na mdomo.
Hatua za kuchanganya
- Tandika turubai safi kwenye sakafu katika sehemu isiyokuwa na upepo.
- Pima nafaka kwa kutumia debe au kwa kutumia mizani ili kupata uzito wa kilogramu 100 (madebe sita)
- Weka nafaka kwenye turubai na funika pua na mdomo kwa kitambaa safi ili kuzuia dawa isiingie mwilini.
- Fungua pakiti ya gramu 200 ya dawa ya asili na mimina juu ya kilo 100 za nafaka.
- Anza kuchanganya dawa nanafaka kwa kutumia beleshi au koleo mpaka mahindi yote yatakapopata dawa.
- Fungasha kwenye magunia safi ya kilo 100 tayari kwa kuhifadhi ghalani au waweza kuhifadhi kwenye kihenge, silo au bini.
- Nafaka zipangwe kimadaraja kwenye ghala. (Maguniua yasiwekwe moja kwa moja sakafuni, mbao huweza kutangulizwa sakafuni kwanza).
Ghala bora la kuhifadhia nafaka
Ghala bora ni chombo chochote kile au jengo lolote lililo imara na lenye sifa zifuatazo;
- Liwe na uwezo wa kuzuia wadudu, panya, mvua na unyevu kutoka chini.
- Liwe na nafasi ya kutosha kuweka mazao, kukagua na kutoa.
- Liwe na uwezo wa kuhifadhi mazao yaliyokusudiwa.
Aina ya maghala bora
1. Sailo au bini
Haya ni maghala yanayojengwa kwa dhana ya kutokuwepo na mzunguko wa kawaida wa hewa ndani ya nafaka iliyohifadhiwa na kusababisha wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa kutoweza kusitawi na kuharibu nafaka.
2. Mapipa
Mapipa yenye mifuniko imara hutumika kuhifadhi nafaka kwa dhana ya kutokuwa na hewa ndani ya mahindi. Pipa likijazwa mahindi na kufungwa sawasawa hakuna hewa inayoingia na hakuna mdudu anayeweza kuishi ndani yake, na hata punje za nafaka hufa baada ya kuhifadhiwa kwa muda hivyo inashauriwa kuwa nafaka inayotegemewa kwa ajili ya mbegu isihifadhiwe ndani ya pipa.
4. Maghala ya nyumba
Hifadhi hii hufanyika katika chumba au nyumba maalumu na maghala haya huhifadhi mazao yaliyofungashwa kwenye magunia. Uwezo wa kuhifadhi hutegemea wingi wa mazao.