- Binadamu, Kilimo, Mifugo

Jarida la MkM limenisaidia kufanya kilimo ikolojia kwa faida

Sambaza chapisho hili

Jarida la MkM limenisaidia kufanya kilimo ikolojia kwa faida

‘’Nimekuwa nikifanya kilimo ikolojia toka utotoni kwani wazazi wangu walikuwa wakijishughulisha na kilimo na walitegemea kilimo pekee kwa chakula na biashara, na njia ya uzalishaji ilikuwa ni njia za asili pekee’’.

Hayo ni maneno ya Bi. Rehema Joel Mbula (48) mkulima mzalishaji kwa misingi ya kilimo ikolojia na mnufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu toka Ilongero (Singida) ambaye anaamini kuwa kilimo ikolojia kwake ni sehemu ya maisha.

Bi. Rehema anasema kuwa, amefanya kilimo hiki kwa muda mrefu sana lakini toka mwaka 2021 alipoanza kupokea jarida la Mkulima Mbunifu ameongeza ufanisi mkubwa katika uzalishaji jambo ambalo anajivunia kuwa sehemu ya wanufaika wa MkM.

Ilikuwaje mpaka kuwa mnufaika wa jarida la MkM?

Bi. Rehema anasema kuwa, alikutana na meneja wa MkM mkoani Dodoma wakati wa mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliokuwa umeratibiwa na shirika la Farm Radio International, mara baada ya kusikiliza kwa umakini kutoka kwa meneja kuhusu jarida alihamasika na kuomba kupewa nakala, na kuanzia siku hiyo akawa miongoni mwa wanufaika wa kila mwezi. “Nilipoelezwa kwa undani kuhusu jarida la MkM (na Bi. Erica Rugabandana) na namna ya kulipata, nilijiandikisha na nikaanza kupokea nakala kwa ajili ya vikundi (6) ninavyosimamia na ndipo nilipoanza kufaidika na elimu itolewayo na jarida hili” alisema.

Kwanini MkM

Kabala ya kuanza kupata jarida hili, Bi Rehema anasema alikuwa akizalisha kwa njia ya kilimo ikolojia lakini jarida la MkM limemuwezesha kutambua kuwa ili kupata mazao bora na mengi, ni vyema kuzingatia urutubishaji wa udongo ndipo akaamua kutengeneza mbolea ya mboji kutokana na elimu aliyoisoma kwenye jarida kuhusu namna ya kutengeneza mboji na matumizi yake na mpaka sasa anazalisha mboji mpaka tani 7 kwa mwaka. ‘’Bila ya MkM nisingeweza kutengeneza mbolea ya mboji.’’alisema.

Aidha, MkM imemuhamasisha juu ya matumizi ya samadi na ikampa motisha ya kuongeza uzalishaji wa mifugo yake ya ng’ombe mpaka kufikia 7 ambao wanampatia mbolea ya samadi ya kutosha kuweza kutumia katika mashamba yake ya uzalishaji.

Mbali na mbolea, Bi. Rehema anaeleza kuwa, alijifunza namna ya kutengeneza dawa za asili kwa ajili ya kufukuza wadudu na kudhibiti magonjwa mbalimbali katika mazao yake jambo ambalo hapo mwanzo lilikuwa likimuwia vigumu lakini kupitia jarida amejifunza hatua kwa hatua na mpaka sasa wadudu na magonjwa kwake ni historia. “MkM imenisaidia na kunifundisha kuwa, usisubiri wadudu wawe wengi au ugonjwa uenee ndipo hutibu ila mara tu uonapo dalili chukua dawa puliza, na nimefanikiwa kwa asilimia zote.” Aliongeza.

“Kupitia jarida la MkM, nimeweza kujifunza kutengeneza busta (kirutubisho cha mmea) ambayo natumia kwenye mazao kuongeza ubora hasa kwenye mbogamboga.’’

Anajishughulisha na nini

Bi. Rehema anasema kuwa, anajishughulisha na kilimo cha mahindi, mtama, maharage, alizeti, karanga, matunda na mbogamboga lakini pia anafanya ufugaji wa kuku, nguruwe, ng’ombe na bata.

Katika shughuli zote hizi, Bi. Rehema anaeleza kuwa MkM imemkwamua kutoka pato la milioni 2 hadi kupata T.sh milioni 4 mpaka 5 kwa msimu mmoja wa mauzo ya mazao ya kilimo na mifugo na soko lake likiwa kwa wananchi waliomzunguka na wa mijini.

Faida alizopata kupitia kilimo ikolojia

Bi.Rehema anaeleza kuwa kilimo ikolojia kina faida nyingi kama ifuatavyo;

  • Usalama wa udongo yaani udongo unakuwa na rutuba ya kutosha kwa msimu mzima wa mwaka.
  • Mazao salama yasiyokuwa na sumu.
  • Mavuno bora na mengi katika eneo dogo.
  • Mazao kinzani kwa magonjwa na wadudu.
  • Uhakika wa chakula safi na salama msimu mzima wa mwaka.
  • Kipato kikubwa ambacho anatumia katika kuendesha miradi mbalimbali kama kusomesha watoto mpaka elimu ya juu, kujenga nyumba, kuongeza mifugo na kuendeleza shughuli za kilimo shambani.

Wito

Bi. Rehema anatoa pongezi kwa Mkulima Mbunifu na anaomba wasiache kuchapisha na kusambaza elimu hii kwa wakulima wengine Tanzania.

Aidha, anawashauri wakulima ambao bado hawajapata jarida hili kuhakikisha wanalitafuta na kulisoma kisha wafanye kilimo ikolojia kwa asilimia zote na si kujaribu.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *