Kuna mbolea nyingi za asili ambazo zinaweza kutumika shambani kama vile samadi, mboji, chai ya mmea na bioslari.
Namna ya kutayarisha mboji/mbolea vunde
Mboji ni sehemu ya viumbe (mabaki ya mimea na wanyama) ambayo imeozeshwa kwa muda mrefu na kusazwa na viumbe wadogowadogo. Sehemu za vitu kama majani, matunda na mabaki ya shambani na ya jikoni hutengeneza mbolea ya mboji. Mboji iliyooza/ iliyoiva hubadilika rangi na kuwa ya hudhurungi, tifutifu na hunukia vizuri.
Mboji ni rahisi kutengeneza, gharama zake ni nafuu na inafaa sana kuongezwa kwenye udongo ili kuinua uzalishaji wa mazao. Mboji iliyotunzwa vyema huwa na rutuba nzuri kwa mimea inapotumiwa shambani. Mboji inapooza kabla ya kutumika shambani hutoa joto kali kiasi cha kuua vimelea vya magonjwa ya mimea na mbegu za magugu.
Namna ya kutengeneza mboji ya mimea
Vifaa na vitu vinavyohitajika
Majani mabichi/kijani na makavu. Majani jamii ya mikunde ni mazuri sana kwani hutengeneza kirutubishi cha naitrojeni (N) kwa wingi, Mabua ya mahindi au Vitawi vidogovidogo vya miti, udongo wa juu shamba, Samadi, mbolea yoyote ya wanyama au mboji ya zamani, majivu au vumbi la mkaa na Maji.
Hatua za kuandaa
- Chagua sehemu iliyokaribu karibu na eneo ambalo mboji itaenda kutumika. Zingatia kama kuna hifadhi ya kutosha kuihifadhi dhidi ya upepo, jua na mvua. Katakata majani makavu na mabichi vipane vidogo dogo ili yaweze kuoza haraka
- Pima eneo la mita sita (6) urefu na upana wake mita 2 kisha weka uzio katika kila kona ya eneo ili kuzuia kuporomoka kwa mali ghafi. Hakikisha kuna nafasi ya kutosha kufanyia kazi kwenye biwi bila kulikanyaga.
- Tifua ardhi katika eneo liliopimwa kiasi ½ futi kisha anza kwa kupanga tabaka la kwanza la vijiti vikavu au mabua ya mahindi/mtama.
- Weka sentimita 10 ya majani makavu tabaka la pili
- Weka sentimita 10 ya majani mabichi na vifaa ambavyo huoza haraka kwa mfano maganda ya mboga na matunda tabaka la 3
- Weka tabaka la 4 sentimita 2 – 3 ya samadi (mboleahai ya wanyama), mabaki ya mbolea ya zamani kama
yaweza kupatikana. - Weka udongo wa juu sentimita 10 kutoka kwenye shamba ambalo hulimwa tabaka la 5
- Majivu na mkojo vyaweza kunyunyuziwa juu ili kufanya biwi/lundo kuoza haraka.
- Nyunyizia maji kwenye biwi mpaka lilowe.
- Rudia mpangilio huu kuanzia namba nne (4) mpaka lundo lifike mita moja (1) hadi moja na nusu (1.5) kwenda juu bila kutumia vijiti/matawi yaliyotumika kwanza.
- Biwi la mboji linatakiwa lifunikwe vizuri ili kupunguza/kuzuia mvuke ama mvua nyingi ambayo hubeba rutuba kutoka kwenye mbolea. Funika kwa gunia, nyasi ama majani ya ndizi yaliyokauka.