Nilianza kupokea majarida ya Mkulima Mbunifu kwa zaidi ya miaka 5 sasa (Eliakarimu G. Gayewi wa kikundi cha Dilega Katesh mkoani Manyara).
Nashukuru sana kuwa sehemu ya wanufaika wa jarida hili kwani toka nianze kupokea nimejifunza na kufaidika na mambo mengi kwenye kilimo na ufugaji.
Kuna elimu nyingi kuhusu kilimo zinazotolewa kwenye jarida hili ambayo sikuwa najua kwani nilikuwa nalima kwa mazoea tu lakini nimejifunza kitu kipya hasa kilimo hai.
Tulikuwa tunalima kwa kutumia mbolea za viwandani lakini toka nianze kufahamu namna ya kufanya kilimo hai na faida zake nimeacha nikaanza kutumia samadi ya ng’ombe iliyoiva na pia mbolea ya mboji ambayo nimekuwa nikizalisha kwa kuozesha taka zingine za kawaida zinazopatikana shambani na nyumbani.
Nimejifunza pia kufunika ardhi na faida zake hivyo sasa naacha mabua shambani mara baada ya kuvuna pamoja na kuotesha maharage aina ya ngwara.
Hakika nimefaidika sana kwani toka nianze kilimo hai mavuno yameongezeka toka gunia 5 mpaka 10 hadi 15 kwa heka.
Kwa upande wa mifugo nimejifunza kuwapa chanjo kwa wakati bila kusubiri mnyama augue, pamoja na namna ya kuhudumia ndama, ng’ombe wa nyama na wa maziwa.
Kama bado hujapokea jarida hili nakushauri litafute kuanzia sasa ili uweze kufaidika na yaliyomo ndani. Mimi binafsi nawapongeza na sitaacha kulisoma jarida hili na naomba Mkulima Mbunifu msisitishe kunitumia kila mara linapotoka.