Soya ni zao mojawapo katika mazao ya jamii ya mikunde ambalo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Morogoro, Rukwa, Lindi, Mbeya, Iringa na Arusha.
Zao hili huwa na virutubisho vingi kama vile wanga, protini, mafuta, madini na hata vitamini. Aidha, lina sifa ya kuwa na kiasi kikubwa cha protini kinachofikia hadi asilimia 40.
Soya ni zao la muda mfupi ambalo hukomaa ndani ya miezi mitatu hadi mitano toka kupandwa kulingana na aina, hali ya hewa na mwinuko kutoka usawa wa bahari.
Dalili za soya iliyokomaa
Majani hubadilika rangi kutoka ukijani na kuwa ya manjano.
Majani na hupukutika na mapodo hubadilika rangi kutoka ukijani na kuwa ya kahawia.
Uvunaji wa soya
Ni muhimu kuvuna mapema mara zao linapokomaa ili kuepuka upotevu wa mazao unaoweza kutokea kutokana na kushambuliwa na wadudu, kupasuka kwa mapodo au kunyeshewa na mvua.
Kipindi kizuri cha kuvuna soya ni wakati wa asubuhi ambapo hakuna jua kali linaloweza kusababisha mapodo kupasuka.
Njia bora za kuvuna
Soya huweza kuvunwa kwa kutumia mikono, mashine maalum za kuvuna nafaka, au mashine za kukokotwa na wanyama.
Kutumia mikono
Soya huweza kuvunwa kwa kutumia mikono kwa kukata au kung’oa mashina kisha kuyarundika mahali pamoja na baadaye kuyapeleka sehemu ya kukaushia na kupuria.
Kutumia wanyama kazi
Unaweza kutumia mashine zenye visu vya kukata ambazo hukokotwa na wanyama kazi.
Kutumia mashine
Soya pia huweza kuvunwa kwa kutumia mashine maalumu za kuvuna nafaka. Umuhimu wa kutumia mashine hizi ni kuwa huokoa muda kwani huweza kuvuna hekta moja kwa saa moja au mbili kulingana na ukubwa wa mashine na jinsi shamba lilivyosawazishwa.
Kukausha na kupura
Baada ya kuvuna, mapodo hukaushwa kwa kutumia kichanja, kribu, maturubai au sakafu safi kisha kupura.
Unaweza kupura soya kwa kutumia miti kugonga hadi mapodo yote yapasuke, au kutumia mashine za kuvuna nafaka ambazo hupura na kupeta.
Baada ya kupura na kupeta, punje za soya huhitajika kukaushwa tena kwenye kichanja, au chekecheke na katika sehemu ambayo hairuhusu uchafu kuingia katika soya, kisha kuhifadhi baada ya kukauka (kausha ili kupunguza unyevu hadi kufikia asilimia 11)
Usindikaji wa soya
Kama ilivyo kawaida kwa aina nyingi za mikunde kuwa na madhara iwapo itatumika bila kuchemsha, soya ni muhimu kuzichemsha kabla ya kutumia ili kuondoa sumu na vimeng’enyo vinavyozuia kutumika kwa protini mwilini.
Soya huweza kusindikwa na kuzalisha bidhaa mbalimbali kama vile, soya zenyewe, unga, maziwa, kahawa na njugu. Kwa kufanya hivyo mkulima ataweza kuzuia uharibifu na upotevu wa mavuno yake unaoweza kujitokeza baada ya kuvuna zao hili.
Kusindika soya zenyewe
Soya zilizosindikwa hutumika kupika kama mboga, kupikia makande, ndizi au chakula chochote kile mlaji atakachoamua kukiandaa.
Vifaa
Sufuria yenye mfuniko, kaushio bora na safi, ndoo safi, jiko, ungo, vyombo vya kusafishia kama beseni na vifungashio.
Namna ya kutengeneza
- Chemsha maji kiasi kulingana na soya unazokusudia kusindika.
- Maji yakishachemka, osha soya kisha weka taratibu kwenye maji yanayochemka.
- Chemsha kwa muda wa nusu saa kisha epua na mwaga maji yote.
- Weka maji ya baridi ili kupooza na ondoa maganda yote.
- Baada ya kuondoa maganda yote, osha kwa maji safi ya baridi kisha weka kwen ye kaushio na kausha.
- Fungasha katika mifuko safi na hifadhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali au peleka sokoni kuuza.
Kusindika soya kupata maziwa
Soya huweza kusindikwa kwa aajili ya kupata maziwa ambayo hutumika kama source kwenye mchuzi au supu.
Vifaa
Sufuria safi, Jiko, Kitambaa au chujio safi kwa ajili ya kuchujia, Brenda (mashine ya kusagia) na vifungashio kavu na safi.
Jinsi ya kutayarisha
Ili kudhibiti ubora wa vyombo na mazingira yote katika hatua zote za usindikaji tumia malighafi zilizo na ubora na fuata hatua sahihi za kusindika.
- Chemsha maji mpaka yachemke vizuri.
- Safisha soya na weka kwa taratibu kwenye maji yanayochemka na iache iendelee kuchemka kwa dakika 30.
- Mwaga maji yote ya moto kutoka kwenye soya na pina na changanya maji ujazo wa vikombe vitatu kwa kila kikombe kimoja cha soya.
- Saga mchanganyikohuo kwa kutumia Brenda na chemsha mchanganyiko huo ukiwa unakoroga kwenye moto mdogo kwa muda wa dakika 20.
- Epua kisha chuja kwa kitambaa safi au chujio na chemsha maziwa hayo ukiwa unakoroga kwa muda wa dakika 10.
- Fungasha kwenye vyombo vilivyochemshwa kisha hifadhi sehemu yenye hali ya ubaridi.
Kusindika soya kupata kahawa (soyee)
Soya iliyosagwa kwa ajili ya kahawa hutumika kama vile chai na hutayarishwa kwa kutumia kiasi kidogo cha unga wa soya katika maji au maziwa ya moto kisha kunywa kama chai au kahawa.
Vifaa
Mashine ya kusaga, jiko, sufuria, mizani, vifungashio na kaushio bora.
Jinsi ya kutengeneza
- Chemsha soya na kausha vizuri kisha kaanga hadi ifikie rangi ya kahawia iliyokolea.
- Saga kwa kutumia mashine hadi upate unga laini.
- Tumia mashine yenye chekecheke dogo kiasi cha milimita 0.5 ili kupata unga laini.
- Fungasha kwenye vifungashio safi visivyopitisha unyevu.
- Hifadhi mahali pakavu na safi kwa matumizi au peleka sokoni kujipatia kipato.
Kusindika soya kupata njugu
Njugu zilizotokana na soya hutumika kama vitafunwa.
Vifaa
Jiko, sufuria/kikaango, mizani, vifungashio safi vya kuhifadhia.
Jinsi ya kutengeneza
- Chemshwa na kukaushwa kisha kukaanga hadi ipate rangi ya kahawia.
- Ongeza chumvi kiasi ili kuongeza ladha baada ya kuipika.
- Fungasha kwenye vifungashio kisha hifadhi mahali pakavu na safi.
Kusindika soya kupata unga
Unga unaotokana na soya hutumika katika kuungia mboga aina mbalimbali. Pia, hutumiwa kwa kuchanganya na nafaka ili kutengenezea vyakula mbalimbali kama vitafunwa au vyakula vya lishe.
Vifaa
Mashine ya kusaga, vifungashio safi na vikavu, na mizani.
Jinsi ya kutengeneza
- Chemshwa kiasi cha soya uliyoandaa kusindika kisha kausha vizuri.
- Baada ya kukauka, saga kwenye mashine ili kupata unga laini.
- Chukua unga na fungasha kwenye mifuko safi isiyopitisha unyevu.