- Kilimo Biashara, Usindikaji

Kutoka kuzalisha maziwa mpaka kiwanda cha kusindika

Sambaza chapisho hili

Biashara ya maziwa ni biashara maarafu sana katika maeneo ya kanda ya kaskazini mwa Tanzania ambapo kuna wafugaji wengi.  Biashara hii imeweza kuwanufaisha wafugaji wengi ikiwa ni miongoni mwa zao la mifugo linalo wasaidia wafugaji kujikwamua kiuchumi.

Uzalishaji na uuzaji wa maziwa ni kitega uchumi kizuri ikiwa itafanywa kwa kuzingatia kanuni, taratibu na kuzalishwa katika hali ya usafi. Biashara hii inafaida nyingi iwapo mfugaji atafanya kwa hiari na atakua anaipenda kazi yake.

Jambo la kuzingatia kabla ya kuanza biashara ya maziwa

Katika biashara yoyote, usimamizi ni jambo muhimu kuzingatia ili kuhakikisha mfanyabiashara anafikia malengo. Vivyo hivyo kwa mkulima yoyote, ni muhimu kuhakikisha anasimamia biashara yake ili aweze kufikia malengo.

Hata hivyo kumekua na changamoto katika kuifanya biashara hii kwani wafugaji walio wengi wamekua wakilalamika kukosa soko la maziwa, jambo linalisababisa maziwa kuharibika na kumwagwa.

Kufuatana na takwimu za bodi ya maziwa Tanzania (TDB) inaonesha kuwa unywaji wa maziwa nchini ni  mdogo kwa wastani wa lita 47 kwa mtu mmoja kwa mwaka wakati shirika la chakula duniani (FAO) linapendekeza kunywa lita 200 kwa mtu kwa mwaka.

Alphayo John Mollel aonyesha njia

“Nilianza ufugaji mwaka 2008 nikiwa na ng’ombe wawili aina ya Freshiani (Friesian) ambao kwa siku walikuwa wanatoa maziwa kiasi cha lita 50”.

Bwana Alphayo anaeleza kuwa, maziwa hayo aliweza kuuza kwa kupeleka sokoni na hata kuuza nyumbani kwa majirani jambo ambalo pamoja na jitihada zote hizo kiasi kingi cha maziwa kilikuwa kikibaki bila kuuzwa na kupelekea kuharibika.

‘’Kutokana na upotevu wa maziwa uliotokana na kukosekana na wateja na kupelekea maziwa hayo kuharibika, niliwaza ni kwa namna gani naikabili changamoto hii na ndipo nilipokuja na wazo la kuwa na kiwanda cha kusindika maziwa” alieleza.

Bw. Alphayo Mollel akiwa na familia yake nje ya kiwanda chake cha kusindika maziwa

Ndoto ya kua na kiwanda ilianzaje?

Kuna usemi usemao “changamoto ni fursa” na kwa Bwana Alphayo ni hakika changamoto ya kukosa soko na kuharibika kwa maziwa ilikuwa fursa na hata wakristo “husema kila changamoto ina mlango wa kutokea”.

Bw. Alphayo alisema, “niliamua kutafuta elimu juu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa na kuongeza thamani katika pata thamani wa maziwa ambapo nilifanikiwa kupata mafunzo hayo kupitia chama cha wakulima Tanzania (TASO)”.

Wakati akiendelea na mafunzo, anasema kuwa, aliendelea na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa huku akipata ushauri kutoka kwa wataalamu wa mifugo waliopo halmashauri ya wilaya ya Arusha.

Namna alivyoanza usindikaji wa maziwa

Bw. Alphayo baada ya kupata elimu, mwaka 2015 alianza usindikaji wa maziwa kwa kuzalisha mtindi ambapo alianza na maziwa lita 10 akaongeza hadi 20 huku akitumia sufuria ya lita 50 na keni ya maziwa ya lita 20.

Aidha, alianza kutoa taarifa kwa watu mbalimbali kuhusu mtindi bora aliokuwa anazalisha, na kuweza kutengeneza soko kuanzia nyumbani kwa kuuza kwa marafiki na majirani na hata baadaye kupeleka sokoni Ngaramtoni.

Hatua za kuanzisha kiwanda cha kusindika maziwa ya mtindi

  • Bwana Alphayo aliwatembelea wataalamu wa SIDO kujitambulisha kuhusu shughuli ya usindikaji anayoifanya. Wataalamu walimtembelea na kumpa utaratibu wa kufuata.
  • Alianza ujenzi wa jengo la kusindikia maziwa (kiwanda kidogo), kwa kuchukua mkopo kutoka Benki ya Biashara ya Akiba – Akiba Commercial Bank (ACB).
  • Ujenzi ulipokamilisha aliwaita SIDO ili kukagua kwa mara ya pili na walimshauri kufanya upanuzi kwani jengo lilikua dogo.
  • Baada ya kukamilisha ujenzi kwa mara ya pili, alifuata utaratibu wa kukaguliwa na mamlaka ya chakula na dawa Tanzania (TFDA) na kupata usajili rasmi mnamo Julai 2018 kwa jina la Olmotonyi Dairy.
  • Kupata leseni ya biashara, pamoja na kuisajili kiwanda shirika la mapato Tanzania TRA kwaajili ya kupata namba ya kulipa kodi yaani TIN.
  • Kukaguliwa na shirika la viwango Tanzania (TBS) ambapo baada ya kupeleka maombi walihitaji kuona leseni ya biashara, namba ya mlipa kodi, ramani ya jengo, mtiririko wa uzalishaji, muundo wa kiwanda na mahali inapotoka malighafi yaani maziwa ya kusindikwa.

Mafanikio

Bw. Alphayo anasema kuwa, “najivunia kuwa mmoja kati ya watu wanaotekeleza agizo la Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu uchumi wa viwanda na nimepata faida kwa kasi kikubwa toka nianze kuzingatia hili”.

Mafanikio aliyoyapata mpaka sasa ni pamoja na;

  • Kumiliki kiwanda cha kusindika maziwa, ambapohadi kufikia wakati huu anasindika lita 100 za maziwa kwa siku.
  • Ameongeza kipato kwa asilimia kubwa na kuweza kununua gari ya kubebea maziwa kupeleka sokoni.
  • Ameweza kuokoa kiwango kikubwa cha maziwa ambacho hapo awali yalikuwa yakiharibika na kupelekea kumwaga, jambo ambalo limepata ufumbuzi wa kusindikwa na kuzalishwa mtindi.
  • Kukua na kuongezeka kwa soko la maziwa anayoyazalisha kwani wote wanaonunua na kutumia maziwa hayo wamefurahia ubora na ladha ya maziwa.
  • Wafugaji wengine wa ng’ombe wamekuwa wakifuatilia kwa karibu sana na kupata mafunzo kutoka kwake juu ya uzalishaji bora wa ng’ombe wa maziwa.
  • Kupitia usindikaji na uuzaji wa maziwa ameweza kununua mashine ya kuchakata majani.
  • Amefanikiwa kuwa mjumbe mzuri kwani amekuwa akishirikishwa kuhudhuria na kuonyesha kwa vitendo bidhaa zake kila semina za wadau mbalimbali zinapotokea.
  • Kupitia kiwanda ameweza kutengeneza ajira kwa watanzania wengine kwani kuna wafanyakazi wanaotumika kusaidia shughuli za kiwandani.
  • Ameweza kuendeleza familia yake kwa kusomesha watoto katika ngazi mbalimbali za elimu kuanzia shule ya msingi, sekondari na vyuoni.

Changamoto

Pamoja na mafanikio Bwana Alphayo anasema kuwa, mwaka 2018, alipoteza ng’ombe 7 kwa kwakati mmoja, na ng’ombe hao waliugua ugonjwa ambao ulishindwa kutambulika.

Aidha, aliongeza kuwa, bei ya maziwa ipo chini hasa ukilinganisha na gharama za uzalishaji kama ununuzi wa  vyakula vya mifugo ambazo zipo juu.

Matarajio

“Ninatarajia kupanua shughuli za usindikaji maziwa kutoka kusindika lita 100 kwa siku hadi lita 500, jambo ambalo endapo nitafanikiwa basi nitaweza kuongeza pato na kutoa ajira kwa watu wengi,” alisema.

Wito

Bw. Alphayo anaiomba serikali iendelee kuelimisha wafugaji na wakulima kufanya kazi kwa bidii kwani viwanda vyetu vinahitaji malighafi kutoka kwa wakulima.

Mbali na hiyo ameomba serikali kuhimiza watanzania kuwa na tabia ya kuthamini bidhaa zinazotengenezwa nchini kwani kwa njia hiyo ni rahisi kuinua pato la taifa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Kutoka kuzalisha maziwa mpaka kiwanda cha kusindika

  1. Naomba msaada wa wapi nitapata mashine ya kugandisha maziwa(pasteurization milk)

    1. Habari,

      Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili.

      Tafadhali watafute watu wa SIDO watakuwa msaada zaidi kuweza kupata mashine hiyo.

      Karibu sana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *