Vanilla ni moja ya zao la viungo ambalo hutumika kila siku nyumbani na maeneo mengine. Matumizi makubwa ya zao hili ni kuongeza harufu nzuri na ladha ya vyakula na vinjwaji mbali mbali.
Baadhi ya vyakula ambavyo vanilla huwekwa ni pamoja na chokoleti, keki, maandazi, biskuti, uji, barafu pia vinjwaji baridi kama soda na juisi. Mbali na utengenezaji wa vyakula, vanilla hutumika pia kutengeza manukato, mafuta ya kulainisha ngozi, sabuni, vipodozi n.k.
Vanila ni zao la biashara na hustawishwa vizuri kwenye mashamba ya migomba na mibuni kwani mazao haya hutoa kivuli, tandazio shambani, hupunguza kasi ya upepo na huongeza hali ya unyevu angani.
Mmea huu huota juu ya uso wa ardhi na hutambaa kwenye mti wa mhimili. Mmea huu hustawi kwa miaka mingi na hurefuka zaidi kutegemea matakwa ya mkulima. Vanilla haishindanii virutubisho na mazao mengine shambani.
Malighafi zinazohitajika
- Rando refu la 2m-lenye afya lisilo na ugonjwa
- Kamba za asili
- Matandazo
- Majivu
- Maji ya kumwagilia
Maandalizi kabla ya kupanda
- Eneo la kupanda ni lazima liwe na kivuli kwa asilimia 50%. Vanilla ni lazima iwe kwenye kivuli wakati wa kipindi cha jua kali, hasa kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa alasiri (04:00 asubuhi -09.30 alasiri).
Miega ambayo ni miti ya kujiegemezea vanilla ni lazima iwe ya mita mbili au zaidi na yenye nguvu ya kutosha kujiegemezea vanila. Nafasi kati ya miega/rando la vanilla inatakiwa iwe mita 2.5-3 kati ya mstari na mstari na mita 1.5-2 kati ya mmea vanilla kwenye mstari.
Ikiwa kuna miti mingine kama mikahawa na migomba ni lazima uache nafasi ya kutosha kwenye eneo la muega wa kujishikizia vanilla ili baadae iweze kujitanua wakati wa kulisha rando. Ikiwa muega wa kujishikizia vanilla umekufa ni lazima ubadilishwe kabla ya kupanda vanilla
- Uchaguzi wa eneo la kupanda vanilla ni muhimu ili kuzuia mmomonyoko wa udongo, kusongamana na mimea mingine, na kama mpango ni kuikuza kwa kilimo hai, mkulima anatakiwa kuacha umbali wa mita 10 kati ya mimea ambayo haikuzwi kwa kilimo hai. Shimo la kupanda rando la vanilla linapaswa kuandaliwa kwa kuweka vitu mbalimbali vya mboji ili kulipa rando la vanilla virutubisho. Hakikisha eneo la kupanda rando la vanilla limeinuka kidogo ili kuepuka mizizi kujaa maji na kuoza.
Hatua za kufuata wakati wa Upandaji
Majani ya mwanzo chini 4-5 ya rando la vanilla yaondolewe kabla ya kupanda endapo mkulima atakuwa na wasiwasi kuwa yataoza. Yanaweza kukatwa na kisu kikali halafu yakaning’inizwa kwenye kivuli kwa siku mbili kabla ya kupanda rando ili kuruhusu sehemu ambayo majani yamekatwa kupona ili kuzuia vimelea vya ugonjwa kuingia kwenye rando la vanilla.
- Safisha eneo dogo la 50sm karibu ya muega na kutengeneza kinfereji kidogo kwenye udongo au weka matandazo inchi 2 kwenda chini.
- Weka rando la vanilla kwenye kinfereji huku 5sm chini ya ncha kwenye shina la rando kutokeza kwa juu ya kinfereji na urefu uliobaki wa 15sm, urefu wa mkono mmoja,toka kwenye muega.
- Fungia rando la vanilla kwenye muega kwa kutumia kamba ya mgomba mfano wa umbo la namba nane. Tumia kamba 3-4 kufungia rando kwenye muega. Kunja kidogo ncha ya juu ya rando ili kuchagiza chipukizi kutokeza kwa juu ya rando.
- Ufunike rando la vanilla ndani ya kinfereji kwa udongo pamoja na maozea ya asili (matandazo) kuhakikisha ncha ya kwenye shina ipo juu kuizuia isije kuoza.
- Tandaza matandazo kuzunguka eneo lote ili kuwezesha mizizi kukua.
- Kulinda dhidi ya kuku hakikisha unaweka vizuizi kuzunguka matandazo hasa mashina ya mgomba au vigogo vya mti vilivyo kauka.
- Ni Muhimu kuupa mmea wa vanilla virutubisho kwa kuweka matandazo ya mara kwa mara. Malighafi mbalimbali zinaweza tumika kama matandazo; mboji mara nyingi hutoa virutubisho vingi na kwa haraka, masalia mengine ya mimea kutoka shambani yanaweza kutumika pia kama matandazo kuzunguka shina la rando la vanilla.
Elimu mnayotoa no muhimu Sana maisha yetu Kila siku.Napenda kujinga nanyi kwani nimeona Aina ya ya majani ambayo yatanisaidia kwa ajili ya ngo”ombe wangu yaani matete.0.Pamoja na hayo yanapatikana wapi
Habari
Karibu sana Mkulima Mbunifu na tunafurahi kusikia kuwa elimu tunayoitoa imekuwa chanya kwenye maisha na kazi zenu za kila siku.
Sisi tunajishughulisha na utoaji wa elimu ya kilimo endelevu na kilimo cha asili kupitia majarida yetu ya kila smwezi ambayo huchapishwa na kusambazwa kwa wakulima na wafugaji kwa njia ya posta, barua pepe ama kwa kusoma moja kwa moja kupitia kwenye tovuti hii.
Kuhusu matete yanapatikana kwa wafugaji wengi mkoani Arsuah hivyo ungetujulisha kama wewe unapatikana wapi tutafute mkulima wa kukuunganisha naye
Karibu Mkulima Mbunifu
nmependa chapisho la kilimo cha vanila
Karibu sana
Nahitaji kuja VP nitapata mbegu za vanilla nataka kujishuhulisha na kilimo cha vanila
Karibu. Kuhusu mbegu sisi Mkulima Mbunifu hatuuzi lakini kuna wakulima wanauza hivyo unaweza kuwasiliana na mmoja wa wakulima wa vanila toka Arusha Bi. Penina Mungure kwa simu namba 0787 202 946
Karibu Mkulima Mbunifu
Habari! Naomba kama kuna mkulima wa vanila apa Dar es salaam, napia naomba ushauri je vanila inasitawi dar ? Naweza kujenga banda la makuti ili kutengeneza kivuri na pia shina moja naweza pata kilo ngapi?
Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako. Zao la vanilla huhitaji hali ya hewa yenye wastani wa nyuzi joto za sentigrade 28 inaweza pia kuhimili katika nyuzi joto za sentigrade 21 hadi 30). Huhitaji mvua zenye mtawanyiko mzuri wa milimita kati ya 1,500 na 3,000, lakini pia inaweza kustawi
vizuri katika mvua za wastani wa milimita 2,000. Zao la vanila huhitaji kivuli kiasi kwani mimea hii haipendi jua kali, sina hakika sana kama unaweza kulima kwenye chumba cha makuti kwani pia huhitaji miti kwajili ya kujishikiza lakini pia hewa safi.
Kuhusu shina moja la vanila kutoa kilo ngapi, hiyo inategemeana na ubebaji wa matunda na uchavushaji mzuri uliofanyika.
naomba kuuliza zao la vanilla kwa mkoa wa lindi ,hali ya hewa inaweza kuwa rafiki?
Habari, karibu Mkulima Mbunifu. Zao la vanila linaweza kustawi vizuri katika mkoa wa Lindi na ni miongoni mwa miko nchini Tanzania yenye hali ya hewa inayoweza kuzalisha zao hili