Shule ya Sekondari Shambalai
‘‘Tuna furaha sana kukutana na Mkulima Mbunifu katika utoaji wa elimu kwani tuna bustani yetu tuliyoianzisha kwa msaada wa mwalimu mkuu, na tumeshindwa kuiendeleza kwa muda mrefu sasa kulingana na kuwa kila tulichokuwa tukijaribu kuotesha tulikosa mavuno lakini jarida hili limetupa nguvu ya kuanza kwa upya.’’
Hayo ni maneno ya mmoja wa wanafunzi wa shule hii Sophia Shabani Shedafa (Kidato cha 3) ambaye ameeleza furaha yake baada ya kupata jarida hili na kugundua kuwa kwasasa wanaweza kufufua kilimo bustani yao ya shule, kwa njia rahisi sana na kwa gharama nafuu wakilenga kuvuna kwa wingi.
Mwanafunzi huyu anaeleza kuwa, wamekuwa wakiotesha mazao ya aina mbalimbali kama vile viazi mviringo bila mafanikio hasa wakati wa mavuno ambapo yalikuwa hafifu sana yakukatisha tama na wakati mwingine hakukuwa na chochote cha kuvunwa isipokuwa kumea kwa majani tu.
Aidha, walihangaika kwa kipindi kirefu sana bila kujua nini cha kufanya lakini anashukuru kukutana na wadau wa elimu Mkulima Mbunifu kwani maswali ya matatizo yote na changamoto walizokuwa wakikutana nazo zimepata suluhisho hasa kujua zao gani wataotesha kwa msimu upi, maandalizi ya shamba, uchaguzi wa mbegu, kutibu magonjwa na yote kwa kufuata kanuni za kilimo hai.