Ni miaka tisa sasa tangu kuanzishwa kwa jarida la Mkulima Mbunifu likiwa limejikita katika kutoa elimu kuhusu kilimo, ufugaji, pamoja na kilimobiashara kwa lengo la kusaidia jamii kujikimu kimaisha.
Jarida hili, limeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, katika kufikisha elimu kwa wadau mbalimbali na kuonesha fursa nyingi zilizopo kwenye kilimo na ufugaji hasa katika kilimo hai.
Mkulima Mbunifu pia limewafikia wanafunzi kwa lengo la kuwajengea misingi bora ya kilimo hai wakiwa wadogo ili waweze kukua wakiwa na elimu ya kutosha kuhusi kilimo na ufugaji na kuweza kufanya kwa ufanisi.
Aidha baadhi ya wanafunzi na walimu katika shule mbalimbali ambazo Mkulima Mbunifu limeweza kufika, kuonyesha furaha yao na kueleza ni kwa namna gani jarida la Mkulima Mbunifu limekuwa na litakuwa mkombozi mkubwa sana katika maisha yao ya kila siku.
Shule ya msingi Kioga
Wanafunzi hawa pamoja na kuwa ni wadogo sana lakini wanapenda kilimo na tayari wanabustani mbalimbali za mboga zinazolimwa kwa kuzingatia misingi ya kilimo hai.
Mwalimu wa wanafunzi hao ambaye ni msimamizi wa kilimo ameeleza kuwa, wanafurahishwa sana na jitihada kubwa waliyonayo wanafunzi katika kuhakikisha bustani za mboga hapo shuleni zinatunzwa vizuri na wakati wote mboga zinapatikana kwa ajili ya walimu.
Aidha anasema kuwa, pamoja na kuwepo kwa ukame, wanafunzi hao wamekuwa wakifanya kila jitihada kuhakikisha bustani zao kila wakati zinashamiri.
‘‘Ninashukuru sana kwa Mkulima mbunifu kuweza kutuletea jarida hili ambalo tunalitumia kuelekeza na kufundisha wanafunzi namna ya kulima na hata kufuga ili waweze kufanya vizuri si shuleni tu bali hata nyumbani kwa kuwashauri wazazi wao na kufanya wao wenyewe kazi za kilimo na ufugaji.’’