- Mifugo, Mimea

Unaweza kuokoa pesa nyingi kwa kutumia mwarobaini

Sambaza chapisho hili

Mimi ni msomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu, na nimefaidika mengi sana. Ningependa kufahamu kuhusiana na mti wa mwarobaini ambao nimekuwa nikisikia kwa muda mrefu kuwa unatibu wanyama na binadamu. Je naweza kuutumia kutibu kuku na mifugo mingine ninayofuga, na je unafaa kwa mazao?-Msomaji MkM

Mwarobaini (Azadirachta indica) ni mti unaofahamika kwa uwezo wake wa kutibu magonjwa ya aina mbalimbali. Inaaminika kuwa mti huu asili yake ni  India na Burma . Mwarobaini hustawi zaidi katika nchi za tropiki na una uwezo mkubwa wa kuhimili ukame.

Nchini Tanzania, mti wa mwarobaini huweza kupatikana kwa urahisi kabisa katika maeneo mengi ya mijini na vijijini.

Mti huu umetumika kutibu magonjwa mbalimbali kwa binadamu pamoja na wanyama. Mfano, inaaminika kuwa kwa binadamu mti huu husaidia kutibu matatizo ya mmeng’enyo wa chakula tumboni, kisukari, kansa, magonjwa ya ngozi, malaria, fangasi, n.k.

Hali kadhalika mti wa mwarobaini umekuwa maarufu sana katika kutibu  mifugo. Hii ikiwa ni wanyama pamoja na ndege.

Dawa ya mwarobaini ina uwezo wa kuua aina mia mbili (200) za wadudu wanaopatikana duniani kote, huku kwa nchi za Afrika ukiwa na uwezo wa kuua aina 50 za wadudu. Dawa hii haidhuru wala kuua wadudu rafiki.

Si kila mwarobaini unafaa kwa dawa

Ili mti wa mwarobaini ufae kutumiwa kama dawa, kuna mambo kadha wa kadha ya kuzingatia ikiwa ni tangu kupandwa.

  • Wakati wa kupanda mti wa mwarobaini ambao unakusudiwa kutumika kwa dawa, ni lazima kukata mzizi mkuu. Hii ni kwa sababu, mzizi wa mwarobaini huenda chini sana ardhini kwa ajili ya kutafuta maji na madini. Hali hufanya mti wa mwarobaini kutokukidhi ubora wa dawa kwani huweza kuwa na mchanganyiko wa madini hatari ambayo huathiri utendaji kazi wake kama dawa, na unaweza kuwa hatari kwa afya ya mtumiaji na wanyama.
  • Ni lazima mti wa mwarobaini kupandwa na miti pinzani. Hali hii hufanya mti wa mwarobaini kupigana kujiwekea kinga, dhidi ya mimea mingine ambayo matokeo yake ni kufanya kiwango chake cha dawa kufikia ubora unaotakiwa.
  • Usitumie mti wa mwarobaini uliojiotea tu ukiwa na lengo la kutengeneza au kutumia kama dawa, kwani unaweza kusababisha matatizo zaidi.

Tibu magonjwa ya kuku

Kwa upande wa ndege, mwarobaini umekuwa ukisaidia kutibu magonjwa ya ngozi, kideri kwa kuku, minyoo, kikohozi, ndui, mahepe na mengineyo.

Unaweza kuandaa dawa ya mwarobaini kwa namna tofauti kulingana na mahitaji yako kwa wakati huo. Kwa ajili ya kutibu kuku, unaweza kuandaa kama ifuatavyo:

Namna ya kuandaa

  • Chukua majani ya mwarobaini viganja viwili
  • Twanga hadi yalainike
  • Loweka kwenye maji lita moja
  • Acha kwa muda wa dakika 20 hadi 30
  • Chuja kwa uangalifu
  • Wawekee kuku wanywe badala ya maji

*Ili kutibu ugonjwa mharo mweupe kwa kuku, changanya mwarobaini na shubiri (Aloevera)

Ugonjwa wa Ndui

Ili kutibu ndui kwa kuku, kamua mbegu za mwarobaini ili kupata mafuta, kisha changanya na shubiri (Aloevera). Paka sehemu zenye vidonda kwa muda wa siku 3 hadi 4. Unaweza kuendelea kupaka mpaka utakapoona vidonda vimepona kulingana na kiasi ambacho kuku alikuwa ameshambuliwa na ndui.

Faida nyingine za  mwarobaini

Hutunza ngozi na kuponya baadhi ya magonjwa yatokanayo na maabukizi ya ngozimwarobaini hutibu magonjwa mengi ya ngozi yanayoambukiza na yasiyoambukiza.Hutibu vidonda vya kuungua vilivyochunika

Mwarobaini unatibu udongo

Mara nyingi uzalishaji wa mazao umekuwa mgumu kutokana na udongo kuwa na magonjwa na wadudu wa aina mbalimbali ambao hufanya uzalishaji wa mazao kuwa duni.

Dawa ya mwarobaini imeonekana kuwa na ufanisi wa hali ya juu katika kutibu udongo kabla ya kupanda mazao shambani.

Mahitaji

  • Mashudu ya mwarobaini
  • Majivu
  • Alizeti mwitu (Tithonia)

*Endapo utakosa alizeti mwitu na eneo lako ni kubwa, unaweza kuchanganya na aina yoyote ya mmea unaolainika ambao majani yake hayajatobolewa na mdudu.

Kuandaa

Weka pamoja mchanganyiko huo baada ya kukausha, kisha saga mpaka ulainike.

Changanya mchanganyiko huo na udongo wakati wa kupanda mazao unayohitaji.

Dawa hii huua wadudu wote maadui na haidhuru wadudu marafiki waliopo shambani.

Kuna baadhi ya wadudu ambao hawafi kwa aina nyingine yoyote ya dawa, isipokuwa dawa ya mwarobaini tu.

* Pia mwarobaini unaweza kutumika kuogeshea mifugo kwa ajili ya kuua kupe na kukinga inzi wanaozinga mifugo kama vile ng’ombe, punda na mbwa.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Ndelekwa Amos Nyiti kwa simu +255 754 598 403

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *