Yapo magonjwa mbalimbali ambayo mfugaji hasa aliyeko kijijini anaweza kuyatibu kwa kutumia dawa za asili ambazo pia zainapatikana katika maeneo yao bila hata kutumia dawa za madukani.
Faida ya kutumia dawa hizi ni kubwa kwani husaidia kuokoa maisha ya mfugo kwa haraka zaidi kama huduma ya madaktari iko mbali, hupunguza gharama za kununua dawa pamoja na kumlipa afisa mifugo.
Mimea yenye kutumika kama madawa ya asili
Zipo aina mbalimbali za mimea ambayo ikitumiwa kwa usahihi itaweza kukinga na hata kutibu mifugo kutokana na maambukizi au magonjwa fulani.
Ikumbukwe tu kuwa, kiwango cha dawa ya asili atakayopewa ng’ombe ni kikubwa au mara mbili ya kiwango atakachopewa mbuzi na kinyume chake, hivyo hakikisha huzidishi dawa kwa mbuzi na hupunguzi pia kwa ng’ombe.
Ndulele kutibu minyoo na kuoza kwato
Ndulele ambayo kitaalamu hujulikana kwa jina la Solunum incanum husaidia kutibu minyoo na hata kuoza kwato.
Namna ya kutumia kutibu minyoo
Chukua mizizi ya ndulele kisha twanga vizuri na hakikisha unapata maji, kamua hayo maji na mnyweshe mbuzi.
Namna ya kutumia kutibu kuoza kwato
Chukua matunda ya ndulele kiasi kisha changanya na majivu na twanga vizuri kisha paka mchanganyiko huo kwenye kwato.
Unaweza pia ukachukua maji, majivu na chumvi kiasi kisha kuchanganya pamoja na oshea kwenye sehemu ya kwato iliyooza mara kwa mara mpaka vidonda vitakapopona kabisa.
Kahawa kutibu kuvimbiwa tumbo
Kahawa ambayo ni zao linalolimwa katika mikoa mbalimbali nchini, huweza pia kutumika kutibu ugonjwa wa kuvimbiwa tumbo.
Namna ya kutumia
Chukua sehemu ya majani mabichi ya kahawa kisha twanga na ongeza maji kidogo. Koroga vizuri na chuja kisha mnyweshe mbuzi au kondoo kikombe kimoja kila siku mpaka atakapopona.
Katani kutibu kuvimbiwa tumbo
Hili ni zao la biashara linalolimwa katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania ambalo asili yake ni huko Mexico.
Namna ya kutumia
Chukua katani na kwangua kama vile unachubua kupata kamba, kisha sehemu ya majani uliyoyakwangua chukua na twanga, ongeza maji na kisha mpe mbuzi kiasi cha kikombe kimoja kila siku.
Mkaa kutibu kuumwa na nyoka
Mkaa unaweza kutumika kama moja wapo ya dawa za asili katika kutibu mfugo pale anapoumwa na nyoka.
Namna ya kutumia
Chukua kiasi cha robo kilo na kisha twanga vizuri mpaka kupata unga na changanya na mafuta ya taa.
Koroga vizuri ndani ya kikombe kisha chuja kuondoa taka ngumu na mnyweshe mbuzi au kondoo maji hayo.
Tumbaku kuua wadudu wanaonyonya damu
Tumbaku ambayo kitaalamu hujulikana kama nicotina tabacum, ni aina ya zao la biashara linalolimwa kwa ajili ya kutengeneza bidhaa ya sigara.
Zao hili hutumika pia kama dawa ya asili ya kuua wadudu wanaonyonya damu kama kupe wakiwa nje ya mwili wa mnyama.
Namna ya kutumia
Chukua majani ya tumbaku na yatwange vizuri kisha ongeza maji. Kamua maji hayo na kisha tumia kumwogesha mnyama kwenye mwili wake wote.
Mtopetope kuua chawa na wadudu wengine
Mtopetope ambao kisayansi hujulikana kama Annona squamosal huweza kutumiwa kama dawa ya asili kuua wadudu wasumbufu kwa wanyama kama vile chawa.
Namna ya kutumia
Chukua mbegu ya topetope na tunda bichi kisha twanga au saga pamoja nap aka kwenye ngozi ya mnyama.
Utupa kutibu chambavu na kuogesha mifugo kuua wadudu
Utupa unaojulikana kisanyansi/kitaalamu kwa jina la Tephrosia vogelii huweza kutumiwa kama dawa ya asili kuogeshea mifugo ili kuua wadudu wasumbufu wan je ya ngozi ya mnyama.
Namna ya kutumia kuogesha mifugo
Chukua kilo moja ya majani ya utupa na maji lita 25, loweka kwa saa mbili mpaka tatu au chemsha kwa dakika 30 na lita 27 za maji, chuja kwa kitambaa kisha weka kwenye bomba la kuogeshea mifugo, changanya na sabuni ya unga kidogo ili iweze kunata kwenye mwili wa mnyama, na hapo inakuwa tayari kwa matumizi.
Unaweza pia kuchukua majani ya utupa, ukatwanga na kuchanganya na maji kisha kupaka katika ngozi ya mnyama mara mbili kwa wili ili kuua na kuzuia kupe, viroboto na chawa.
Greenheart “osokonoi” kutibu nemonia
Osokonoi ni jina la kimaasai ambapo kitaalamu hujulikana kwa jina la warburgia ugandensis huweza kutumika na kutibu kabisa ugonjwa wa pneumonia kwa wanyama.
Namna ya kutumia
Chukua magome yake na kwangua kwa utaratibu mzuri ili kupata unga. Chukua kiasi cha kijiko kimoja cha Chakula cha unga huo kisha weka kwenye maji ya uvuguvugu na koroga mchanganyiko huo vizuri.
Chukua kiasi cha glasi moja tu na umnyweshe mnyama mara mbili kwa siku mpaka pale utakapoona mnyama amepona kabisa.
Mbono/nyonyo kutibu ugonjwa wa ngozi kama ukurutu
Mbono maarufu kwa wengi kama mchimba kaburi ni aina ya mti uotao sana katika maeneo yaliyoathirika kimazingira na yenye mmomonyoko wa udongo. Mmea huu hutoa maua na mbegu ambayo hutumika sana kutengenezea mafuta.
Namna ya kutumia
Chukua majani ya nyonyo pamoja na shina lake kisha kata vipande vidogo vodogo na ongeza maji. Chukua mchanganyiko huo na pasha moto hadi kukaribia kuchemka kisha kamua na tumia maji hayo kuogesha mnyama.
Hakikisha wanyama hawanyi maji yake kwani ni sumu ikitumika kunywa.
Mpapai kutibu minyoo ya tumboni
Mpapai ambao kitaalamu hujulikana kwa jina la carica papaya huweza kutumika kama dawa ya asili ya kutibu minyoo ya tumboni hasa kwa nguruwe.
Namna ya kutumia
Chukua matunda machanga ya mpapai yakiwa mabichi kisha twanga na kuwalisha nguruwe kama Chakula.
Endelea kuwalisha kila siku kwa muda, huku ukifuatilia maendeleo yao kwani mara utakapoanza tu kulisha watakuwa wakitoa minyoo kidogokidogo na hatimaye kuisha kabisa.
Ningependa kupokea machapisho mbalimbali ya mkulima mbunifu ili nijifunze zaidi kilimo ikolojia!
Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida la Mkulima Mbunifu.
Unahitaji kupokea majarida yetu kwa njia gani?
Thanks for the great work you’re doing
You are mostly welcome