- Mifugo

Tuelimishane kuhusu mradi wa samaki kwa uzalishaji wenye tija

Sambaza chapisho hili

Ni mazingira gani yanafaa zaidi kwa ufugaji wa samaki!

Emma Peter anauliza: Nimefuatilia sana huu ujasiriamali kweli nimevutiwa na ningependa kujaribu kufanya. Nina eneo Rukwa lenye maji yakutosha ya asili takribani mita za mraba 2000, naomba ushauri wako Musa, Jinsi ya kuandaa hayo mabwawa na wapi nitapata samaki hasa sato maeneo ya Mbeya au karibu na Rukwa.

Musa Said anajibu: Bw. Emma, katika miradi mara nyingi tunapenda kutumia neno kufanya/kutekeleza na sii kujaribu kwani kutekeleza jambo utafanya kwa juhudi zote kuliko ukisema unajaribu utakuwa unafanya kitu kwa mashaka.

Kwa mita za mraba 2000 ni nyingi ila nakushauri tu ukijenga kwa kuligawa vipande yaani ukatengeneza la mita 20 kwa 15, mita za mraba 300,ambapo utakuwa na mabwawa 6.

Hii itakuwa rahisi kwa kusimamia mradi wako, kupanga bajeti vema katika chakula, na pia ugawaji wa mabwawa husaidia endapo bwawa moja ikatokea samaki wana matatizo basi bwawa jingine litabaki salama.

Pia itakusaidia kupanda kwa awamu hivyo utakuta umejenga mfumo wa kuvuna samaki wako kila mwezi kwa bwawa moja, na siyo kusubiri bwawa moja baada ya miezi sita uje uvune. Katika hilo pia, kuna mambo mengi inabidi utambue kama sifa za bwawa lako, mfumo wa kuingiza na kutoa maji, kuta za bwawa lako na pia kujua bwawa lako udongo wake ni wa mfinyanzi au kichanga ili kujua unajenga bwawa kwa kutumia malighafi za aina gani.

Suala la mbegu za sato, kwa mimi nafanya hizi shughuli Dar es salaam na mtwara. Kwa upande wa mkoa wa rukwa na mbeya nimejaribu kufanya mawasiliano na maafisa uvuvi wa hiyo mikoa hakuna kituo cha uzalishaji wa mbegu za sato, ila mara nyingi huwa tunasafirisha kutoka Dar es salaam kwenda mikoa mingine kitaalamu na wanafika bila ya shida yeyote. Kama mbegu za kambale, huwa tunafanya mfumo wa kuzalisha ukiwa nyumbani kwako, ingawa mfumo huu unahitaji maelezo kwa kina.

Kambangwa anauliza: Mussa mungu akubariki sana, nimepata faida kubwa juu ya ufugaji wa samaki. Swali langu, samaki anachukua muda gani kama umemtunza vizuri toka kifaranga hadi kumvuna aina ya sato au pelage.

Musa Said anajibu: Ahsante ndugu yangu kambangwa. Ukizungumzia kumtunza vizuri ina maana, maji unafanyia vipimo mara kwa mara, unaangalia ph ipo kiwango gani na viwango vingine vinavyo hitajika katika maji, chakula unalishia katika ujazo unaotakiwa kwa wakati na pia chenye ubora, ubadilishaji wa maji unafanyika kwa wakati pindi unapo baini kuna tatizo, samaki wako umeweka katika idadi inayotakiwa.

Ukizingatia matunzo ya aina hiyo, ndani ya kipindi cha miezi 6-8 kupata samaki mwenye ujazo wa gram kuanzia 300-500 na kuendelea ila kwa kambale huwa zaidi ya hapo. Ahsante kwa swali lako zuri.

Mohammed Mbiku anauliza: Mimi napenda kufuga samaki lakini watu wengi wamekuwa wakitoa maelezo ambayo ukiwatembelea kuwaona mafanikio yao yanakuwa siyo sahihi na maelezo ambayo wametoa. Kwa mfano, kuna wengi wanajigamba wanafuga samaki na baada ya miezi sita samaki anakuwa na uzito wa gramu 800 hadi kilo moja. Lakini ukweli wa mambo wafugaji wanne ambao nimewatembelea samaki wao wamekuwa ni kati ya gramu 150-300 na sio gramu 800 hadi kilo moja kama wanavyodai.

Kwa hali hiyo mimi wamenikatisha tamaa sana ya kufuga samaki. Mimi namtafuta mwenye taarifa sahihi ili nipate kufuga samaki. Nawaomba sana mnaotoa elimu au matangazo acheni uongo toeni taarifa iliyosahihi.

Musa Said anajibu: Mohamed Mbiku, kiukweli unachosema ni sahihi, wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitoa taarifa ambazo sio halisi kulingana na nchi yetu. Takwimu kwa nchi za wenzetu mathalani Kenya, Uganda na Rwanda kama ukibahatika kutembelea utaamini kwa kuona kuwa ukuaji wa samaki wao ni tofauti na wakwetu.

Kwa hali halisi, nchi yetu ni kubwa na haifanani kijiografia mfano; hali ya hewa ya Iringa maeneo ya Mufindi au Mafinga ukilinganisha na Mtwara ni tofauti. Sasa hiyo pia ni moja wapo ya sababu.

Usahihi ni kwamba, bado watu walio wengi wanaingia katika ufugaji wa samaki wakiwa hawana taaluma ya kutosha juu ya ufugaji wa samaki, hivyo wengi hukurupuka na kuanza kufuga jambo linalopelekea kutokuwa vizuri kwa samaki na baadae kulaumu wataalamu kuwa ni waongo jambo ambalo sio kweli, japo wapo ambao ni matapeli wanaojifanya wataalamu wa samaki na kuanza kuelezea watu kwa nia ya kushawishi ili apate fedha, lakini baadhi ya watu hao waliobainika hatua za kisheria ziliweza kuchukuliwa.

Kiukweli kama utabahatika kutembelea maeneo mengi tanzania wanayofuga samaki na ukitembelea nchi za jirani utagundua kuwa tofauti kubwa. Watanzania tukubali kuwa tunatabia ya kukurupuka hususani tunaposikia biashara fulani inalipa pasipo kufanya utafiti wa kutosha juu ya hilo suala ulilolisikia lina lipa.

Tilapia katika hali ya kawaida ndani ya miezi 6-8 inabidi awe na uzito kuanzia gramu 250-500.lakini inategemea umesimamia vipi mradi wako? Kama hutoweza kusimamia vema mradi wako kutimiza uzito tarajiwa utakuwa ni ndoto. Mfano; kuna watu hupandikiza samaki wakiwa wadogo bila kujua wana uzito gani, tunashauri kupandikiza samaki wakiwa na gram kuanzi 20-25, lakini kwa utafiti wangu wengi kupandikiza samaki wakiwa na gram chini ya 5, sasa hapa niambie ukuaji wao utafanana?.

Kiukweli bado kuna makosa mengi sana yanayotokea kwa wafugaji samaki hali inayopelekea ukuaji hafifu hususani katika upande wa chakula, hili ni moja ya tatizo la wafugaji wengi. Kwa wale wanaotaka kuona uhalisia zaidi ni vyema wakatembelea mabwawa ya Mbeya, Iringa,Mwanza, kujionea zaidi haya ninayoyasema.

Kikubwa ni elimu, ushirikishwaji wa wataalamu katika hatua zote. Tatizo kubwa wafugaji hupenda kuchukua wataalamu kwa kuangalia unafuu wa gharama ama wakati mwingine kukwepa kabisa kutumia wataalamu wakihofia gharama.

Kuna maelezo mengi kwa kweli nami kama mtaalamu naumia kuona wafugaji wengi hamfanikiwi japo uhalisia wa biashara hii inalipa vizuri, someni na tembeeni mjifunze. Tembelea pia hii blog utajifunza zaidi hususani makosa yanayofanywa na wafugaji hapa nchini.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Musa Said kwa simu +255718986328

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *