Katika suala zima la ufugaji kuna kanuni na taratibu za kufuata kutoka na mabadiliko mbalimbali ya hali ya hewa. Msimu wa kiangazi na msimu wa masika ni muhimu kuifuatilia ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Katika makala hii Mkulima Mbunifu inakuangazia mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa msimu wa jua na wakati wa msimu wa mvua ili kufanikisha ufugaji wako.
Msimu wa mvua
Katika msimu wa mvua ni vema sana kuzingatia hatua zifuatazo ili kuepuka madhara katika mradi wako wa samaki.
1.Hakikisha bwawa ulilojenga linamfumo mzuri wa kutolea maji na kutapisha maji (OVERFLOW). Mfumo huu husaidia bwawa kutojaa maji kiasi ambacho kitafanya maji kujaa zaidi katika bwawa lako na kupelekea samaki kutoka nje ya bwawa lako. Jambo hili husababisha samaki kupungua na kupelekea kupata hasara.
Katika hali ya kawaida mfumo huu hujengwa mapema kabla ya kupandikiza samaki, wakati wa ujenzi wa bwawa sehemu ya chini kabisa huwekwa bomba kwa ajili ya kutolea maji (outlet pipe) na juu hukatwa kwa wastani wa mita moja ambapo maji huishia hapo kisha kufunikwa kwa wavu ilikuzuia samaki kutoroka.
2.Punguza au sitisha kabisa kiwango cha ulishaji kwa samaki wako. Kutolisha samaki kwa nyakati hizi za mvua hususani mvua inaponyesha kwani hali ya joto kwenye maji hupungua na joto la mwili wa samaki hushuka. Samaki hupoteza hamu ya kula kwani huwa ni vigumu kwao kula chakula wakati matone ya maji ya mvua yanapodondokea kwenye bwawa samaki. Katika hali ya kawaida samaki huja juu kufuata chakula endapo unalisha hicho chakula samaki itawawia vigumu kula hicho chakula.
Madhara ya kulisha samaki mvua ikinyesha
- Hupelekea kuchafuka kwa maji kwa haraka kwani chakula hicho huoza na kuharibika na hatimaye huchafua maji kitu ambacho huongeza gharama za ziada za ubadilishaji wa maji kabla ya wakati.
- Wakati mwingine usipo badilisha kwa wakati huenda ukapelekea vifo kwa samaki kutokana kuchafuka kwa maji hayo ambayo hutengeneza hewa chafu na kupelekea samaki kushindwa kupumua vizuri na hatimaye kufa.
- Kupoteza chakula ambacho hakijaliwa na samaki na kingeweza kutumika wakati mwingine na kusababisha hasara ambayo kama utazingatia kanuni na ushauri wa kitaalam zinaweza kuepukika.
3.Kumirisha tuta na kingo za bwawa hususani kwa mabwawa yaliyojengwa kwa udongo wa mfinyanzi au katika njia za maji. Ni vema kukagua na kuangalia kuta za bwawa lako kama linaupana wa mita zaidi ya moja au mbili kwa uimara zaidi. Kingo za tuta ziwe kubwa na ndefu kiasi ambacho endapo maji mengine yaliyo kwenye mkondo wa maji hayawezi kuingia ndani ya bwawa lako la samaki.
Katika kuchukua tahadhari ni vema sana kufunika bwawa lako kwa wavu mzuri ili kwa mabadiliko yeyote yale samaki wako wabaki salama ndani ya bwawa lako.
Baadhi ya wafugaji wa samaki wamekua wakilalamika juu ya samaki kutoroka kutokana na kupasuka kwa bwawa, maji kupita juu bwawa, samaki kufa hizi ni baadhi ya sababu ambazo huchangiwa hasara katika ufugaji wa samaki. Jambo la msingi ni kuzingatia kanuni na taratibu za ufugaji zinazoelekezwa na wataalamu.
Hata hivyo wataalamu wanashauri ni vema kufanya ukaguzi na udadisi kabla ya kujenga bwawa la kufugia samaki. Mshirikishe mtaalamu katika hatua zote za ujenzi ili akushauri kulingana na eneo husika ikiwemo asili ya eneo kama vile mwinuko bondeni au tambale, aina ya udongo na uoto wa eneo husika.
Kuna baadhi ya samaki wamekufa katika mabwawa yaliyopo bondeni kutokana na shughuli za kilimo zinazoendelea nyanda za juu na kusababisha chemikali za viuatilifu na mbolea za chumvichumvi kushuka ardhini kuathiri samaki.
4.Vuna samaki wako, endapo hatua zote zimekuwa ngumu kutekelezeka, ni vema kuvuna samaki wote na kuwauza ili kuepuka hasara zaidi. Hii itakufanya kufuga kwa msimu tu pekee yaani unafuga zaidi msimu wa kiangazi na inapofika msimu wa mvua unavua samaki wote kisha baada ya msimu wa mvua kuisha unaendelea na ufugaji wa samaki.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Musa Saidi wa Fish Farming Service Tanzania kwa simu namba 0718986328