Wakulima na wafugaji wanashauriwa kuwa katika vikundi au vyama vya ushirika ili kukuza na kupanua kilimo biashara.
Ushirika ni biashara zinazojikita kwa watu; zinamilikiwa, zinadhibitiwa na zinaendeshwa na wanachama na kwa madhumuni ya kufikia mahitaji na malengo yao ya pamoja, ya kiuchumi, kijamii, na kitamaduni.
Kupitia vyama vya ushirika, wakulima wanaweza kuokoa pesa kutokana na gharama za usafiririshaji wa maziwa kibinafsi, kupata mikopo ya kununua ng’ombe zaidi na pembejeo. Ili mfugaji kupata faida hizi inamlazimu kujiunga pamoja na kuweka msingi thabiti wa kukuza ushirika.
Ni taasisi tofauti kisheria
Ushirika wa wafugaji unatambulika kisheria na inaweza kuingia katika makubaliano au mikataba na kampuni, mashiraka mengine na biashara zingine zinazotambulika pia kisheria kwa niamba ya wafugaji wanachama.
Hali hiyo inawaondolea wafugaji jukumu la kisheria linaloambatana na kuwa na biashara. Wakulima wanaweza weka nguvu zao kwenye uzalishaji wa maziwa zaidi na kuboresha shughuli zao shambani.
Inaendeshwa kwa kanuni za kibiashara
Madhumuni ya kuzalisha maziwa ni kupata faida, ingawa uzalishaji wa maziwa pia unachangia lishe bora na usalama wa chakula kwenye familia.
Ili kupata faida ya juu lazima ushirika uwe na mtazamo wa kibiashara na kuendeshwa kwa kanuni za biashara. Hii ni pamoja na kuweka rekodi za uzalishaji, mauzo na matumizi.
Faida inapopatikana, lazima ielezwe wazi ni kiasi kinapaswa kulipwa kwa wanachama kwa mgao na kiasi gani kinarudishwa kwa ushirika ili kupanua biashara.
Bila kumbukumbu, baadhi ya wanachama wanaweza kuhisi wamefanya kazi zaidi na wameachwa nje au kupata mgao kidogo wa faidia.
Utafiti umeonesha kuwa waanzilishi wengine wa vyama vya ushirika husahau kuwa ushirika ni mkubwa kuliko wao. Dhana hii huleta ugomvi, hudunisha usimamizi, kuharibu biashara na kufanya mapato kwenda chini.
Kuongeza thamani
Vyama vingi vya ushirika vinafanya biashara ya maziwa mabichi tu. Vinahitaji kupiga hatua nyingine na kuongeza thamani maziwa ili kuuza bidhaa tofauti-tofauti kutoka na maziwa.
Hii pia inapunguza hasara inayotokana na maziwa kuharibika haraka. Bidhaa za thamani za maziwa kama mala, mtindit, n.k. zinaweza kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika. Kuongeza thamani inaongeza mapato kwa mfugaji.
Kupokea huduma za ugani
Vyama vya ushirika vya maziwa vinajengwa kutokana na ng’ombe wanaozalisha maziwa.
Kwa mantiki hiyo, ng’ombe na maziwa vinafaa kushughulikiwa ipasavyo na kupewa umuhimu mkubwa. Utaalamu na ushauri nasaha kuhusu ufugaji na teknolojia ya maziwa lazima iletwe karibu na wafugaji. Vyama vya ushirika ni njia moja ya kuwafikia wakulima wengi kwa pamoja na moja kwa moja.
Vyama vya ushirika vya maziwa vinapoanguka moja ya sababu huwa ni upungufu wa maziwa kwa sababu ya magonjwa ya ng’ombe yanayoweza kuzuilika.
Vyama kama hivyo havitumii ushauri wa kitaalam wa mtaalamu wa afya ya mifugo. Changamoto nyingine ni ubora wa maziwa yanayokusanywa.
Kwa sababu ubora wa maziwa ni chapa ya ushirika, wanachama wanahakikisha kwamba wanadumisha usafi wa hali ya juu. Magonjwa kama Mastitis unaoambukiza kiwele na matiti ya ng’ombe unadunisha ubora wa maziwa. Tumia ushauri wa kitaalamu kuzuia magonjwa.
Vyama vya ushirika vile vinaweza kufanya kazi zifuatazo: –
- Kusanya maziwa kutoka kwa mashamba na vituo vya wafugaji.
- Kutengeneza bidhaa tofauti kulingana na mahitaji ya watumiaji.
- Uuzaji wa bidhaa zinazotokana na maziwa.
- Kuwapa wanachama huduma na bidhaa kama chakula cha ng’ombe, dawa, huduma za mifugo, n.k.
- Kuweka bei ili kudumisha kuongezeka kwa uzalishaji na matumizi.
- Kujadili na serikali juu ya masilahi ya wazalishaji ikiwa ni pamoja na kodi kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Afisa wa ushirika
- Vyama vya ushirika nchini Tanzania vinasimamiwa na sheria za ushirika, hasa Sheria ya Vyama vya Ushirika, Na. 6 ya 2013.
- Zungumza na afisa wa ushirika ugani katika eneo lako kuhusu uwezekano wa kuanzisha Ushirika wa wazalishaji wa maziwa.
- Chama cha ushiririka inahitaji idadi ya wanachama kati ya 20 hadi 30, ambao wamefikia umri wa chini wa miaka 18 na wenye akili timamu.
- Cha muhimu ni kuwa na mahitaji na malengo yanayoambatana nay a wanachama wengine, na ambayo ushirika unatafuta kukidhi.
- Ushirika unategemea maadili ya uhuru, yaani mwanachama anajiunga bila kushurutishwa, uwajibikaji wa kibinafsi, demokrasia, usawa, na mshikamano. Pia, wanachama wanaamini maadili ya uaminifu, uwazi, uwajibikaji wa kijamii, na kuwajali wengine.