Ili kuku waweze kuishi, kukua na kuleta matokeo chanya ni lazima wale chakula kingi chenye ubora unaotakiwa.
Uwingi na ubora wa chakula cha kuku ni lazima uzingatie makundi ya chakula ambazo ni, vyakula vya kutia nguvu, kujenga mwili, kuimarisha mifupa, kulinda mwili pamoja na maji.
- Vyakula vya kutia nguvu
Vyakula vya kutia nguvu vinaweza kuwekwa katika makundi matatu;
- Kundi la kwanza ni vyakula kama vile pumba za mahindi, pumba laini za mpunga na pumba laini za ngano.
- Kundi la pili linajumuisha vyakula vya nafaka kama vile mtama, chenga za mahindi, chenga za mchele, uwele na ulezi.
- Kundi la tatu lina vyakula vya mimea ya mizizi kama vile muhogo, viazi vitamu na magimbi.
Kabla ya kulisha kuku vyakula vya kundi la tatu, hakikisha miziz hiyo inalowekwa kwa muda wa saa moja au kupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ambayo kwa asili ipo katika vyakula vya aina hii.
Inashauriwa pia kuwa, miziz hiyo ilishwe kuku kwa kiwango cha asilimia 10% ya chakula chote anacholishwa kuku.
Katika kundi hili la kutia nguvu, vyakula vya mafuta kama vile kutoka kwenye vyakula kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki, husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini.
Vyakula vya kutia nishatia, huchangia asilimia 60% hadi 70% ya mchanganyiko wote wa chakula.
- Vyakula vya kujenga mwili
Katika kundi hili, kunapatikana vyakula vya aina mbalimbali kama ifuatavyo;
- Mashudu: Haya ni makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya, korosho na ufuta.
- Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa) hii inafanywa ili kuepuka uwezekano wa kuku kupata magonjwa ya kuambukizwa.
- Mabaki ya samaki, dagaa au nyama.
- Vyakula vya asilia kama vile minyoo, mayai ya mchwa, masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu waliooteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine.
Vyakula hivi huchangia asilimia 20% hadi 30% ya mchanganyiko wote wa chakula cha kuku.
- Vyakula vya kuimarisha mifupa
Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifua, maganda ya yai, kukua na kuuweka mwili wa kuku katika afya njema kwa ujumla.
Madini ya muhimu sana ni madini ya chokaa (kalsiamu) na fosiforasi.
Ili kuku watage mayai yenye ganda gumu ni lazima wapate madini ya chokaa, maganda ya konokono, na mayai yaliyosagwa vizuri.
Aidha, inapendekezwa kwamba, unapoongeza madini ya fosiforasi inakubidi uongeze pia madini ya chokaa kadri inavyotakiwa kwasababu kiwango cha madini cha aina moja kikizidi kingine husababisha upungufu wa kile kidogo.
Viini lishe vinavyohitajika kwenye madini
- Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa na maganda ya konokono wa baharini, konokono wan chi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa.
- Kabla maganda ya mayai na nyumba za konokono havijatumika inashauriwa yachomwe moto mkali au yachemshwe ili kuua vidudu vya maradhi.
- Chumvi ya jikoni na madini yaliyotengenezwa viwandani kama vile Di-calcium phosphate pamoja na magadi (kilambo).
- Vyakula vya kulinda mwili
Kundi hili linajumuisha vyakula vya mbogamboga kama vile;
- Mchicha, samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa, mchicha pori, chainizi, kabeji nakadhalika.
- Mchanganyiko wa madini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).
- Jua ni muhimu katika kuhakikisha vitamin A na D vinatumika vizuri mwilini kwa hiyo banda ni lazima lijengwe kwa mtindo ambao utaruhusu mwanga kupita hasa nyakati za asubuhi na jioni.
- Chakula cha kuku wanaofugwa ndani, ni lazima kichanganywe na vitamin vinavyotengenezwa kutoka viwandani.
Gharama za ulishaji kuku
Huduma ya chakula cha kuku huwa na gharama, na huweza kuchukua zaidi ya asilimia 80% ya gharama zote kwenye mradi wa ufogaji wa kuku.
Gharama hizi za ulishaji huweza kupunguzwa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kuhakikisha mchanganyiko wa chakula umehusisha makundi yote ya vyakula.
Pili, kuku walishwe kiwango tu cha chakula kinachotakiwa kulingana na umri wa kuku, pamoja na kutumia makapi au masalia ya mazao au vyakula vinavyopatikana kwenye eneo lako.
Tatu, mfugaji analazimika kuchunguza mwenendo wa afya wa kuku mara baada ya kutumia chakula kipya ikilinganishwa na chakula cha hapo awali.
Hii huonekana mapema kwani uzito wa kuku na ukuaji wake huonekana haraka sana ndani ya wiki moja mara baada tu ya kubadilisha chakula.
Ubora wa chakula cha kuku
Chakula cha kuku kinaweza kuwa chenye ubora unaohitajika lakini mfugaji akashindwa kupangilia namna ya kulisha kuku wake na hivyo akakosa matokeo mazuri.
Kuku wakipishana maumbo wakiwa chini ya umri wa wiki nane, wataendelea kupishana hadi umri wa kuzalisha mayai au nyama, hivyo ulishaji ujikite kwa lengo la kuku wote kufanana ukubwa na uzito.
Kuku wa mayai malezi yao huishia wiki ya 18 hadi ya 19 na kuingia sasa kwenye uzalishaji wa mayai.
Wakati huo kabla ya umri huo wa uzalishaji mayai, ni lazima mfugaji azingatie kuwa na vifaa vingi vya kutosha kiasi cha kuku wote walio bandani, wale na kushiba kwa pamoja bila kupishana.
Angalau asilimia 90 ya kuku wote waliopo bandani wakue kwa pamoja kwa mfanano wa ukubwa na uzito.
Kuku wakikua kwa mfanano mmoja huanza kutaga kwapamoja na kufikia kilele wakiwa na uwezo mkubwa sana wa kuzalisha na mfugaji kupata faida inayoendana na shughuli yake ya ufugaji.
Kuna shida kubwa sana katika malezi ya kuku hafifu
- Unapoweka vyombo vya kulishia kuku, chukua muda wako kuangalia kuku wakati wa kula kwani utaona baadhi ya kuku wakihangaika kutafuta sehemu ya kupenya kwa ajili ya kula.
Ukiona hivyo, ujue kuku ni wengi kuliko uwezo wa vyombo kuwahudumia ndiyo maana wanahangaika na kukosa sehemu ya kulia kutokana na wenzao kujaa kwenye vyombo vya kulia.
Kitendo hicho kitamsaidia mfugaji kujua kuwa anahitajika kuongeza vyombo kwa ajili ya kulishia hadi hapo atakapoona wanakula wote kwapamoja.
Mfugaji anatakiwa kuanza na mfumo huu tangu kuku wakiwa vifaranga na kuendelea kuongeza vyombo kadri wanavyokuwa hadi wanapoanza kutaga au kufikia umri wa kuwauza kama ni kuku wa nyama.
- Pia, vyombo vya maji viwekwe na maji yawepo bandani muda wote kwa kila baada ya kula kuku wanapenda kunywa maji.
Usafi wa vyombo vya maji ni wa muhimu sana kuzingatiwa kwani utasaidia kuepusha kuwepo kwa maambukizi ya magonjwa mbalimbali.
Vifaa au vyombo vyote vya maji vining’inizwe usawa wa migongo ya kuku ili kuepusha kumwaga chakula na maji wakati wa kula na kunywa.
- Mfugaji anatakiwa kutambua kuwa chaku na ulishaji ndiyo mradi wenyewe na ndiyo faida yake mfugaji.
Chakula na ulishaji vinaweza kumfanya mfugaji kuweza kuendelea na mradi na kufuga kwa faida au kushindwa kuendeleza mradi huo.
Ulishaji wa kuku kwa kutumia masalia ya mazao
Chakula cha kuku ni muhimu kuangaliwa kabla ya kununuliwa na kulisha.
Tunajua kwamba makapi na masalia ya vyakula vya binadamu ndivyo hutumika kwa wingi kwa chakula cha kulishia mifugo.
Makapi haya hupatikana kutokana na kupembua nafaka, kukoboa au kukamua mafuta. Katika uchakataji wa azao ili kuyafanya yafae kwa matumizi ya binadamu, kuyaongeza thamani na kurahisisha utunzani tunapata vyakula vya mifugo.
Mazao kama vile, alizeti, pamba, mawese, karanga na mengine, hukamuliwa na kutoa mafuta kupikia na kuacha makapi (mashudu) ambayo hutumika kwa ajili ya chakula cha mifugo.
Kwanini masalia ya mazao kwa kulishia
Makapi au masalia haya kwa kuku hutoa virutubisho aina ya protini ambayo hujenga mwili na kutoa kinga dhidi ya magonjwa.
Mazao kama vile mahindi, mpunga, ngano na mengine hukobolewa na kutoa pumba ambazo ni chakula cha wanga chenye kutoa nguvu ya kukua kwa kuku.
Kwa kiasi kikubwa, mifugo aina mbalimbali ikiwamo kuku hutegemea mabaki haya ambayo kwa binadamu hayana lishe ya kutosha au pengine huenguliwa kutokana na tumbo la binadamu kukosa kemikali za kusaga makapi haya.
Tumbo la binadamu siyo sawa na matumbo ya wanyama yenye uwezo mkubwa wa kusaga aina nyingi za mazao ghafi hivyo hupata fursa ya kuhakikisha kila kinachosalia kama makapi kinatumika kwa njia nyingine.
Masalia hayo ndiyo yanayotumika kulishia mifugo, na baadaye mifugo hiyo kumpatia vyakula vya aina mbalimbali ikiwamo nyama, maziwa na mayai.
Masalia hupunguza gharama kwa mfugaji
Chaguo la kutumia masalia au makapi kulishia kuku badala ya kutumia mazao halisi yanayoliwa na binadamu inatokana na unafuu wake wa kuyapata na kununua.
Mifugo pia ina uwezo mkubwa wa kubadilisha makapi au masalia hayo na kumpatia mfugaji nyama, maziwa na mayai.
Halikadhalika, kuepusha uhaba wa mazao ya chakula kwa binadamu na kuruhusu chenye thamani kubwa kitumike kwa ajili ya binadamu, huku chenye thamani ndogo kitumike kwa ajili ya mifugo.
Aidha, makapi au masalia hayohayo ambayo ni chakula cha mifugo, hutumika kama mbolea kwa kuozesha na kupeleka shambani, hivyo kusitawisha mimea.