- Mifugo

Nawezaje kutunza g’ombe na kukabilina na magonjwa

Sambaza chapisho hili

Bila matunzo mazuri na kuzingatia kanuni za ufugaji, mfugaji hawezi kupata faida na kufikia malengo yake. Shauriana na wataalamu unapoona kuna jambo linalokutatiza.

Ufugaji hasa wa ng’ombe wa maziwa ni shughuli ambayo imejipatia umaarufu kwa kiasi kikubwa sana katika jamii mbalimbali, maeneo ya vijijini na hata mijini. Pamoja na shughuli hii kuwa maarufu na yenye faida, kuna changamoto mbalimbali zinazoambatana na ufugaji. Ni muhimu kuzingatia kanuni na taratibu ili uweze kuepuka hasara.

Matunzo ya ng’ombe

Matunzo hutegemeana na aina ya ufugaji, pamoja na aina ya malisho wanayopatiwa. Ni muhimu sana kuzingatia ng’ombe kupata virutubisho stahili, ili waweze kujenga miili yao na kuzalisha inavyotakiwa. Hakikisha kuwa ng’ombe wanapata virutubisho na lishe muhimu ili waweze kujenga miili yao na kuzalisha sawa sawa.

Virutubisho

Kama ilivyo kwa binadamu, ng’ombe anahitaji kupata virutubisho pamoja na madini ya aina mbalimbali, na virutubisho hivyo viwe na uwiano kamili. Ni muhimu pia ng’ombe kupatiwa vyakula vyenye vitamini. Ng’ombe wanapolishwa virutubisho vya kutosha husaidia kutengeneza kinga ya mwili.

Usafi

Mazingira wanayofugwa na kuishi ng’ombe ni lazima yawe safi wakati wote. Hii itasaidia kuepusha magonjwa mbalimbali, mfano ugonjwa wa kiwele na matiti (Mastitis), minyoo. Si hayo tu lakini kwa ujumla usafi husaidia kuzuia aina zote za magonjwa.

Banda

Banda la kufugia ng’ombe ni lazima lijengwe kwa ustadi na kuhakikisha kuwa halituamishi maji, na lina hewa ya kutosha. Banda linapokuwa na unyevu husababisha ng’ombe kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.

Baadhi ya magonjwa yanayoshambulia ng’ombe

Ugonjwa wa kichomi (Pneumonia)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na baridi inayotokana na banda kuwa na unyevu na kutokuwa na hewa ya kutosha. Ugonjwa huu wa kichomi hushambulia zaidi wanyama wadogo.

Kinga: Wanyama wapaitiwe chanjo mara kw amara kulingana na aina ya magonjwa yanayotokea mara kwa mara katika eneo husika, hii itasaidia kuongeza kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa lengwa.

Ugonjwa wa miguu na midomo (FMD)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambao hushambulia ng’ombe na aina nyingine ya wanyama wenye kwato kwenye sehemu ya miguuni na mdomoni.

Virusi wanaosababisha ugonjwa huu wamegawanyika katika makundi saba. Hii hutegemeana na nchi, maeneo flani kulingana na hali ya hewa ya eneo husika. Ugonjwa huu wa miguu na midomo ni moja ya magonjwa ambayo yamekuwa yakisumbua sana hapa nchini Tanzania.

Kuenea: Ugonjwa huu huenezwa kwa njia kuu mbili. Njia ya kwanza ni wanyama kugusana. Wanyama kula chakula chenye wadudu

Ugonjwa huu huenea kwa haraka sana, hasa kwa wanyama walio kwenye banda moja.

Dalili

Ni rahisi sana kutambua dalili au kama mnyama ameathirika na ugonjwa huu, hii ni kwa sababu huwa na dalili zifuatazo

  • Mnyama hutoa povu na ute mdomoni
  • Ng’ombe anakuwa hali au anakuwa anakula kwa shida
  • Kuwa na malengelenge mdomoni
  • Kuwa na vidonda mdomoni
  • Miguu huwa na vidonda katikati ya kwato
  • Ng’ombe huchechemea wakati wa kutembea
  • Ng’ombe hupendelea kulala kwa sababu ya maumivu miguuni
  • Afya ya ng’ombe au mnyama alie athirika huzorota kwa sababu hula kwa shida hivyo kushindwa kula chakula kwa kiwango kinachotakiwa
  • Kiwango cha uzalishaji wa maziwa hupungua au kupotea kabisa hata baada ya kupona

 

Kutokana na ugoinjwa miguu na midomo, afya ya mnyama inakuwa dhaifu sana na ni vigumu kurudi katika hali yake ya kawaida hata baada ya kupona. Wanyama wadogo hufa kwa urahisi ukilinganisha na wanyama wakubwa wanaoshambuliwa na ugonjwa huu.

Chanjo: Inashauriwa  kuchanja mifugo kila mwaka dhidi ya ugonjwa huu. Hii itasaidia kuepuka hasara inayosababishwa na ugonjwa huu wa miguu na midomo

Tiba

  • Ili kuweza kuweza kukabiliana na ugonjwa huu, jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kuwatenga wanyama wenye ugonjwa mara tu baada ya kugundua (Karantini).
  • Baada ya kuwatenga mifugo, watibiwe kwa kutumia kiua vijisumu-antibiotics.
  • Safisha vidonda kwa kutumia dawa aina ya salvon na kuviweka katika hali ya usafi. Unaweza pia kuvipaka iodine.

*Zingatia kuwa chanjo na usafi ndiyo njia pekee itakayokuwezesha kuondokana na ugonjwa huu

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

1 maoni juu ya “Nawezaje kutunza g’ombe na kukabilina na magonjwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *