- Mifugo

Namna ya kutunza mifugo wakati wa msimu wa mvua

Sambaza chapisho hili

Ni ukweli usiopingika kwamba msimu wa mvua ni mzuri kwa ustawi wa mifugo. Hii ni kutokana na ongezeko la malisho kwa mifugo hasa kwa wafugaji wanaojishughulisha na ufugaji wa mifugo kama vile ng’ombe, kuku, sungura, mbuzi, kondoo, nguruwe, punda n.k.

Msimu wa mvua kwa wafugaji huambatana na changamoto zisizo rafiki kwa maisha ya mifugo. Hii ni pamoja na magonjwa na wadudu wasumbufu, kama kupe.  Pia mazingira mengine ya malisho kutofikika kutokana na athari za mvua zinazopelekea kuwepo matope, makorongo.

Kwa kipinidi hiki chote wafugaji wasipokuwa makini na kujibidiisha kuzingatia utunzaji bora wa afya za mifugo wataishia kupata hasara kubwa.

Mwanzo wa msimu wa mvua, nyasi huota kwa wingi na kipindi hiki mifugo hupendelea kula majani hayo machanga ambayo kimsingi yanakuwa ni laini na rahisi kwa mifugo kula mengi. Majani haya machanga yanakuwa yamejaa maji kwa sehemu kubwa wakati uhitaji wa mifugo kama ngombe ni majani yaliyokomaa na kuwa na kiwango kikubwa cha nyuzi nyuzi (fibre content).

Majani hayo yanaweza kusababisha mifugo jamii ya ngombe, mbuzi au kondoo tatizo la kuarisha kwasababu ya ulaini wa majani hayo na mengine yakiwa machanga yanakuwa na kiwango kikubwa cha sumu. Hivyo inaweza kuathiri mifugo ndiyo maana inashauriwa majani yatumike baada ya kufikia katika hatua ya kuchanua maua.

Baadhi ya changamoto ambazo mfugaji anaweza kukutana nazo katika msimu wa mvua:

  1. Kupe: hawa ni moja ya wadudu ambao ni tishio kubwa kwa afya na uzalishaji wa mifugo. Kupe wakiwa wengi wananyonya damu ya mifugo na kudhoofisha afya lakini vile vile kupe hueneza magonjwa kwa mifugo kama vile ndigana kali (ECF), ndigana baridi (anaplasmosis), kukojoa damu (babesiosis) nakadharika.
  2. Msimu wa mvua mifugo wakubwa kama ngombe, nguruwe, kondoo, mbuzi hupata changamoto ya ugonjwa wa kuoza kwato (foot rot diseases)
  3. Inzi: Msimu wa mvua inzi huzaliana sana na hivyo kusababisha usumbufu na kueneza magonjwa kwa mifugo. Katika kundi hili la inzi wapo inzi wabaya kama vile ndorobo (tsetse fly) ambao siyo tu kwamba wanawasumbua mifugo bali ung’ataji wake uambatana na maumivu makali sana na vilevile ueneza ugonjwa ujulikanao kama ndorobo nagana (Trypanosomiasis). Pia magonjwa ya macho utokea zaidi katika msimu huu wa mvua.
  4. Minyoo kuzaliana kwa wingi; Ikumbukwe kwamba minyoo isipodhibitiwa vizuri huathiri afya na uzalishaji wa mifugo kwa ujumla wake. Wafugaji ni vema kipindi hiki cha mvua kutumia dawa za minyoo zenye nguvu ya kupambana na minyoo zaidi ya aina moja.
  5. Magonjwa yaenezwayo kwa sababu ya uchafu kama kuharisha damu (coccidiosis) homa ya matumbo (typhoid or salmonellosis) ni rahisi kutokea kwa mifugo karibu wote na haswa jamii ya ndege katika kipindi cha mvua
  6. Panapokuwa na kiwango kikubwa cha unyevu husaidia katika vimelea wa magonjwa kama bakteria, fangasi, na protozoa kuzaana kwa wingi na hivyo kusababisha magonjwa
  7. Ugonjwa wa kiwele (mastitis): Ugonjwa wa kiwele kwa mifugo wa maziwa unaweza kutokea wakati wowote. Kisababishi cha ugonjwa huu kipindi cha mvua ni mazingira machafu ambayo huruhusu uzalianaji wa bakteria. Dalili za ugonjwa huu ni kuvimba kiwele, kiwele kuwa na joto kali, kiwele kuwa na maumivu kikiguswa, kushindwa kutoa maziwa na kutoa maziwa yaliyoganda au kuwa maji au kuwa na mchanganyiko wa damu.
  8. Kuoza kwa chakula: Chakula cha mifugo ambacho kimekuwa kwenye mazingira yenye unyevu mwingi huanza kuoza mapema na kuwa na utando mweusi au wa kijivu (mouldy) chakula cha hali hii hubeba bakteria na visababishi vya magonjwa vingine; hakikisha kwamba chakula cha mifugo kimehifadhiwa sehemu kavu na salama.

Nini kifanyike;

Kuzingatia usafi kwa ujumla wake

Mfugaji akizingatia usafi huepuka kwa kiasi kikubwa madhara ya magonjwa yanayoweza kuwapata wanyama. Uchafu unaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa au kuwa chanzo na mazalia ya wadudu mbalimbali kama vile inzi, kupe, viroboto, utitiri, chawa na minyoo.  Wakati wa msimu wa mvua, mazingira yasipokuwa safi husababisha mazalia ya wadudu kama konokono ambao husaidia kuenea kwa minyoo wa kwenye ini, mazingira. Mifugo wote wanahitaji usafi wa vyakula, maji, mazingira na vifaa vyote.

Kuzingatia chanjo

Chanjo ni moja wapo ya njia muhimu katika kukabiliana na magonjwa kwa nyakati zote, ni muhimu kwa mfugaji kuzingatia ratiba chanjo kwa mifugo. Zaidi ni muhimu kwa mfugaji mwenyewe kukuza uelewa wa chanjo zinazohitajika kwa mifugo yake na kuweka ratiba.

 

Zingatia lishe

Kuna baadhi ya magonjwa hutokea kama matokeo ya lishe duni kwa mifugo. Mfugaji ni lazima kuhakikisha kwamba mifugo wanapatiwa lishe bora ambayo itawezesha mwili kujilinda dhidi ya magonjwa. Lishe bora ni muhimu ili kuwapatia mifugo wako wanga, madini, vitamini, protini na maji.

Kudhibiti visababishi vya magonjwa

Wafugaji wanapaswa kuelewa njia sahihi za kudhibiti kuenea kwa wadudu wasababishi wa magonjwa hususani kwa kipindi cha mvua. Wafugaji wanapaswa kuzingatia njia zote za udhibiti zinazosababisha kuenea kwa magonjwa kama vile (i) kuzuia kuzagaa kwa mizoga na kuzika kwa ufasihi (ii) kuzuia mazalia ya wadudu kwa kusafisha banda kila wakati na kuepuka mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa wadudu (iii) kuzuia uchafuzi wa mazingira (iv) kudhibiti wadudu hatarishi kama kupe, minyoo nakadhalika (v) kutenga wanyama wagonjwa.

Kuepeuka mazingira hatarishi

Epuka mazingira yafuatayo: maeneo ambayo yanatuamisha maji kwa muda mrefu. Epuka muingiliano na wanyama pori kwasababu wengi wao wanauwezo wa kuhimili magonjwa kuliko mifugo. Mifugo inapaswa kukaa katika mazingira masafi na chakula kihifadhiwe  katika sehemu safi na kavu.

Muhimu: Hata katika kipindi cha kiangazi magonjwa hutokea kwa mifugo kutokana na uhalisia wa kisababishi cha ugonjwa kumudu aina fulani ya hali ya hewa. Hivyo tunawashauri wafugaji wakati wote kuwa makini katika kuweka mkazo madhubuti katika ufugaji wao.

Kwa mfano; mfugaji wa kuku anayemaanisha katika ufugaji ni lazima atazingatia usafi (hapa ataweza kupunguza hasara kwa sababu magonjwa mengi ya kuku huenezwa kwa uchafu), pia atazingatia chanjo; kwa yale magonjwa yenye chanjo, lishe bora kulingana na aina ya kuku anaowafuga).

 

Makala hii imeandaliwa na Eliud Mathayo Letungaa kutoka MVIWAA anayepatikana kwa simu namba +255754438136

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *