Majani ya matete ni moja ya zao maarufu kwa lishe ya mifugo Afrika mashariki. Hata hivyo, wafugaji wengi wamekuwa wakilipuuzia huku wakikosesha huduma muhimu zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji mzuri. Moja ya tatizo kubwa katika uzalishaji wa maziwa ni kukosekana kwa malisho sahihi na ya kutosha kwa ajili ya mifugo ili kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato, hasa wakati wa kiangazi.
Pamoja na wafugaji wengi kuwa na ardhi ya kutosha ambayo wanaweza kuzalishia malisho mazuri na yakutosha bado utunzaji wa malisho hayo ni hafifu na ni vigumu kuendeleza mifugo yao. Utunzaji mzuri wa malisho humhakikishia mfugaji kuwa na lishe ya kutosha kwa ajili ya mifugo yake katika kipindi chote cha mwaka.
Moja ya zao la lishe ni majani ya matete. Majani ya matete hutoa mavuno mengi ukilinganisha na aina nyingine zote za lishe ya mifugo. Wafugaji hawapati faida ya zao hili kutokana na kutokupenda kufanya matunzo kwa njia sahihi.
Matete yanahitaji virutubisho
Ili kuongeza uzalishaji wa majani ya matete, ni muhimu kuongeza kiasi cha mbolea ya samadi iliyoiva katika ardhi ambayo majani haya yataoteshwa. Weka kiasi cha tani 5 hadi 10 za mbolea ya samadi katika shamba kwa ajili ya kupanda. Kwa miaka ya mbeleni, weka kiasi hicho hicho kila baada ya mavuno.
Ni wafugaji wachache sana ambao huweka mbolea ya samadi katika shamba la majani ya matete. Njia nzuri ya kuongeza mavuno ni pamoja na kuchanganya matete na jamii ya kunde kama desmodium. Hii husaidia kuboresha malisho pamoja na kupunguza gharama za ununuzi wa mbolea ya Nitrojeni.
Mbinu za kupanda Tumbukiza: Ni mbinu mpya ya kupanda majani ya matete. Gharama za awali zinazotumika kwa ajili ya kuchimba mashimo na mitaro ni ya juu kidogo kuliko njia ya kawaida, lakini Tumbukiza hutoa mavuno mengi kuliko njia iliyozoeleka na pia haitumii eneo kubwa kwa malisho ya ng’ombe mmoja.
Kupanda kawaida: Matete yanaweza kupandwa kawaida kwa kuchimba mashimo na kuweka mapandikizi. Ni muhimu kupanda matete kwa mstari na kwa nafasi ili kuweza kupata malisho kwa kiasi kikubwa na kuruhusu machipukizi mapya.
Palizi
Hiki ni kipengele muhimu katika utunzaji wa matete. Hii ni kwa sababu magugu hunyonya madini pamoja na maji ambayo yalitakiwa kutumika kama lishe ya majani hivyo kusababisha kupungua kwa uzalishaji. Palizi ni lazima ifanyike kila baada ya mavuno ili kuongeza uzalishaji mkubwa na wenye tija.
Wafugaji wenye malisho kidogo hulazimika kukata majani machanga mara kwa mara kwa ajili ya kulisha mifugo yao bila kujua kuwa majani machanga ya matete siyo mazuri kwa ajili ya kulishia mifugo kwani yana maji mengi na kiasi kidogo sana cha madini.
Majani ya matete yanatakiwa kuvunwa yanapokuwa na urefu wa mita 1 au kila baada ya wiki 6 hadi 8 ili kupata majani yenye ubora pamoja na mavuno mengi. Hakikisha unabakiza bua urefu wa sentimita 5 hadi 10 kutoka usawa wa ardhi katika kila mavuno ili kuzuia kudhoofika kwa mfumo wa mizizi na kusababisha kupata mavuno hafifu katika mavuno yajayo.
Kulisha mifugo
Wafugaji wengi wadogo hufuga wanyama wengi bila kuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya malisho. Ng’ombe mmoja anayetakiwa kuzalisha maziwa kiasi cha kilo 7 anatahitajika kula wastani wa kilo 70 za majani ya matete. Kwa ng’ombe anayepata lishe ya mchanganyiko wa majani ya matete na majani jamii ya kunde atazalisha kuanzia kilo 9 hadi 12.
Ekari moja ya majani ya matete hutosheleza kulisha ng’ombe mmoja tu kama hakuna malisho ya aina nyingine yanayofanyika. Ekari moja ya majani ya matete kwa mbinu ya tumbukiza inaweza kutosheleza kulisha ng’ombe 2 hadi 3 kwa mwaka mmoja.
Matete huzuia mmomonyoko wa udongo na wadudu
Majani ya matete yana faida nyingi kwa mkulima. Endapo yataoteshwa kuzunguka shamba la mahindi itasaidia kuzuia katapila wanaovamia zao la mahindi au mtama. Wakulima wanashauriwa kuotesha mistari mitatu ya majani ya matete kuzunguka shamba lote la mahindi.
Matete yanapooteshwa pamoja na mchanganyiko wa majani jamii ya kunde katika makingo ya maji, matete husaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo.